Header Ads

LIYUMBA ATUMIA HOJA YA YESU KUTOA UTETEZI


*ASEMA SERIKALI HAIJUI ITENDALO KWA KESI YAKE
*HUKUMU YAKE KUTOLEWA MEI 24
*AMTUPIA MZIGO MAREHEMU BALLALI

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba (62), ambaye sasa anakabiliwa na shtaka moja la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma, amedai serikali haijui itendalo dhidi ya kesi iliyomfungulia.


Liyumba ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, izingatie ukweli wakati wa kutoa hukumu dhidi yake Mei 24 badala ya kuwasikiliza watu wasiojua watendalo.

Maneno hayo mawili ‘hawajui watendalo’ yanafanana na yale aliyotumia Yesu Kristo, anayeaminika kuwa ni Mwokozi wa waumini wa Kikristo wakati akieleza kitendo cha Wayahudi waliokuwa wakimsulubisha (Luka 23:34).

Mshtakiwa huyo jana alipanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kutoa utetezi wake mbele ya Kiongozi wa Jopo la Mahakimu Wakazi, Edson Mkasimongwa, aliyekuwa akisaidiwa na Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa.

Kesi hiyo ambayo imevuta hisia za watu wengi ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam ilifikishwa mahakamani hapo Januari 26 mwaka jana ambapo Liyumba alikuwa akikabiliwa na makosa mawili ambayo ni matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia hasara serikali ya sh bilioni 221.

Hata hivyo Aprili 9 mwaka huu, mahakama hiyo ilimfutia shtaka la kuisababishia hasara serikali baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha hasara kwa namba kama ilivyokuwa ikitakiwa.

Liyumba, aliongozwa kutoa ushahidi wake na wakili mahiri wa kujitegemea Majura Magafu aliyekuwa akisaidiwa na Jaji Mstaafu Hillary Mkate, Onesmo Kyauke na Hudson Ndusyepo huku upande wa mashitaka ulikuwa ukiongozwa na mawakili waandamizi Juma Mzarau, Ben Lincoln na Tabu Mzee.

Mstahakiwa huyo, alianza kujitetea saa tano asubuhi hadi saa saba mchana mbele ya umati wa watu uliofurika ndani ya mahakama hiyo na kusababisha watu wengine kusimama nje ya ukumbi wa mahakama, alidai kuwa anaiomba mahakama kuzingatia ukweli katika kuandika hukumu yake.

Amedai kuwa ameamua kutoa tahadhari hiyo kwa sababu upande wa mashitaka umewasilisha vielelezo ambavyo baadhi yake ni barua alizozisaini zilikuwa zinatoa maelekezo kwa kampuni ya ujenzi wa mradi wa Ten Mirambo Extention “Minara Pacha” ya Design&Service wakati kuna barua nyingine zilisainiwa na wasaidizi kwa niaba yake, na barua za kampuni ya Design&Service zilizokuwa zikiandikia BoT, hazikuletwa mahakamani hapo kwa makusudi.

“Waheshimiwa naomba sana mzingatie ukweli kabla ya kufikia kutoa hukumu dhidi yangu, kwani upande wa mashitaka umeleta barua hizo tu kwa sababu zimesainiwa na Liyumba, kama upande wa mashitaka unatenda haki ni kwa nini ulishindwa kuleta barua zilizosainiwa na wasaidizi wangu kwa niaba yangu ambao nao walikuwa wakitoa maelekezo mazito tu kuhusu mradi huo?

“Na kama kweli walikuwa wanatenda haki ni kwa nini wameshindwa kuleta zile barua ambazo kampuni ya ujenzi ilikuwa ikiiandikia BoT na mimi kwa kuwa niliteuliwa na Gavana (Marehemu Balali) kushughulika na masuala ya uongozi katika mradi huo, nilikuwa nazijibu baada ya kupata idhini ya gavana.

“Kwa faida ya waendesha mashitaka mimi nilikuwa nikijibu barua za Design&Service na barua hizo nilizosaini zimeonyesha wazi nilikuwa najibu barua hizo kwa kutumia kumbukumbu mbalimbali za barua zilizokuwa zinatoka nje kuja BoT...narudia tena kama hawa waendesha mashitaka walikuwa wanatenda haki wangeleta nyaraka hizo zote nilizozitaja.

Kwa sababu wanazozijua wao walipoona tu barua hizo zinasaini yangu wakazichomoa kwenye jalada ambalo linahifadhiwa kwenye ofisi ya Meneja wa Mradi na kuzileta mahakamani,” alidai Liyumba na kusababisha watu kuangua vicheko na wakili mwandamizi wa serikali Juma Mzarau ambaye alikuwa akimhoji kujiinamia na kisha kucheka.

Liyumba ambaye ni mchumi kitaaluma, aliiambia mahakama kuwa katika kipindi cha mwaka 2001-2006 alikuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa BoT na alistaafu kwa mujibu wa sheria Desemba 2008. Majukumu yake akiwa na wadhifa huo alikuwa akishughulika na shughuli zote zinazohusu uendeshaji wa benki.

Alieleza kuwa kiongozi wake wa kazi alikuwa Naibu Gavana huku nafasi ya Gavana ilikuwa ikishikiliwa na Daudi Balali na alikuwa akiwajibika kwake lakini kama hakuwepo alikuwa akiwajibika kwa naibu wake.

Alidai anaufahamu mradi wa ujenzi wa Minara Pacha kwani wakati anahamishiwa Makao Makuu ya BoT Dar es Salaaam, akitokea mkoani Mwanza alikuta mradi huo upo kwenye mchakato na ilikuwa mwaka 2000 na ujenzi wa mradi huo ulianza rasmi mwaka 2002.

Liyumba ambaye anamiliki hoteli moja na kampuni moja ya kutoa mikopo midogo midogo , alidai kuwa kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na benki hiyo, mradi ulikuwa chini ya kurugenzi aliyokuwa akiiongoza yeye ila kulikuwa na kitengo kinachojitegemea chini ya Meneja Mradi Deogratius Kweka na meneja huyo alikuwa anapeleka taarifa za mradi huo moja kwa moja kwa gavana.

“Huyo meneja mradi hakuwa mwajiriwa wa kudumu wa BoT bali alikuwa na ajira ya mkataba ambayo aliipata kutokana na kuanzishwa kwa mradi huo. Mimi nilikuwa nahusika kiutendaji kwa sababu Kweka hakuwa mwajiriwa wa kudumu wa BoT, na kwa kuwa hakuwa na ajira ya kudumu meneja huyo hakuwa na mamlaka ya kusaini barua za BoT kwenda kwa kampuni ya Design&Service.

“Mimi ndiye niliyeteuliwa na Gavana kuwa nasaini barua mbalimbali kwa niaba ya BoT zilizokuwa zikihusu mradi huo na kama mimi sipo alikuwa akizisaini msaidizi wangu na kumbukumbu zipo...kama Kweka angekuwa amepewa dhamana ya saini barua hizo za mradi wala mimi nisingeweza kusaini,” alidai Liyumba.

Huku akionyesha kujiamini, Liyumba alieleza utaratibu wa barua zilizokuwa zikienda BoT na zile zilizokuwa zikielekezwa kwake, barua zote zilizokuwa zikihusu mradi, zilifikia kwa gavana na yeye huzipeleka kwa Meneja Mradi na meneja huyo anatoa ushauri wa kitaaluma.

“Gavana, alikuwa akitoa maelekezo kwangu ya jinsi ya kuzijibu barua hizo ambazo mimi nilikuwa naweka saini yangu, ushauri wote wa ujenzi wa mradi ule Meneja Mradi alikuwa anautoa kwa gavana kwa sababu wafanyakazi wa Benki hawakuwa mainjinia,” alieleza.

Alifafanua kwamba watu wanapoizungumzia Menejimenti ya Benki Kuu, watambue kwamba menejimenti hiyo ni Gavana; hayo yametamkwa wazi kwenye Sheria ya Benki Kuu na kuongeza kuwa Jamhuri kudai yeye aliidhinisha mabadiliko ya ujenzi wa mradi huo bila idhini ya bodi ‘haijui itendalo’.

Alidai kwamba yeye na bodi ya wakurugenzi hawafanyi kazi kama inavyodaiwa kwa sababu haimhusu na wala haikumteua kuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala huku akisisitiza kuwa yeye alihusika katika mradi huo kwa shughuli za kiutawala tu.

“Aliyekuwa na jukumu la kupeleka chochote kilichohitajika kwenye mradi ni Meneja Mradi kwani ndiye aliyekuwa anaandaa taarifa za mradi kwa gavana, ndiye alikuwa anazipeleka taarifa hizo kwenye bodi.

Mapendekezo ya ushauri mabadiliko ya mradi yalikuwa kamati ya mradi na ilijadili na kuwahusisha washauri kutoka kampuni tatu ambazo zilikuwa zinatoa ushauri wa ujenzi huku malipo ya kazi yao yalikuwa yakilipwa na BoT.

“Baada ya gavana kupelekewa ushauri huo, kama akitaka kufanya mabadiliko ya ujenzi alikuwa anamuelekeza Meneja Mradi ambayo hurudi kuiarifu kamati na hatimaye hufikisha kile kilichoamuliwa kwa gavana.

“Mwisho kabisa naiomba mahakama hii tukufu wakati inaandaa hukumu dhidi yangu izingatie ukweli na iniachilie huru kwani hilo shitaka ambalo Jamhuri inadai nimetenda ...sioni kama linanihusu mimi kwani sijatenda kosa hilo na kwa kunishitaki Jamhuri imeonyesha haijui ilitendalo,” alidai Liyumba na kusababisha watu kuangua vicheko.

Naye aliyekuwa Kaimu Katibu wa Benki Kuu na Katibu wa Bodi ya Benki hiyo ambaye ni mwanasheria kitaaluma, Bosco Kimela (52), aliieleza mahakama kuwa shitaka linalomkabili Liyumba hastahili kushtakiwa nalo kwani hajalitenda.

Kimela ambaye anakabiliwa na kesi moja ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma na mbili za EPA na anaendelea kusota rumande kwa ajili ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, aliiambia mahakama pamoja na aliyekuwa na wadhifa huo pia alikuwa na wadhifa wa kuandaa vikao mbalimbali vya benki ambavyo gavana alikuwa anaviitisha.

Alidai taarifa za kitaalamu za mradi huo zilikuwa zinaandaliwa na Meneja Mradi na kuhusu mradi huo Liyumba hakuhusika kwa namna yoyote kutoa maamuzi yake binafsi kwani gavana alikuwa akimpatia orodha ya majina kabla ya kikao kufanyika na yeye alikuwa akiiandaa barua za mialiko na ya kuwaita wajumbe.

‘Kwenye vikao Gavana alikuwa akiwasilisha taarifa mbalimbali zinazohusu benki na Meneja Mradi, Deogratius Kweka, aliyekuwa akiwasilisha taarifa zinazohusu mradi huo na tangu mwaka 1992 hadi 2008 nikiwa na nyadhifa hizo sijawahi kushuhudia Liyumba akifanya maamuzi bila idhini ya Gavana, hilo halijawahi kutokea...mimi ndiye nilikuwa naandaa taarifa za vikao, ajenda, yatokanayo na mkutano, utekelezaji wa yaliyoamuliwa na kikao na nikishaandaa napeleka kwa Gavana na si vinginevyo.”

Baada ya kutoa maelezo hayo Wakili wa serikali Juma Mzarau aliiomba mahakama ipokee maelezo ya onyo ya Bosco kama kielelezo lakini ombi hilo lilipingwa vikali na wakili wa utetezi kwa madai kwamba shahidi huyo si wa upande wa mashitaka na kama jamhuri ilimuona shahidi huyo ni muhimu kwao isingemuondoa kwenye orodha yake ya ushahidi na kwamba upande wa mashitaka haujatoa sababu za kutaka mahakama hiyo ifute ushahidi ulitolewa jana na Bosco.

Akitoa uamuzi kuhusu ombi hilo la upande wa mashtaka, Hakimu Mkazi Mwandamizi Benedict Mwingwa alisema jopo hilo linatupilia mbali kwa sababu upande huo umeshindwa kutaja sababu za kukutaka ushahidi wa Bosco mahakama hiyo ikatae na kuamuru Bosco apande tena kizimbani kwa mara nyingine ili aendelee kutoa ushahidi wake.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, wakili Magafu aliiambia mahakama kuwa walikuwa wamekusudia kuleta mashahidi wanne, lakini kutokana na mashahidi hao wawili waliomaliza kutoa ushahidi wao jana, wameona ushahidi huo unakidhi haja hivyo wamefikia uamuzi wa kufunga kesi yao.

Aidha, Hakimu Mkazi Edson Mkasimongwa alisema mahakama imekubali ombi hilo la kufunga kesi kwa upande wa utetezi, na akazitaka pande zote katika kesi hiyo kuwa Mei saba , zilete majumuisho ya mchanganuo wa ushahidi ulitolewa jana, Mei 21 kesi hiyo itakuja kwa ajili ya kutajwa na Mei 24, mahakama hiyo ndiyo itatoa hukumu ya kesi hiyo.

Januari 26, mwaka jana, Liyumba na Meneja Mradi wa Benki Kuu, Deogratius Kweka, walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kusomewa mashitaka hayo ya kuidhinisha mradi wa majengo ya minara pacha bila idhini ya bodi ya wakurugenzi na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Mei 27 mwaka jana, mahakama hiyo iliwafutia kesi, lakini muda mfupi baada ya kuachiliwa walikamatwa tena mahakamani hapo na Mei 28 mwaka jana, Liyumba peke yake ndiye aliyerudishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka hayo na Kweka akawa ameachiliwa huru. Tangu kipindi hicho hadi sasa Liyumba anaendelea kusota rumande, baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, ambapo mahakama ilimtaka atoe fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya sh bilioni 110.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Aprili 23 mwaka 2010


2 comments:

Anonymous said...

I selԁom leave a гespοnse, but i diԁ а feω searchіng and wound up herе "LIYUMBA ATUMIA HOJA YA YESU KUTOA UTETEZI".
And I do hаve a cοuρle of quеstions for
you if you usually do not mіnd. Could іt bе just me oг ԁoes іt look lіke a few οf these comments look likе thеy aгe lеft by
braіn dead indiviԁualѕ? :-P And,
if yοu are pоѕting at additional online social
sitеs, Ι would like to keep up wіth everything fresh you have
to post. Coulԁ you maκe a list of every one of all your communal sites like your
Facebooκ page, twіtter feed, or linkeԁin profile?



Heгe is my ωeblog - premature ejaculation pills

Anonymous said...

Informative article, exactly what I needed.

my site: cheap legal highs

Powered by Blogger.