Header Ads

31 WAACHIWA 'KESI YA SAMAKI WA MAGUFULI"

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imewaachilia huru raia wa kigeni 31 kati ya 36 waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uvuvi haramu bila leseni maarufu kama “kesi ya samaki wa Magufuli”katika ukanda wa Tanzania, baada ya kuwaona hanawana kesi ya kujibu.


Sambamba na hilo,mahakama hiyo imemwamuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na taasisi nyingine za serikali kuandaa haraka iwezekanavyo utaratibu wa usafiri ambao ni salama wa kuwarejesha katika nchi zao raia 31 wa kigeni iliyowaachilia huru ili waweze kwenda kuungana na familia zao.

Wakili wa Serikali waandamizi Biswalo Mganga na Prosper Mwangamila waliikumbusha kuwa kesi hiyo ilikuja kwaajili ya mahakama hiyo kutoa uamuzi wa ama washtakiwa hao ambao wanatetewa na wakili wa kujitegemea Ibrahim Bendera na John Mapinduzi ama wana kesi ya kujibu au la.

Jaji Agustino Mwarija ambaye alisoma uamuzi huo kwa saa mbili, alisema baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi 13 wa upande wa ujamhuri, vielelezo kadhaa,hoja za mawakili wa pande zote mbili, mahakama hiyo imefikia uamuzi wa kuwaona washtakiwa watano yaani mshtakiwa 1,7,9,33 na 34 kati ya 36 ndiyo wana kesi ya kujibu na washtakiwa 31 hawana kesi ya kujibu.

Jaji Mwarija aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Nahodha wa meli hiyo ya Tawariq 1 ambayo ilikuwa ikivua bila leseni na kuaribu mazingira ya ukanda wa Tanzania, Hsu Chin Tai,mawakala wawili wa meli hiyo ya Tawariq 1, Zhao Hanguing,Hsu Shang Pao na mainjinia wawili Ca’ Dong Li na Chen Rui Hai.

Jaji huyo alisema anakubaliana na hoja moja ya mawakili wa utetezi kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja uliotolewa na upande wa Jamhuri kwamba washtakiwa wote walikuwa wakivua samaki katika ukanda huyo, ambapo alisema anakubaliana na hoja huyo kwamba upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha kuwa washtakiwa wote walikuwa wakifanya shughuli za uvuvi kwani baadhi ya washtakiwa wengi walikuwa ni wapishi, wafagizi hivyo makosa ya uvuvi haramu wanayodaiwa kutenda, hayawahusu.

“Kwa kuwa upande wa Jamhuri umelete kielelezo cha leseni inayoonyesha kutumiwa na meli ya Tawariq 2 ambayo shahidi mmoja aliambia mahakama kuwa leseni hiyo ilikutwa kwa mshtakiwa wa kwanza ambaye alimweleza mpelelezi wa kesi hii kuwa meli ya Tawariq 1 ilikuwa ikitumia kibali cha Tawariq 2…hivyo mahakama hii inaona anayepaswa kuzungumzia suala hilo la leseni ni nahodha wa meli, mawakala wa meli na mainjinia siyo wapishi, wahudumu wa meli hiyo.

“Hata hivyo nakubaliana na upande wa jamhuri kuwa ushahidi waliouleta umeweza kuwagusa washtakiwa hao watano …na ndiyo maana mahakama hii imefikia uamuzi wa kuwaona washtakiwa hao yaani mainjinia, mawakala wa meli na nahodha kuwa wana kesi ya kesi ya kujibu na inawaachiria huru washtakiwa wengine ambao ni wapishi, wahudumu wa meli hiyo kwani ni wazi kabisa mpishi, mhudumu wa meli hawezi kufahamu masuala ya leseni na kibali cha meli husika…mwenye jukumu la kujua hilo ni nahodha …hivyo kuanzia sasa washtakiwa 31 nawaachiria huru baada ya kuwaona hana kesi ya kujibu”alisema Jaji Mwarija na kusababisha raia hao wa kigeni kulipuka kwa furaha na wengine kuangua vilio.

Jaji Mwarija alisema kutokana uamuzi wake wa kuona washtakiwa hao watano wana kesi ya kujibu, watapaswa wapande kizimbani kujitetea na akasema wataanza kujitetea katika kikao kingine cha Mahakama ambapo uongozi wa mahakama utapanga tarehe rasmi ya kesi hiyo kuendelea na mahakama itazijulisha pande zote kwa njia ya maandishi tarehe hiyo ambayo itakuwa imepangwa.

Aidha Jaji Mwarija alikubaliana na ombi la wakili wa utetezi John Mapinduzi lilioiomba mahakama hiyo itoe amri kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ya kuandaa usafiri wa kuwasafirisha raia 31 wa kigeni chini na jaji huyo alitoa amri hiyo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ashilikiane na idara nyingine za seriakali kuwarudishi hati za kusafiria raia hao walioachiwa huru na kisha waandalie utaratibu wa usafiri salama ambao utawafikisha katika nchi zao.

Mabalozi , maofisa ubalozi wa balozi mbalimbali walifika mahakamani hapo kwaajili ya kusikiliza uamuzi huo ambao muda mfupi baada ya jaji Mwarija kumaliza kusoma uamuzi huo walionekana kupeana mikono ya pongezi na kufurahi na raia hao na sekunde chache baadaye Tanzania Daima liliwashuhudia makachero toka Kituo cha Kikuu cha Polisi Kati, wakiingia moja kwa moja ndani ya ukumbi namba moja ambapo kesi hiyo ilikuwa ikiendeshwa na kuwachukua raia hao 31 waliochiwa huru na kisha kuondoka nao na washtakiwa watano ambao walikutwa na kesi ya kujibu waliendelea kubakia mikononi mwa maofisa wa Jeshi la Magereza.

Itakumbuka kuwa Februali 25 mwaka huu, jaji wa awali aliyekuwa akisiliza kesi Razia Sheikhe alitoa uamuzi wa kuwanyima dhamana washtakiwa hao na kusema makosa yanayowakabili washtakiwa yanadhamana ila kutokana na mazingira ya kesi hiyo mahakama hiyo imetumia mamlaka yake kuwanyima dhamana.

Uamuzi ambao ulipingwa vikali na mawakili wa wastakiwa Bendera na Mapinduzi ambapo walimwomba jaji huyo ajitoe kusikiliza kesi hiyo kwasababu hawana imani naye hali iliyosababisha Machi 3 mwaka huu, Jaji Sheikh kutangaza uamuzi wa kujitoa katika kesi hiyo hali iliyosababisha uongozi wa mahakama hiyo siku chache kumpanga jaji mpya ambaye ni Mwarija kuendelea kusikiliza kesi hiyo.

Machi 8 mwaka 2009 washtakiwa hao walikamatwa na askari wa doria wakiwa kwenye meli ya Tawariq 1 na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kisha Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashtaka matatu ya uvuvi katika kina kirefu katika Ukanda wa bahari ya Tanzania,kufanya shughuli za uvuvi bila leseni na kuaribu mazingira ya ukanda huo.Tangu wakamatwe washtakiwa hao walikuwa wakiishi magerezani.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Julai 15 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.