MAHANGA ATAKA KESI YA MPENDAZOE IFUTWE
Na Happiness Katabazi
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Mbunge wa Jimbo la Segerea(CCM) na Msimamizi wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 wa jimbo hilo, wanaokabiliwa na kesi ya madai kupinga matokeo ya uchaguzi huo, wamewasilisha majibu katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, na wameomba kesi hiyo iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo (CHADEMA), Fred Mpendazoe ifutwe kwa gharama.
Sambamba na hiyo wadai wawili AG, na Msimazi wa Uchaguzi wa jimbo hilo wamewasilisha mapingamizi mawili ambapo pingamizi la kwanza wanadai kuwa hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho na kuwasilishwa na Mpendazoe Mahakamani ni batili kwasababu imekiuka amri ya mahakama iliyomtaka mlalamikaji huyo akaifanyie marekebisho tu hati hiyo ya madai lakini cha kustaajabisha mlalamikaji huyo amewasilisha hati hiyo iliyofanyiwa marekebisho huku akiwa ameongeza dai jipya ambalo halikupaswa kuwekwa kwenye hati hiyo hivyo wakaomba hati hiyo iliyofanyiwa marekebisho nayo itupwe.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo na wanatetewa na mawakili wa serikali David Kakwaya na Patience Ntwina wakati Mahanga ambaye ni Naibu Waziri wa Kazi,Ajira na Maendeleo ya Vijana anatetewa na wakili wa kujitegemea Jerome Msemwa waliwasilisha majibu hayo ya hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho kumetokana na amri iliyotolewa na Jaji Profesa Ibrahim Juma, Juni 22 mwaka huu kwa wadai hao kuwa ifikapo jana wawe wamewasilisha majibu ya hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho.
Kwa mujibu wa majibu hayo ambayo yamewasilishwa mahakamani kwa njia ya maandishi na Tanzania Daima inayo nakala yake, wadaiwa hao wanaiomba mahakama iifute kesi hiyo kwasababu madai ya mlalamikaji yanayodai taratibu za sheria ya Uchaguzi zilikiukwa katika uchaguzi ule ambao ulimtangaza mdaiwa wa pili(Mahanga) kuwa ndiyo mshindi hayana msingi.
“Sisi tunasema uchaguzi ule ulifuata taratibu zote za Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2010 na ndiyo maana Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilimtaka Dk.Mahanga kuwa ndiyo mshindi kati ya wagombea wote walioshinda na hivyo kufanya Mahanga kuwa mbunge….kwa hiyo sisi tunashangazwa na hayo madai ya mlalalamikaji kuwa sheria na taratibu za uchaguzi zilikiukwa na ndiyo maana tunaiomba mahakama hii tukufu iifute kesi hii tena kwa gharama”alidai Wakili Kakwaya.
Kuwasilishwa mahakamani kwa hati hiyo iliyofanyiwa marekebisho, kulitokana na utekelezaji wa amri iliyotolewa na Jaji Profesa Juma, Juni 6 mwaka huu, ambapo aliamuru hati ya madai ya awali ikafanyiwe marekebisho kwa kuviondoa vituo 10 vya kupigia kura ambavyo mlalamikaji hakuvitaja kwa majina.
Baada ya kufanyiwa marekebisho, Wakili wa mlalamikaji Peter Kibatala alieleza hivi sasa hati hiyo inasomeka kuwa wamebakiwa na vituo vya kupigia kura 249 ambapo vituo 120 ni vya Kata ya Kiwalani na vituo 129 ni vya Kata ya Vingunguti.
Jaji Juma aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 12 mwaka huu ambapo kesi hiyo itatajwa na kupanga tarehe ya kuanza kusikilizwa.
Novemba mwaka 2010 Mpendazoe alifungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo ambayo yalimtangaza mbunge wa sasa Dk. Mahanga kuwa ndiye mshindi kwa sababu uchaguzi huo ulikiuka matakwa ya sheria ya uchaguzi ya mwaka 2010.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Julai 6 mwaka 2011.
No comments:
Post a Comment