Header Ads

JAJI MKUU AONGOZA KUSIKILIZA RUFAA YA MOKIWA

Na Happiness Katabazi
KANISA la Anglikana Tanzania, limeiomba Mahakama ya Rufaa Tanzania kutengua amri ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha iliyoamuru Askofu Mkuu wa kanisa hilo Dk.Valentino Mokiwa akamatwe na ashtakiwa kwa sababu ametenda kosa la jinai la kudharau amri ya mahakama.


Katika kesi ya madai ya msingi iliyofunguliwa na waumini wa kanisa hilo katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ni Lothi Oilevo ,Godfrey Mhone na Frank Jackob ambao wanatetewa na Meinrad D’ Souzer.

Ambapo wadaiwa kwenye kesi hiyo ya msingi ambayo inayosikilizwa na Jaji Kakusulo Sambo ni Bodi ya Wadhamini ya kanisa hilo(So 4757) na Stanley Hotay ambaye ni askofu mteule ambao wanatetewa na wakili Joseph Thadayo na Albert Msando.

Ambapo katika madai hayo ya msingi waliwasilisha kwa Jaji Sambo ambapo waliomba mahakama yake itoe amri ya kuzuia uchaguzi wa askofu wa dayosisi Mount Kilimanjaro usifanyike na askofu mteule wa dayosisi hiyo asiapishwe ambapo mahakama kuu baadaye ilitoa amri ya Mhashamu Dk.Mokiwa akamatwe na ashtakiwa na adhibiwe kwa sababu amedharau amri ya mahakama kwani amemwapisha mdaiwa wa pili (Hotay) wakati mahakama hiyo bado haijatoa maamuzi yake.

Ombi hilo la kanisa la Anglikana la kutaka amri hiyo itenguliwe liliwasilishwa jana wakili wa kanisa hiyo Joseph Thadayo mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Chande Othman aliyekuwa akisaidiwa na majaji wa mahakama ya rufaa William Mandia na Steven Bwana.

Kusikilizwa kwa ombi hilo jana na Jopo hilo la majaji liloongozwa na Jaji Mkuu Othman, kulitokana hatua ya Mahakama ya Rufaa yenyewe kwa mamlaka iliyonayo (sue moto) kuliitisha jalada la kesi hiyo iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kuletwa katika Mahakama ya Rufaa ili mahakama hiyo ya juu nchini iweze kusikiliza pande mbili katika kesi hiyo, kutazama amri zilizotolewa na Jaji Sambo na kisha itatoa maamuzi yake.

Wakili Thadayo aliiomba mahakama hiyo itengue amri hiyo kwasababu hadi sasa hakuna amri ya mahakama iliyopuuzwa na wateja wake kwani hadi sasa Dayosisi hiyo bado haijapata askofu ila kilichofanyika ni mdaiwa wa pili (Hotay) kwa mujibu wa taratibu za kiimani za Kanisa la Anglikana walimweka wakfu na baada ya kuwekwa wakfu aliwekwa kwenye kiti na kisha kuzungukwa na maaskofu wa kanisa hilo.

Thadayo alieleza kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Kanisa hilo, askofu anaapishwa na Msajili wa Kanisa hilo ,Profesa Paramaganda Kabudi, na kwwamba Hotay akakuapishwa kuwa askofu na ndiyo maana hakuna mahali kokote mahakama na hao walalamikaji wanaweza kupata ushahidi kuwa mdaiwa huyo wa pili ameapishwa kuwa askofu wa dayosisi hiyo wakati tayari kulikuwa na kesi mahakamani ya kupinga kuapishwa.

“Watukufu majaji wa mahakama ya rufaa ,shauri hili limejikita kwenye imani za ya dini na kila kanisa linataraibu na kanuni zake jamani….Hotay ajaapishwa kuwa askofu kilichofanyika ni Hotay aliwekwa katika inada ya wakfu…sasa tumesikitishwa sana amri ya jaji Sambo inayotaka Mokiwa akamatwe kwa kudharau amri ya kwa kitendo cha kumuapisha Hotay kuwa askofu wa dayosisi hiyo wakati ukweli ni kwamba Hotay hajaapishwa kuwa askofu wa dayosisi hiyo kilichofanyika ni Kanisa lilimuandaliwa misa kumsimika Wakfu.

“Pia tumesikitishwa na amri hiyo ambayo sisi tunaiita ni batili kwani hata huyo Mokiwa siyo mdaiwa katika hii kesi…na kupitia amri ile ni wazi Jaji Sambo alishamhukumu Mokiwa kuwa ametenda kosa la kuidharau mahakama na kwamba anastahili kupatiwa adhabu ambapo kisheria mtu anayepatikana na kosa hilo atapaswa kwenda jela miezi sita ….sasa wakati jaji huyo anatoa amri hiyo alimnyima fursa ya askofu Mokiwa kujielezea”alidai Wakili Thadayo.

Kwa upande wake wakili wa walalamikaji Meinrad D’ Souzer aliliomba jopo hilo la majaji watatu kutupilia mbali pingamizi hilo la wakili wa wadaiwa kwa maelezo kuwa amri ya kukamatwa kwa askofu Mokiwa ni sahihi kisheria na kwamba tangu amri ile ilipotolewa, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alipaswa kumfungulia mashtaka Mokiwa.

Aidha Jaji Mkuu Othman alisema jopo lake limesikiliza hoja za pande zote za kesi hiyo ya madai Na. 1/2011 na kwamba tarehe ya uamuzi huo kutolewa, pande zote mbili zitaarifiwa na Msajili wa Mahakama ya Rufaani.

Juni mwaka huu, Jaji Sambo alitoa amri hiyo ya kiongozi huyo mkuu wa kanisa la Anglikana kukamatwa kwasababu jaji huyo alikuwa amesikiliza hoja za pande zote mbili ambapo kabla hajatoa uamuzi wa maombi ya kuzuia au kutozuia kufanyika kwa uchaguzi na ibada kumsimika uaskofu, kanisa hilo likadaiwa kabana ibada ya kumsimika uaskofu wa dayosisi hiyo mdaiwa wa pili kitendo kilichotafsiriwa na mahakama hiyo kuwa ni kuidharau mahakama hiyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Julai 16 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.