Header Ads

KESI YA JERRY MURRO YAPIGWA KALENDA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kwa mara nyingine jana ilishindwa kuanza kusikiliza utetezi wa aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1), Jerry Murro na wenzake wawili wanaokabiliwa na kesi ya kula njama, kushawishi na kuomba rushwa ya sh milioni 10 kutokana na wakili wa utetezi, Majura Magafu kushindwa kutokea mahakamani.


Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Stanslaus Boniface mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Moshi, aliieleza mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya washtakiwa kuanza kujitetea na kwamba upande wa jamhuri upo tayari kuendelea na kesi hiyo.

Hata hivyo, Wakili wa Jerry, Pascal Kamala, aliimbia mahakama kuwa wakili wa mshtakiwa wa pili na watatu ambaye ni Magafu hajafika mahakamani, hivyo wanaomba kesi iairishwe.

Hakimu Moshi alikubali ombi hilo na kuahirisha kesi hadi Agosti 3 mwaka huu washtakiwa hao watakapoanza kujitetea.

Mbali na Murro, washitakiwa wengine ni Edmund Kapama na Deogratius Mugasa ambao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 15 mwaka 2010.

Washitakiwa haop wanadaiwa kula njama, kushawishi na kuomba rushwa ya sh milioni 10 kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Karoli Wage. Kati ya mashitaka matatu yaliyofunguliwa dhidi yao, Murro anakabiliwa na mashitaka mawili.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Julai 7 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.