Header Ads

'MARANDA,FARIJALA WANAKESI YA KUJIBU"

Na Happiness Katabazi
UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya wizi wa sh bilioni 2.2 katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu ya Tanzania, inayomkabili Kada wa (CCM), Rajabu Maranda na Farijala Hussein umejigamba kuwa umeweza kuithibitisha kesi hiyo na umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, iwaone washtakiwa wote wana kesi ya kujibu.


Wakili Mwandamzi wa Serikali Arafa Msafiri aliyekuwa akisaidiwa na Oswald Tibabyekomya mbele ya Jaji Fatma Masengi aliyekuwa akisaidiwa na Hakimu Mkazi Catherine Revocati na Projestus Kahyoza aliwasilisha majumuisho hayo jana ambapo aliiomba mahakama hiyo iwaone washtakiwa wana kesi ya kujibu katika makosa yote saba wanayokabiliwa nayo.

Washtakiwa wote wanaishi gerezani baada ya Mei 23 mwaka huu, mahakama ya Kisutu kuwa hukumu kifungo cha miaka mitano jela kwa makosa ya kughushi na kisha kujipatia ingizo la sh bilioni 1.6 toka BoT na hivi wanakabiliwa jumla ya kesi tatu za EPA ambazo bado hazijatolewa hukumu.

Wakili Msafiri alikuwa akiwasilisha majumuisho hayo kwa mtindo wa kuchambua kosa moja moja huku akitumia ushahidi na vielelezo vilivyokwishatolewa na upande wa Jamhuri mahakamani hapo na kupokelewa, alidai kosa la saba ni la kughushi hati ya usajili wa jina biashara la Money Planners and Consultant ambacho ni kielelezo cha tatu ambayo walionyesha imetolewa na kusainiwa na shahidi wa kwanza wa Jamhuri ambaye ni Msajili Msaidizi wa Makampuni(BRELA).

Msafiri alidai kwa mujibu wa ushahidi wa shahidi huyo wa kwanza aliutoa hapa mahakamani,ambapo alikanusha kutoa jina hilo la biashara kwa washtakiwa hao na kwamba saini iliyodaiwa na washtakiwa kuwa ni ya kwakwe si yake na ripoti ya mtaalamu wa maandishi ilitolewa mahakamani hapa na shahidi mwingine ilidhibitisha washtakiwa hao waligushi jina la biashara,majina wa miliki na saini ya Naibu Msajili wa BRELA.

“Naibu Msajili wa BRELA katika ushahidi wake alieleza katika kampuni hizo hakukuwa na mabadiliko ya majina ya wamiliki wala jina la biashara la Money Planers kama ilivyodaiwa na upande wa utetezi na kwamba mtu anapotaka kubadili jina la biashara au wamiliki nilazima BRELA itampatia hati ya kubadilisha wamiliki au jina (Certificate Change of Particular) na washtakiwa hawana hati hiyo.

“ Na sisi Jamhuri katika kuthibitisha kosa hili tunasema kuna vielelezo viwili ambavyo ni maelezo ya onyo washtakiwa hao ambapo Farijala alikiri kuwa yeye ndiyo aliyeandaa fomu ya kujaza majina ya wamiliki wa kampuni yao ya Money Planers and Consultance BRELA kwa kutumia majina ya Fundi Kitunga na Thobias Nyingo ambao wanaonekana ndiyo wamiliki wa kampuni kwa maelekezo aliyoepewa na Maranda na kwamba yeye hawafahamu watu hao na hajawahi kuwaona.

“Na kwa mujibu wa maelezo ya onyo ya Maranda mshtakiwa huyo wa kwanza naye anadai hamfahamu Fundi na Nyengo ila akadai kuwa Fundi ni mtu wa karibu wa Farijala ….kwa maelezo hayo sisi upande wa Jamhuri tunasema washtakiwa hao ndiyo walitenda kosa hilo kwani nyaraka hizo za kughushiwa zimekutwa mikononi mwao wakizimiliki na sheria iko wazi kuwa anayekamatwa akimiliki nyaraka za kughushi ndiyo anayeshtakiwa kwa kosa la kughushi” alidai wakili Msafiri.

Akichambua kosa la tatu, ambalo ni la kuwasilisha nyaraka hizo zilizoghushiwa kwenye Benki ya Umoja wa Africa(UBA) ambao kwa sasa inatambulika kama BOA Benki, wakili huyo alidai kuwa washtakiwa hao ndiyo walikwenda kufungua akaunti yao Na.10913790010 kwa majina yao ya Farijala, Maranda kupitia nyaraka hizo zilizoghushiwa ambazo zilikuwa na majina ya kufikirika ya Fundi na Nyengo na kisha kujipatia ingizo la bilioni 2.2 toka kwa BoT.

Alidai kosa la nne, ni kughushi hati ya kuamisha deni (deed of assignment) ambapo ni kielelezo cha kumi ambacho kinaonyesha kampuni ya B.Grancel and Company ya Ujerumani iliyowakilishwa na Jones Bach na kampuni ya Money Planers iliwasilishwa na Fundi katika kuandaa hati hiyo ya kuamisha deni na kwamba kuna ushahidi wa mazingira wa kutosha kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo.

“Jamhuri tunasema huyo Fundi ni mtu wa kufikirika washtakiwa walimtunga kwa lengo la kuibia Tanzania, kwani katika maelezo ya onyo mshtakiwa wa pilisi Farijala alidai amfahamu Fundi wala Nyengo…na Fundi hajausika kwenye utoaji fedha kwenye akaunti, kuifungua akaunti hiyo…waliofungua akaunti, kuchuchukua fedha hizo ni washtakiwa wenyewe.

“Na ukiitaza hati hiyo ya kuamisha deni ambayo sisi upande wa Jamhuri tunasema imeghushiwa, utaona hati hiyo ilisainiwa Ujerumani baina ya kampuni hizo mbili Septemba 8 mwaka 2005, ukiangalia folio ya pili utaona kampuni ya B Grancel ya Ujerumani tarehe hiyo hiyo waliituma hapa nchini kwa Gavana wa BoT na Folio tatu inaonyesha siku hiyo hiyo , Fundi alimtumia hati hiyo Gavana wa wakati huo marehemu Daud Balali….sasa inawezekanaje hati hiyo isainiwe Ujerumani halafu siku hiyo hiyo ikatumwa kwa gavana na hati ya Fundi inaonyesha hati hiyo ameituma akiwa hapa nchini “alidai wakili Msafiri.

Aidha akilichambua shtaka la tano ambalo ni la kuwasilisha hati hiyo ya kuamisha deni ambayo imegushiwa na kwamba wameweza kuthibitisha kosa hilo kwasababu ushahidi uliopo unaonyesha ni washtakiwa hao ndiyo waliwasilisha hati hiyo ya kuamisha deni ambayo imegushiwa katika BoT na kisha kujipatia ingizo la Sh bilioni 2.2.

Wakili Msafiri alidai shtaka la sita ni la wizi, ambapo alidai pia kuwa wameweza kulithibisha kwani kwa mtiririko wa ushahidi uliotolewa na mashahidi wa jamhuri ni ambao unaonyesha washtakiwa walikula njama, wakaghushi nyaraka mbalimbali na kisha wakatumia nyaraka hizo kufungua akaunti na kisha washtakiwa hao walikiri mahakamani hapo waliingiziwa fedha hizo kihalali na BoT.

Wakili huyo alidai shtaka la kwanza ni la kula njama, ambapo alidai wameweza kuthibitisha kosa hili kwani kupitia maelezo ya onyo ya washtakiwa hao na yalipokelewa na mahakama hii kama vielelezo,yanadhiirisha wazi washtakiwa hao walipanga kwa pamoja kuibia BoT kiasi hicho cha fedha.

Kwa upande wake kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi wanaosilikiza kesi hiyo Jaji Fatma Masengi alisema wamesikiliza kwa makini majumuisho yaliyotolewa na upande wa Jamhuri jana na majumuisho yaliyotolewa na upande wa utetezi siku za nyuma na kwamba Julai 18 mwaka, watakuja kutoa uamuzi wa kuwaona washtakiwa wana kesi ya kujibu au la.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne,Julai 5 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.