Header Ads

MAHAKAMA YA KISUTU ,HII NI AIBU

Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, ni miongoni mwa mahakama za hadhi hiyo yenye umaarufu kuliko nyingine zote hapa nchini.


Naweza kusema umaarufu wa Mahakama ya Kisutu unatokana na baadhi ya mambo kadha wa kadha kama waandishi wa habari za mahakama kila siku tano za juma kuweka kambi mahakamani hapo kwa ajili ya kufuatilia kesi mbalimbali na kisha kuziripoti.

Baadhi ya watu wenye umaarufu katika jamii, maofisa wa serikali, taasisi za kidini na michezo wamefunguliwa kesi katika mahakama hiyo na baadhi kufungwa jela baada ya kukutwa na hatia na wengine kushinda kesi zao.

Mambo mengine yanayoifanya mahakama hiyo iwe maarufu ni kwa sababu mahakama hiyo ipo katikati ya Jiji la Dar es Salaam na sifa nyingine ni kwamba hivi sasa mahakama hiyo ipo katika hatua za mwisho za ukarabari wa majengo yake.

Napongeza kukarababitiwa kwa mahakama hiyo.

Leo nazungumzia kuhusu uchafu wa vyoo vitatu vya nje vya mahakama hiyo ambavyo vinashusha heshima na hadhi ya uongozi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kwa wale wenzangu ambao tunapata fursa ya kufika mahakamani hapo kwa siku tano za juma, au wale wananchi wanaofika mahakamani hapo kwa ajili ya shida mbalimbali na kupata fursa ya kuingia kwenye vyoo vitatu vilivyopo nyuma ya mgahawa wa mahakama hiyo, watakubaliana na mimi kuwa vyoo hivyo vinatia kinyaa na kichefuchefu kwa ajili ya uchafu na aviwekwi maji kwa ajili ya watumiaji.

Binafsi ninachokizungumza hapa nimekuwa nikikishuhudia kwa macho yangu na mara ya mwisho ni Ijumaa iliyopita, nilipoingia ndani ya vyoo hivyo nikiwa na mwandishi mmoja, sote tukashuhudia kadhia hiyo iliyotukera.

Kwa kuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii chini ya Waziri Dk. Haji Mponda kila mara imekuwa ikitusisitiza wananchi tuweke mazingira yetu safi na tunapotoka vyooni tunawe mikono ili kujiepusha na magonjwa ya milipuko na kuweka vyoo vyetu safi, lakini msisitizo huo wa wizara hiyo naona unapuuzwa na wahusika wa usafi wa Mahakama ya Kisutu ambao wamepewa jukumu la kuhakikisha vyoo hivyo vitatu vinakuwa visafi.

Sote tunafahamu mahakamani ni sehemu ambayo watu wengi wanakuja na kama watu wengi wanakuja ni dhahiri taasisi hiyo inapaswa iwe na vyoo safi ili kuepusha magonjwa ya milipuko.

Katika mgahawa wa Mahakama ya Kisutu nyuma yake ndiyo hivyo vyoo.

Watu wanapata vyakula na vitafutwa wakati wakisubiri kesi zao na wengine huwa wanakwenda kwenye vyoo hivyo ambavyo hivi sasa vimebadilika rangi kwaajili ya uchafu.

Hatuoni kwamba kama uongozi wa mahakama unaohusika na masuala ya usafi wa mazingira ya eneo hilo usipojirekebisha na kuvifanyia usafi vyoo hivyo mwisho wa siku vinaweza kuleta magonjwa ya mlipuko mahakamani?

Au ni kwa sababu vyoo hivyo havitumiwi na waheshimiwa mahakimu ndiyo maana havisafishwi ipasavyo na kuwekwa maji? Au kwakuwa vyoo hivyo vinatumiwa na watu wa kawaida ambao si mahakimu?

Siku hizi karibu kote barabarani dawa za kusafisha vyoo zinauzwa tena kwa bei ndogo.

Sasa kinachowashinda ni kitu gani kumwajiri mtu atayekuwa akisafisha vyoo hivyo kwa uhakika, kujaza maji na kutoa mabaibui yaliyotanda kwenye vyoo hivyo?

Mbona hali sivyo kwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mahakama ya Rufani? Au ndiyo mahakama ya Kisutu itajitetea kuwa inapewa fungu dogo la fedha hivyo haliwezi kutosha kununua dawa za choo, kumlipa msaficha vyoo hivyo?

Lakini katika hilo la uchafu kuhusu vyoo hivyo vitatu sishangai sana, kwani ningali nikikumbuka miaka mitatu nyuma vyumba vya wazi vinne vya kuendeshea kesi vya mahakama hiyo vilivyokuwa vimekithiri kwa uchafu wa tanda bui, feni ambazo zilikuwa zimechakaa na kulika na kutu na ndege kujenga jumba zao(viota) kwa majani katika feni hizo zilizokuwa zimeharibika, pamoja na kunuka kwa harufu ya mikojo kutoka ndani ya mahabusu ya mahakama hiyo.

Licha ya matatizo hayo ya miaka ya nyuma kutatuliwa kutokana na kufunguliwa kesi 12 za wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu ya Tanzania (EPA) Novemba 4 mwaka jana, baada ya waandishi wa habari za mahakama kuziripoti kesi hizo kikamilifu pamoja na kuyageukia matatizo hayo kuyaandika katika vyombo vya habari na hatimaye mwisho wa siku matatizo hayo yakatatuliwa na feni mpya zikanunuliwa na kufungwa.

Lakini kwa sasa feni hizo zimeanza kuwa na vumbi na hazionyeshi dalili za kufutwa vumbi hilo mara kwa mara.

Nayaandika haya kwa nia njema ya kujenga na si kuboboma.

Kupitia mtazamo huu naamini wahusika kama ni wasikivu na wapenda changamoto wataifanyia kazi kero ya uchafu wa vyoo ambao unaipa sifa mbaya mahakama hiyo yenye mahakimu wakazi wanaoongozwa na Hakimu Mkuu Mfawidhi Elvin Mugeta, watanashati wanaovalia suti na majoho safi, lakini vyoo vitatu vilivyopo ndani ya mahakama wanayoiongoza ni vichafu.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

0716 774494.
www.katabazihappy.blogspot.com
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Julai 12 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.