Header Ads

MPENDAZOE ADAI AG ANANJAMA NA KESI YAKE

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA mgombea Ubunge wa Jimbo la Segerea(Chadema), Fred Mpendazoe amwandikia barua Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ya malalamiko kwamba mapingamizi yanayoondelewa kuekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wenzake katika kesi yake yana njama ya kuchelewesha kesi hiyo ya kupinga matokeo ya jimbo hilo isimalizike kwa wakati.


Katika kesi ya kupinga matokeo ya jimbo hilo Na.98/2010. Mpendazoe anamshtaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Mbunge wa jimbo hilo Dk.Makongoro Mahanga(CCM) na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo ambalo wanatetewa na David Kakwaya, Patience Ntinwa na Jerome Msemwa ambapo mlalamikaji anataka ushindi huo utenguliwe kwasababu kanuni na taratibu za sheria ya uchaguzi zilikiukwa.

Barua hiyo hiyo iliandikwa Julai 5 mwaka huu, na wakili wa mlalamikaji, Peter Kibatala yenye sababu saba ambayo inaanza kwa kumuomba Msajili huyo aifikishe barua hiyo kwa Jaji Profesa Ibrahim Juma ambaye ndiye anasikiliza kesi hiyo ya msingi.

Wakili Kibatala anaeleza kuwa Juni 6 mwaka huu, Jaji Juma alitoa uamuzi wa kutaka hati ya madai iende ikafanyiwe marekebisho baada ya kutaka vituo vinne vya kupigia kura vya Kata ya Buguruni, vituo 2 vya Kata ya Tabata, na vituo 4 vya Kata ya Kipawa viondolewe katika hati ya madai ya awali.

Wakili huyo anasema baada ya uamuzi huo wa mahakama, Juni 20 mwaka huu, mlalamikaji aliwasilisha hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho mahakamani hapo, na upande wa wadai Julai 4 mwaka huu, nao waliwasilisha majibu ya hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho.

“Lakini siku hiyo wakati wadaiwa wanawasilisha majibu yao kwa maandishi, mdaiwa wa kwanza (AG) na mdaiwa wa tatu ambaye ni Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Segerea, waliwasilisha mapingamizi mawili wakitaka mahakama hiyo iifute hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho kwasababu ni batili na imeongeza lalamiko jipya kinyume na amri ya mahakama iliyotolewa Juni 6 mwaka huu, ambayo ilimwamuru mlalamikaji kwenda kuifanyia marekebisho hati ya madai kwa kuviondoa vituo hivyo vya kupigia kula katika hati hiyo.

“Naandika barua hii kwako mheshimiwa kwa masikitiko makubwa na uamonifu mkubwa licha hatuna jinsi ya kuizuia mahakama hii isikilize pingamizi hilo la wadaiwa ila pingamizi hilo linatufanya tuwe na hisia mbaya kwamba wadaiwa hao wameliwasilisha mbele yako kwa lengo la kuchelewesha kesi hii isimalizike ndani ya muda wa mwaka mmoja ambao umewekwa na Sheria ya Uchaguzi…kwa kuwa tunaamini kabisa hati yetu yetu tuliyoifanyia marekebisho siyo batili kama inavyodaiwa na hao wenzetu ” alidai Wakili Kibatala.

Hivyo wakamuomba Jaji Juma kuwazuia wadaiwa kuwasilisha mapingamizi ambayo yanarudisha nyuma kasi ya uendeshwaji wa kesi hiyo ya Uchaguzi ambayo kwa mujibu wa Kanuni na Sheria ya Uchaguzi inataka kesi ya uchaguzi imalizike ndani ya mwaka tangu ilipofunguliwa wakati kesi hiyo imefunguliwa Novemba mwaka jana, na hadi sasa bado ushahidi haujaanza kutolewa.

Aidha kesi hiyo ilikuja jana mbele ya Jaji Juma kwaajili ya kupanga tarehe za kuanza kusikiliza kesi hiyo lakini jaji huyo alishindwa kupanga tarehe hizo kama alivyoahidi Juni 6 mwaka huu, kwa sababu ya wadaiwa wawili kuwasilisha mapingamizi mawili ambapo kisheria mahakama inapaswa iyasikilize kwanza na kuyatolea uamuzi mapingamizi hayo ndiyo ije ipange tarehe za kuanza kupokea ushahidi.

Hata hivyo jaji huyo alisema Julai 27 mwaka huu, ndiyo atayasikiliza mapingamizi hayo mawili na kuwataka mawakili wa pande zote mbili wafike mahakamani hapo bila kukosa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Julai 13 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.