Header Ads

POLEPOLE LOWASSA


Na Happiness Katabazi

HIVI karibuni Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, alisema mengi yenye tija bungeni na kuwataka viongozi wachukue maamuzi magumu.


Lowassa aliwashambulia viongozi wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete kuwa wana ugonjwa wa kuogopa kufanya maamuzi magumu. Bila kufafanua, alisema ni bora kiongozi uhukumiwe kwa kufanya maamuzi magumu kuliko kuogopa.

Pamoja na mambo mengine, alisema wakati taifa likiadhimisha miaka 50 ya Uhuru, serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imefanya mambo mengi ambayo si vema watu kuyabeza.

Binafsi nakubaliana na hoja ya Lowassa kwamba wakati taifa likiadhimisha miaka 50 ya Uhuru wake, serikali ya CCM imefanikiwa kuleta maendeleo kwa kiwango fulani katika sekta ya elimu, teknolojia hasa ya habari, nishati na barabara.

Anayebisha katika hili ni wazi hajapata fursa ya kuizunguka Tanzania Bara na Zanzibar, kamwe sitamlazimisha mtu akubaliane nami kwamba katika kipindi hiki cha miaka 50 ni wazi kuna hatua za maendeleo taifa limepiga.

Lakini kuhusu hoja ya Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli kwamba hivi sasa viongozi wana ugonjwa wa kutochukua maamuzi magumu, binafsi kauli hii imeniachia na maswali mengi kuliko majibu.

Mimi ni miongoni mwa wanahabari tunaofuatilia mambo yanayohusu mustakabali mwema wa taifa hili, matamshi na matendo yanayofanywa na baadhi ya wanasiasa wetu, huwa nayaweka kwenye kumbukumbu zangu.

Itakumbukuwa kuwa Rais Kikwete aliapishwa Desemba 23 mwaka 2005 kuliongoza taifa hili akiwa ni rais wa awamu ya nne, siku chache baadaye aliliteua jina la Lowassa likapelekwa bungeni ili kuidhinishwa kuwa waziri mkuu.

Kweli Lowassa alianza kazi hiyo kwa kishindo, na mpongeza kwa kazi nzuri ya kushupalia ujenzi wa shule za sekondari kila kata licha ya changamoto kadha wa kadha zilizopo kwenye shule hizo, zimesaidia kuwapa tamaa wazazi wengi kuwapeleka watoto wao ili wapate elimu.

Lakini ningali nikimkumbuka kwa jengo la Hoteli ya Chang’ombe Village lililoanguka na kuua mtu mmoja, Lowassa alitembelea eneo hilo na kuamuru mhandishi wa Manispaa ya Temeke na mainjia wake wakamatwe.

Agizo lake lilitekelezwa na wahusika walifikishwa mahakamani, kwa kosa la kuua bila kukusudia. Mwisho wa siku mainjinia wa manispaa hiyo walishinda kesi hiyo na wakaachiliwa huru.

Pia ningali na kumbukumbu ya majengo mawili ya ghorofa yaliyopo Masaki jijini Dar es Salaam ambapo ulizuka utata kuwa wamiliki wa majengo hayo walijenga eneo hilo bila kibali cha Manispaa ya Kinondoni.

Utata ulikuwa kwamba kuna baadhi ya watumishi wa manispaa hiyo waliwapatia kibali cha ujenzi kilichoghushiwa.

Mgambo walitekeleza agizo la Lowassa na kuyabomoa majengo hayo ambayo ujenzi wake ulikuwa umekamilika.

Hata hivyo wamiliki wa majengo yale walikimbilia Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi na kuifungulia kesi serikali na walishinda, mahakama ikaamuru wenye majengo walipwe mamilioni ya fedha.

Ikumbukwe wakati Lowassa ni mwana CCM na Ibara ya 18(a) ya Katiba ya nchi ya mwaka 1977 inasema kila mtu anao uhuru wa kutoa maoni na kueleza fikra zake hivyo Lowassa wakati akizungumza alikuwa akiitumia haki yake hiyo ya kikatiba.

Lakini anapotuambia viongozi wengi hivi sasa wana ugonjwa wa kutochukua maamuzi magumu, kwanini hajatutajia viongozi walioshindwa kuchukua maamuzi hayo?

Maana hata ndani ya majeshi yetu kuna viongozi,kwenye dini,serikalini na bungeni kuna viongozi pia. Swali nililonalo ni je, hata viongozi walio kwenye majeshi yetu nao wanasumbuliwa na ugonjwa na kushindwa kuchukua maamuzi magumu?

Namtaka Lowassa atambue kuwa kuna baadhi ya viongozi huko kwenye serikali inayoongozwa na chama chake, kwenye majeshi yetu na kwenye mhimili wa mahakama ni wachapakazi na waaminifu, wenye uthubutu wa kuchukua uamuzi wa haki na si wa jazba.

Wanachukua uamuzi mgumu wenye masilahi kwa taifa letu na kamwe viongozi hao hawajitokezi hadharani wakitamba kuwa wamechukua uamuzi mgumu.

Viongozi wa aina hii binafsi nawafahamu na wengine wamekuwa wakiingia ofisini saa 12 asubuhi lakini hata siku moja sijawaona wakipita mitaani na kujitapa.

Kama ni kweli Lowassa anasema viongozi wa serikali ya awamu ya nne wanasumbuliwa na ugonjwa huo, kwa nini wananchi wengi katika Uchaguzi wa mwaka 2010 waliipatia tena kura za ndiyo CCM ikashinda na kisha ikaendelea kutawala?

Ugonjwa huo ameubaini lini? Ni baada ya kuwa nje ya utumishi wa serikali tangu alipojiuzulu kwa kashfa ya Richmond mwaka 2008? Na kama kweli ugonjwa huo ameubaini, anakusudia kutumia dawa ipi ili kuwatibu viongozi hao?

Nimalizie kwa kusema, Watanzania tunahitaji kuwa na viongozi makini wasio na jazba.
Viongozi wanaochukua uamuzi wakati wana jazba, mara nyingi viongozi wa aina hiyo huigharimu serikali, kwani walioonewa na hukimbilia mahakamani, fedha za walipa kodi ndizo zinazotumika kuwalipa fidia walioonewa.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
0716 774494
www.katabazihappy.blogspot.com
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Julai 5 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.