HUKUMU YA MARANDA YAYEYUKA TENA
Na Happiness Katabazi
KWA mara ya pili sasa, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imejikuta ikishindwa kutoa hukumu katika kesi ya wizi wa sh bilioni 2.2 kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu inayomkabili kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rajabu Maranda na binamu yake, Farijala Hussein kwa sababu baadhi ya mahakimu waliokuwa wakiisikiliza wana matatizo ya afya.
Jana kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutolewa hukumu ambayo ilishindikana kutolewa Mei 17 mwaka huu, kwa sababu ya kuugua kwa Hakimu Mkazi Catherine Revocate ambaye anaunda jopo jopo la mahakimu watatu wanaosikiliza kesi hiyo, pamoja na Jaji Fatma Masengi na Projest Kahyoza.
Hakimu Mkazi Kahyoza aliyefika mahakamani hapo jana, ambapo ukumbi wa mahakama ulikuwa umefurika ndugu wa washitakiwa hao na waandishi wa habari, alianza kwa kusema kuwa ni kweli kesi hiyo ilikuja jana kwa ajili ya kutolewa hukumu, lakini haitawezekana kwa sababu mwanajopo mmoja bado afya yake haijatengamaa na ndio amerudi nchini akitokea nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
“Kwa sababu hiyo, napenda kusema kuwa hukumu ya Maranda leo haitasomwa na badala yake itasomwa Julai 24 mwaka huu, na tutajitahidi wanajopo wote tuwepo ili tuweze kuisoma kwani tayari tumeishaindaa hukumu yetu, ipo na hatutaki tukae nayo sana kwani haya makaratasi yasije yakatuzoea,” alisema.
Baada ya Hakimu Kahyoza kusema hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Oswald Tibabyekomya alisema hana pingamizi na amri hiyo ya mahakama.
Hadi sasa washitakiwa wanatumikia kifungo katika Gereza la Ukonga, na kumalizika kwa kesi hiyo kutawafanya wabakiwe na nyingine tatu ambazo zimefikia hatua ya kuendelea kusikilizwa.
Mei 23 mwaka jana walitiwa hatiani na mahakama hiyo kwa makosa ya kughushi, kula njama na kujipatia ingizo la sh bilioni 1.8 za EPA.
Wakati huo huo, upande wa jamhuri unaowakilishwa na wakili wa serikali, Prosper Mwangamila katika kesi ya kuendesha upatu inayowakabili viongozi wa Taasisi ya DECI, ulifunga kesi hiyo baada ya mashahidi wake 16 kumaliza kutoa ushahidi wao.
Hakimu Mkazi Stewart Sanga aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 17 mwaka huu, ambapo siku huyo atakuja kutoa uamuzi wa ama washitakiwa wana kesi ya kujibu au la.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Julai 27 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment