Header Ads

KESI YA KIBANDA YAFIKA PATAMU

Na Happiness Katabazi UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kuandika na kuchapisha makala ya uchochezi inayomkabili Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima,Absalom Kibanda na wenzake jana uliwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam. Mbali na Kibanda washitakiwa wengine ni Samson Mwigamba ambaye ni mwandishi wa makala wa gazeti la Tanzania Daima na Kaimu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd, Theophil Makunga ambao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Mabere Marando ,Gabriel Mnyele, Isaya Matamba, Juvenalis Ngowi na Hohn Mhozya na Frank Mwilongo. Wakili wa serikali Elezabeth Kaganda mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema alianza kwa kuikumbusha mahakama hiyo kuwa kesi hiyo ilikuja kwaali ya kuwasomea maelezo ya awali na kwamba wapo tayari kwaajili ya kufanya hivyo na akaanza kuwasomea maelezo ya awali kama ifuatavyo. Kaganda alidai alidai mshtakiwa wa kwanza na wapili(Mwigamba na Kibanda) wanakabiliwa na kosa la kwanza la kuandika makala ya uchochezi iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “Waraka maalum kwa askari wote’. Alidai kuwa Mwigamba ambaye Mhasibu wa Chama Cha Demokrasi Chadema na Kibanda ambaye ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la Tanzania Daima, kwa pamoja waliandika na waliruhusu makala hiyo ichapishwe kwenye gazeti hilo ambayo iliandikwa na gazeti la Tanzania Daima la Toleo Na. 2552 la Novemba 30 mwaka 2011 na makala hiyo ambayo ni ya uchochezi ikaja kuchapishwa na mshiutakiwa wa tatu (Makunga) kupitia kiwanda cha upachaji ambacho kipo chini ya uongozi wake. “Sisi upande wa jamhuri tunadai kuwa makala hiyo ni ya uchochezi na ilikuwa ikiwashawishi askari wa Jeshi la Wananchi,Polisi,Magereza na KMKM wasiitii amri za makamanda wao jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi na hata Desemba 6 na Desemba 20 mwaka jana, washitakiwa hao walipofika katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini na kuhojiwa ,walikiri kutenda makosa hayo ya kuandika na kuchapisha makala hiyo”alidai wakili Kaganda. Hata hivyo Hakimu Lema baada ya wakili Kaganda kumaliza kuwasomea maelezo hayo aliwataka washitakiwa hao waseme wanayakubali nini katika maelezo hayo ya awali , washitakiwa wote walikubali majina yao tu na wakayakana maelezo mengi kwa madai kuwa maelezo hayo si sahihi. Baada ya kumaliza hatua hiyo, wakili Kaganda alivitaja vielelezo watakavyovitumia wakati kesi hiyo ikianza kusikilizwa ambavyo ni makala yenyewe, maelezo ya washitakiwa na maoni ya wataalamu na hata hivyo akakataa kutaja orodha ya majina ya mashahidi ambao watawaleta kutoa ushahidi. Kwa upande wake Hakimu Lema alitoa amri ya kuutaka upande wa Jamhuri uakikishe unawapatia maelezo ya mlalamikaji wa kesi hiyo upande wa utetezi mapema iwezekanavyo na kwamba anaiarisha kesi hiyo Agosti 7 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa rasmi. Machi 7 mwaka huu, Wakili Kaganda akiisoma hati mpya ambayo ina mashtaka mawili tu ambapo kosa la kwanza ni la uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1)(c) na 31(1)(a) cha Sheria ya Magazeti Sura ya 229 ya mwaka 2002 ambalo lina mkabili mshtakiwa wa kwanza na wa pili yaani Mwigamba na Kibanda. Ambapo wakili Kaganda alidai kuwa mnamo Novemba 30 mwaka 2011 jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao wawili kwa makusudi na kwa nia kuvunja sheria za mamlaka ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitenda kosa hilo la uchochezi kwa kuruhusu makala hiyo ichapishwe kwenye gazeti la Tanzania Daima la Novemba 30 mwaka 2011 iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “ Waraka Maalum kwa askari wote’ ambapo ilikuwa ikiwachochea askari hao wasitii mamlaka za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Julai 27 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.