VIGOGO BODI YA WATINGA KORTINI
Na Happiness Katabazi
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Watalaam wa Manunuzi na Ugavi (PSPT), Clemence Tesha na wenzake jana walijikuta wakifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, wakikabiliwa na makosa ya matumizi mabaya ya madaraka.
Mbali na Tesha washitakiwa wengine ni Winfrida Igogo ambaye ni Afisa Rasilimali watu Mwandamizi na mshitakiwa wa tatu ni Amani Ngonyani ambaye ni Meneja Biashara na Maendeleo wa Bodi hiyo ambapo wanatetewa na wakili wa kujitegemea Frank Kiliani.
Mawakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), Salha Abdallah na Sophia Gula mbele ya Hakimu Mkazi Faisa Kasamba walidai kuwa kosa la kwanza ni la matumizi mabaya ya madaraka kinyume cha na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana Rushwa ya mwaka 2007, ambapo kosa hilo linamkabili mshitakiwa wa kwanza na wa pili.
Wakili Abdallah alidai Juni 22 mwaka 2010 katika ofisi za Bodi hiyo, washitakiwa walimuajiri mshitakiwa wa tatu(Ngonyani) kushika wadhifa huo wakati Ngonyani hajasajiliwa na Bodi ya Watalaamu wa Manunuzi na Ugavi,kitendo ambacho kinakwenda kinyume na kifungu cha 46(1) cha Sheria ya Bodi hiyo ya (PSPT) ya mwaka 2007.
Wakili Abdallah alidai kuwa shitaka la pili ambalo linamkabili mshitakiwa wa kwanza na wapili , ni la kumwajili mshitakiwa wa tatu (Ngonyani) kushika wadhifa huo wakati wakijua mshitakiwa huyo alikuwa hajasajiliwa na bodi hiyo kitendo ambacho ni kinyume na kifungu cha 46(1)(3) cha Sheria ya Bodi hiyo.
Alidai kuwa Juni 22 mwaka 2010 Tesha na Igogo wakiwa na nyadhifa zao walimwajiri Ngonyani kama Menej wa Biashara na Maendeleo wa bodi hiyo hku wakijua Ngonyaji hakuwa amesajiliwa na bodi hiyo ya wanataaluma wa masuala ya ugavi na manunuzi.
Aidha wakili Abdallah alidai shitaka la tatu ni kwa ajili ya mshitakiwa wa tatu pekee ambalo ni kujipatia ajila hiyo ya kazi za manunuzi kinyume na sheria jambo ambalo ni kinyume na kifungu cha 46(2),(3) cha sheria ya bodi hiyo kwamba Juni 22 mwaka 2010 katika ofisi ya bodi hiyo alijipatia ajira hiyo wakati akijua wazi hakuwa amesajiliwa na bodi hiyo na kuongeza kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Hata hivyo washitakiwa wote walikana mashitaka hayo na Hakimu Mkazi Kahamba alisema kesi inayowakabili ina dhamana na hivyo kumtaka kila mshitakiwa awe na wadhamini wa wiwili wanaotoka ofisi zinazotambulika na serikali ambapo watasaini bondi ya Shilingi milioni 10.Washitakiwa wote walitimiza masharti hayo na wapo nje kwa dhamana na akaiarisha kesi hiyo hadi Julai 26 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Julai 29 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment