Header Ads

KESI YA HASSANOL YADODA

Na Happiness Katabazi MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilishindwa kuanza kusikiliza kesi ya wizi wa madini ya shaba yenye thamani ya sh milioni 400, inayomkabili Katibu wa zamani wa Simba, Hassan Hassanol (43) na wenzake watatu. Hiyo imetokana na wakili wa serikali aliyekuwa akiindesha kesi hiyo tangu awali, Elizabeth Kaganda kuwakabidhi jukumu hilo mawakili wengine kwani yeye ametingwa na majukumu mengine. Mbele ya Hakimu Mkazi Devotha Kisoka, mawakili wapya wanaoendesha kesi hiyo, Theophil Mtakyawa na Ester Kyala, waliieleza mahakama kuwa, kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya mashahidi wa upande wa jamhuri kuanza kutoa ushahidi. Hata hivyo, walisema hilo halitawezekana kwa sababu wakili wa serikali (Kaganda), aliyekuwa akiendesha kesi hiyo amewakabidhi wao kuiendesha kwa kipindi chote kutokana yeye kupewa majukumu mengine ya kiserikali. “Na leo (jana) asubuhi ndiyo tumekabidhiwa jalada la kesi hii, hivyo hatujajiandaa kabisa, tunaomba mahakama itupatie muda ili twende tukalisome jalada hii tufahamu vizuri kesi hii,” alidai wakili Mtakyawa. Hakimu Kisoka alikubaliana na ombi hilo na akaahirisha kesi hiyo hadi Julai 25, maka huu itakapokuja kutajwa na Agosti 6-7 itaanza kusikiliziwa. Katika hati ya mashitaka, wanadaiwa Agosti 28 mwaka 2011 jijini Dar es Salaam, washitakiwa hao kwa pamoja, walipanga njama ya kuiba mali hizo. Shitaka la pili, tarehe hiyo hiyo, washitakiwa hao waliiba tani 26 za madini ya shaba yenye thamani ya fedha hizo yaliyokuwa yanasafirishwa kutoka Zambia kuja nchini. Ilidaiwa kuwa, madini hayo yalikuwa yanasafirishwa kwenye lori lenye namba za usajili T 821 BCL na tela namba T 566 BCL ambayo ni mali ya Kampuni ya Liberty Express. Katika shitaka la tatu, wanadaiwa washitakiwa hao walipokea mali hiyo huku wakijua kuwa ni ya wizi. Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Wabura Magenga (32), Dk. Najim Msenga na Salim Shekibala. Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Julai 27 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.