WAHUNI NDIYO WALIOFANYA UHALIFU ZANZIBAR
Na Happiness Katabazi
JUNI 26-27 mwaka huu, huko kwenye Jiji la Zanzibar viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu maarufu kwa jina la Uamsho, walileta katika mkoa wa mjini Magharibi ,Unguja iliyosababisha uvunjifu wa amani na kuchoma makanisa mawili , maduka ya watu kuvunjwa na mali zao kuibiwa kwa madai kuwa wanapinga Muungano.
Taasisi hiyo imeanzishwa kwa madhumuni ya kidini, lakini hivi
sasa viongozi wake wanaonekana wazi kuyaacha madhumuni hayo na kubeba ajenda
za siasa.
Awali ya yote kwanza nataka ieleweke wazi waliofanya uhuni,uhalifu huu sio Wazanzibari wote na wala siyo waislamu kama baadhi ya watu wanavyotaka kuamini waliofanya uhuni ule ni wazanzibar na waislamu wote.
Ni genge la waharifu tu ambalo limevaa sura ya jumuiya ya kidini ndiyo limefanya uhalifu huo kwa kuwa limefanya uhalifu na linataka liiungwe mkono likajaribu kutaka kuonyesha kuwa ni waislamu na wazanzibar wote wapo nyuma yao na wanakerwa na muungano,jambo ambalo si la kweli na ninawashukuru wale viongozi wa dini ya Kiislamu waliojitokeza kukanusha hilo na pia kuwashukuru viongozi wa dini ya Kikristo kuwa na moyo wa uvumilivu kwa vurugu hizo.
Ni wahuni hao ambao uenda wametumwa na kupewa ujira na maadui zetu wanaotuonea wivu na amani tuliyonayo ili waanzishe vurugu mwisho wa siku amani yetu tuliyoirinda kwa miaka mingi itoweke.
Kwa sababu haingii akilini kabisa jumuiya ya kidini ambayo moja ya jukumu lake ni kuamasisha amani ndiyo inakuwa mstari wa mbele kutofuata taratibu za kisheria kudai hayo madai yao matokeo yake wanatumia njia za kihalifu kudai madai yao jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi.
Nasisitiza waliofanya uhalifu ule ni wahuni kwasababu wameshindwa kuheshimu mamlaka iliyopo duniani kwani hata vitabu vya dini vinatutaka tuheshimu mamlaka zilipo duniani.
Hivi hii Jumuiya ya Uamusho ni Muungano kweli ndiyo unawakera hadi wanachoma makanisa na maduka na kuleta vurugu kweli?
Kwa sisi tuliofika Zanzibar zaidi ya mara nne tumeweza kushuhudia baadhi ya vitendo vichafu ambavyo vinapingwa na vitabu vya dini.Mfano vitendo vya watu wa jinsi moja kujamiana yaani vitendo vya ushoga na usagaji,matumuzi ya dawa za kulevya.Licha matendo hayo pia hata huku Tanzania Bara yapo.
Kwahiyo hayo matendo machafu hayaikeli hiyo jumuiya ya uamsho?Maana jumuiya hiyo ni ya kidini na inajumuku la kuyakemea kwa nguvu zote lakini hatuisikii ikielekeza nguvu zake zote kukemea uchafu huo ambao unaipaka matope Zanzibar yetu.
Binafsi sipingi Muungano wetu usijadile,napenda ujadiliwe kwa amani na wanaojadili wawe na nia safi mioyo mwao na watoe maoni yao kwa njia ya amani tu bila vurugu.Na kero za Muungano kisiwe chanzo cha kuleta vurugu.
Tunapaswa kujiuliza kwanza hivi huo Muungano umeanza kuikera kwa sana hivi karibuni jumuiya hiyo hadi wafikie kufanya uhalifu huo? Tuiulize hiyo jumuiya njia ile ya vurugu ya kupinga muungano wiki iliyopita,ndiyo imewasaidia kutatua shida yao? Jibu ni kwamba tatizo lao halijatatuliwa.
Nilichokiona mimi njia hiyo haramu waliyoitumia sana sana imewafanya wajikute wakiangukia kwenye mikono ya dola kwa kufunguliwa kesi mahakamani na kutokana na hali hiyo waliofikishwa mahakamani ndiyo wameanza kuwa watumwa wa mahakama hadi pale mahakama itakapotoa maamuzi yake.
Kwa wale tuliofika Zanzibar, tutakubalina kuwa eneo waumini wa dini ya Kiislamu ndiyo wanaoishi kwa wingi huko.Lakini kuishi kwao huku kwa wingi hakuwazui wakristo kuishi wala kufanyakazi na kushirikiana pamoja katika masuala ya kijamii na kiserikali.
Wazanzibar ni wenzetu na Muungano wetu utabaki kuwa ni wa kipekee hapa duniani kwani tangu uundwe haujawahi kuvunjika wala kuleta maafa makubwa.
Lakini wakati machafuko hayo yametokea siyoni wanawake,vyama vya siasa na vile vyama vya kiraia vikijitokeza kulaani vurugu hizi,wamekaa kimya utafikiri Zanzibar ikitokea maafa makubwa hawataathirika.Makundi hayo yamekuwa mabingwa ya kuchangia mada za kisiasa,ufisadi na maandamano lakini kwenye mambo kama haya yanayoatharisha usalama wa wenzetu kule Zanzibar wamekaa kimya.Inashangaza sana.
Napenda kuisa Idara ya Usalama wa Taifa(TISS), Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi(JWTZ), bila kufanya papara wachunguze kwa undani kuhusu chanzo cha vurugu hizo na mwisho wa siku waweze kubaini Je ni kweli hao viongozi wa jumuiya walifanya vurugu hizo kwa utashi wao au kuna watu wanawatumia kuanzisha vurugu hizo ili mwisho wa siku Zanzibar na Tanzania Bara tujikute tukingia kwenye vita ya udini na uzanzibari na utanzania Bara.
Maana tayari tumeishapata funzo toka kwenye nchi ambazo ziliwahi kukumbwa na vita,baadhi ya mataifa yenye fedha yalikuwa yakiwatumia baadhi ya wananchi wanayoishi kwenye taifa wanalokusudia kulisambaratisha au kumng’oa rais aliye madarakani kuleta chokochoko na mwisho wa siku wakafanikiwa. Na matokeo yake wanaokuja kuteseka ni sisi wakina mama na watoto.
Naamini mfumo wa upelelezi wa hapa nchini bado ni thabiti licha ya hivi sasa umekuwa ukikosolewa na wakosoaji kuwa umelegalega,ila binafsi naamini bado upo imara.
Mwisho nimalizie kwa kusema ni Jeshi la Polisi hapa Tanzania Bara na Zanzibar ndiyo wamekuwa wakivilea vikundi hivyo ambapo hapa Dar es Salaam, pale viwaja vya Bakhresa Manzese kila siku jioni ndiyo wamekuwa wakitoa miadhara na wakati mwingine mkihadhara hiyo imekuwa ikitoa maneno ya kukashifu dini ya Kiislamu au Kikristo na polisi wala hawachuki hatua kwani nakumbuka waandishi wa habari nikiwemo mimi miaka ya nyuma tulishaandika habari za kulitaka jeshi la polisi kudhibiti matamshi yanayotolewa katika mihadhara hiyo bila mafaniko. Na Wahenga walisema ‘Mazoea ujenga tabia’.
Mungu ibariki Tanzania ,Mungu Ibariki Afrika
0716 774494
www.katabazihappy.blogspot.com
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Juni 7 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment