VIONGOZI WA BAKWATA MMEKOSEA
Na Happiness Katabazi
TAYARI kuna baadhi ya Watanzania wenzetu ambao wameanza kuonyesha dalili ya kuichoka amani iliyopo hapa nchini hivyo sasa kila kukicha wanatamani kushuhudia machafuko ya kidini yakitokea hapa nchini.
Uenda wamefikia hatua ya kutamani hayo kwasababu uenda wamechoka kuona machafuko hayo kupitia kwenye Televisheni na kusikia kwenye redio yakitokeo kwenye nchi za wenzetu ambao zimekumbwa na machafuko yanayosababishwa na udini,ukabila na madaraka.
Nimelazimika kusema hayo kwasababu hivi karibuni tumeshuhudia viongozi wa Kikundi cha Uamsho kule Zanzibar wakileta machafuko kwa kuchoma kanisa na kuchoma moto maduka kwa kisingizio wanapinga Muungano lakini navishukuru sana vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vimeweza kuwashughulikia kimya kimya waasisi wa vurugu zile na ndiyo maana leo hii wale viongozi na wafuasi wa Kikundi cha Uamsho kimefyata mkia na hatuwasikii tena wakijinasibu kwenye vyombo vya habari.
Lakini Jumatano ya wiki hii tena tumelisikia Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na viongozi wa jumuiya za Kiislamu 31,walitangaza kulisusia zoezi la kuhesabu watu na makazi linalotarajia kufanyika Agosti mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Bakwata kwa niaba ya Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa bin Shaaban Simba, Amir Mkuu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu nchini, Musa Kundecha alisema waislamu hawakusikilizwa ndiyo maana wamesusia .
“Kama kukataliwa ni vyema basi tukataliwe sote,kwa kitendo cha Kanisa Katoliki kufanya sense na kuweka mitandaoni ni lazima pia watakuwa wanashirikiana na sense,hivyo basi kwa nini na wailasmu wasiruhusiwe hivyo”alisema Kundecha.
Wengi wetu tuliosikia kauli hiyo ya Bakatwa tulishtuka na kuanza kutafakari na kuanza kujiuliza maswali yafuatayo hivi sensa imeanza kufanyika kwa mara ya kwanza mwaka huu?
Mbona miaka yote huko nyuma serikali imekuwa ikiendesha zoezi la Sensa na Bakwata na jumuiya zake zilikuwepo lakini hatukuwahi kuzishuhudia zikijitokeza adharani kutangaza kususia sensa kwa kigezo kuwa serikali imekataa ombi lao la kutaka kipengele cha udini kiingizwe kwenye sensa?
Inaeleweka wazi kuwa lengo moja wapo la serikali kufanya sensa kwa wananchi wake ni kutaka kufahamu takwimu halisi la wananchi wake waliopo kwaajili ya kuwaletea maendeleo na kupanga mipango yake ya kimaendeleo hata kwa vizazi vijavyo.
Kamwe taifa lolote haliwezi kupanga mipango yake ya kimaendeleo au kuwaletea maendeleo wananchi wake kupitia maeneo wanayoishi bila kufahamu eneo fulani lina idadi ya wakazi wa ngapi kwahiyo hata kama serikali inataka kujenga hospitali katika eneo hilo basi itajenga hospitali ambayo itaweza kutumiwa na idadi fulani ya wakazi wa eneo hilo.
Sasa inashangaza kuona leo hii Bakatwa na hizo jumuiya zake zinajitokeza adharani na kuwataka waumini wa dini ya kiislamu wasusie sensa. Hivi tuiulize hii Bakwata na jumuiya zake zinaitii serikali ipi?
Maana kama kweli inaitii serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama sheria za nchi zinavyotutaka wanachi na taasisi zote zilizopo hapa nchini kuiitii serikali iliyopo madarakani, wasingetoa tamko la aina hiyo kwani tamko hilo walilolitoa ni wazi kabisa linaamasisha waamuni wa dini ya kiislamu wakatae agizo la serikali linalowataka wananchi wote wajitokeze kuhesabiwa katika zoezi la sensa.
Hivi mtu yoyote anayekaidi agizo lolote la serikali ,si sheria zinatueleza mtu au taasisi inayokaidi agizo la serikali anapaswa kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria?
Uenda Sheikh Kundecha wakati anatoa tamko hilo hakuwa hakifahamu madhara na uzito wa tamko hilo.Angefahamu madhara na uzito wa endapo tamko hilo litatekelezwa na waumini wake kama ni kweli kiongozi huyo wa dini ana uzalendo wa kweli na serikali yake asingethubutu kutoa tamko hilo.
Kwani tamko hilo linaweza kusababisha baadhi ya waumini wa kiislamu ambao wanawatii kikamilifu viongozi wao dini kweli wasusie sensa, watakuwa wamekwamisha malengo ya serikali ya kufahamu idadi sahihi ya wananchi wake.
Na kama serikali itapata takwimu zisizo sahihi za wananchi wake, mwisho wa siku serikali itajikuta ikitenga bajeti za kimaendeleo kwa takwimu zisizosahihi na matokeo yake wananchi wengine ambao walijitokeza kuhesabiwa nao watajikuta wakikosa au kupata mgao finyu wa kimaendeleo kwasababu ni wazi serikali itakuwa imetenga bajeti ya watu wachache lakini wakati mwisho wa siku watumiaji watakuwa wengi wakiwemo wale waliosusia sense.
Na hilo likitokea hiyo Bakwata na jumuiya zake itapata faida gani? Na mbona hiyo Bakwata haisemi wazi lengo hasa la kutaka kipengele cha udini kiingizwe kwenye sense?Maana serikali tayari imeshaweka wazi lengo la kufanya sensa kwa wananchi wote.
Hivi kwani Bakwata wakiamua kufanya sensa yao na ikishapata takwimu za waumini wao ikaziifadhi kwenye taasisi hizo kuna ubaya gani?Ni kwanini basi wanang’angania kipengele hicho cha udini kiingizwe kwenye sensa ya serikali?
Kundecha amenukuliwa akisema wao wamefikia uamuzi huo kwasababu wahawajasikilizwa ombi lao hilo.Hivi jamani kila anayewasilisha ombi lake kwa mamlaka husika ni lazima ombi hilo likubaliwe?
Kundecha amenukuliwa akisema haoni sababu ya serikali kugoma kuingiza kipengele cha dini ilhali wenzao wakristo (Kanisa Katoliki) wameruhusiwa kuingiza takwimu hizo mitandaoni bila kujulikana walikozipata.Tumuulize kiongozi huyo hivi Kanisa katoliki ndiyo waumini wote wa dini ya Kikristo hapa nchini?Jibu ni hapa. Na kama hivyo ndivyo hizo Takwimu za Kanisa Katoriki ndiyo imekuwa sensa ya Taifa au imebaki kuwa sensa ya kanisa hilo?
Ibara ya 19(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inasema “ Kazi ya kutangaza dini, ,kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi, na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi”.
Kwa maana hiyo ombi hilo la Bakwata kwa serikali linapingana na matakwa ya ibara hiyo.
Ikumbukwe kuwa taifa letu haliendeshwi kwa misingi ya kidini wala kikabila.Linaendeshwa kwa misingi ya sheria na Katiba hivyo ni vyema basi viongozi hao wa kidini na wale wa dini nyingine wakatambua kuwa Katiba na serikali kwa ujumla ina heshimu dini na imani za watu na ndiyo maana Ibara ya 19(1) ya Katiba imetoa uhuru wa mtu kuamini dini atakayo.
Leo hii serikali ikiiruhusu kuingizwa kipengele cha udini katika sensa, kesho kutwa na sisi watu wa kabila la Wanyambo tutaibuka na kushinikiza kipengele cha ukabili kiingizwe kwenye sensa ili sisi wanyambo tujifahamu tupo kiasi gani.Mwisho wa siku tutajikuta sasa tuanza kusigana katika udini na ukabila, ambao hautusaidii lolote katika taifa.
Kuna mambo mengi sana ya kimaendeleo viongozi wetu wa dini wanatakiwa wawe wanayasemea kwa kauli nzito ,lakini cha kushangaza hawayasemi wala kutoa maagizo mazito kama hayo.
Ningeona busara sana kama Kundecha na wenzake wangetangaza kuwataka waumini wao wenye umri wa kwenda shule ambao wazazi wao hawana huwezo wa kifedha wa kuwalipia ada,wajiorodheshe majina yao na wafike katika ofisi za Bakwata kwani tayari wameishawatafutia wafadhali wakuwasomesha,ningeona hilo ni jambo jema sana lenye manufaa kwa baadhi ya waumini.
Hivyo basi misioni haja ya leo hii ya viongozi wetu wa dini kuingia kwenye malumbano hayo ambayo ni wazi hayailetei tija taifa kwani hivi sasa wananchi wanachokitaka ni kuletewa maendeleo wao wenyewe na serikali yao .
Na taifa hivi sasa linashahuku ya kufahamu idadi mpya ya watanzania wanaishi hapa nchini ili waweze kuzitumia takwimu hizo katika shughuli mbalimbali.
Ikumbukwe kuwa kiongozi ni mtu anayepaswa kuwaongoza watu wake katika kufanya mambo fulani ili waweze kufikia mafanikio ya malengo waliyojiwekea sasa inapotokea baadhi ya kiongozi anashindwa kuwaongoza waumini au wafuasi wake kufikia maendeleo waliojiwekea ni wazi kiongozi huyo hatastahili kuendelea kuwa kiongozi.
Tayari tumeshuhudia nchi za wenzetu zikiingia kwenye machafuko yaliyosababishwa na udini, ukabila na ung’ang’aniaji wa madaraka na watu wakajikuta wakipoteza maisha ,sasa maagizo kama haya yanaweza kusababisha baadhi ya waumini wa kiislamu kuanza kuwachukia wakristo(Katoliki) na wakatoriki kuanza kuwachukia waislamu.
Hatutaki tufike huko na ninaamini ndugu zetu waislamu ambao tunaishi nao vizuri na kwa upendo na wanaofahamu nini maana ya kuhesabiwa watalipuuza agizo hilo lilotolewa na viongozi wao wa Bakwata.
Kwasababu siyo siri viongozi wao wa Bakwata hawana mvuto,ushawishi na huwezo wa kuwashawishi waislamu wote wakakubali kutekeleza agizo hilo lao la kususia sensa kwani kuna baadhi ya waislamu akiwemo Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais Dk.Mohamed Ghari Bilal ,watendaji wa Taasisi ya Takwimu ya Taifa na wale waumi wa kawaida wa dini wa kiislamu hawawezi kususia sensq kwani wameridhia lifanyike na hadi sasa wanaendelea kushiriki kikamilifu katika kuakikisha sensa inafanyika kwa umakini wa hali ya juu.
Mungu ibariki Tanzania,Mungu ibariki Afrika
0716 774494
Email:katabazihappy@yahoo.com
www.katabazihappy.blospot.com
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Juni 17 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment