Header Ads

VIONGOZI ACHENI TABIA HII

Na Happiness Katabazi BABA wa taifa aliwahi kusema ‘ukweli una tabia moja nzuri sana kwani auchagui rafiki wala adui’. Na kwa mara yingine leo nalazimika kutumia nukuu hilo kwasababu mada yangu nitakayoijadili leo kwa asilimia kubwa itagemea sana kuhusu suala zima la ukweli. Itakumbukwa kuwa Mei 29 mwaka huu, mwili wa gwiji la uendeshaji wa mashitaka nchini ambaye alikuwa na wadhifa wa Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha uendesha mashitaka na pia ndiye aliyekuwa Msimamizi mkuu wa uendeshaji kesi zenye maslahi kwa umma, Stanslaus Boniface Makulilo (44),uliagwa na kuzikwa katika nyumba yake ya milele pale katika Makaburi ya Kinondoni Dar es Salaam. Jamii ya wasomi wa fani ya sheria wakiwemo majaji,mahakimu, mawakili wa serikali na kujitegemea na wananchi wengine wa kada tofauti walishiriki katika mazishi mazishi hayo na wengi wao walikuwa na huzuni na wengine kushindwa kujizuia na kujikuta kila mara wakibubujikwa na machozi kutoka na majonzi ya kumpoteza gwiji hilo la mashitaka ambalo lililikuwa ni mwiba mkali,ambaye alikuwa akiisaidia kwa hali na mali kitaaluma mahakama kufikia maamuzi ya haki na aliyekuwa ametanguliza maslahi ya taifa kwanza. Binafsi niliudhulia msiba huu mwanzo hadi mwisho yaani kuanzia siku aliyokufa yaani Mei 27 alfajiri katika Hospitali ya Regency pale nyumbani kwa mdogo wa marehemu Dk.Alexander Makulilo tangu hadi siku Mei 29 siku tuliyoenda kumzika Boniface makaburi ya Kinondoni. Ni kweli mimi nimwandishi wa habari za kimahakama na nilikwenda msibani kwanza kama mfiwa kwasababu Boniface na mawakili wengine wa serikali na kujitegema kila siku tumekuwa tukifanya nao kazi pamoja,pia nilikwenda msibani pia kama mwandishi wa habari kwaajii ya kutazama na kurekodi matukio yote yaliyokuwa yakiendelea katika msiba huo ili niuabarishe umma. Ama kwa hakika kwa siku zote hizo miongoni mwa viongozi wa chache ambao nilikuwa nikiwashuhudia wakifika msibani hapo na wanakaa hadi usiku ni Mwanasheria Mkuu wa serikali Fredrick Werema na Naibu wake George Masaju ,Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Eliezer Feleshi,Mkuu wa Chuo cha Sheria(Law School) Gerad Ndika, aliyekuwa Mkuu wa Shule ya Sheria(UDSM),Profesa Paramaganda Kabudi ,Mbunge wa Kigoma Mjini,Peter Serukamba,maofisa wa jeshi la polisi ,waandishi wa habari za mahakamani mawakili wakujitegemea na wale wa serikali na kada nyingine na siku ya mazishi kule makaburini ndiyo Waziri wa Katiba na Sheria Mathias Chikawe alikuja. Kwanza naomba ieleweke wazi kuwa wale wote ambao hawakuhudhulia msiba wa Boniface hawajatenda kosa la jinai na wala siyo deni.Na pia kuzikwa na watu wengi siyo kwenda mbinguni. Lakini mimi binafsi na baadhi ya watu walioudhulia msiba huo tumebaki tukijiuliza ni kwanini viongozi wa juu kabisa wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais Dk.Mohamed Gharib Bilal,Waziri Mkuu Mizengo Pinda.Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,Nape Nnauye, Katibu Uenezi wa Chama Cha Demokrasi Chadema, john Mnyika na vyama vingine na vile vyama vya kiraia, wale wapambanaji wa ufisadi walishindwa kabisa kuudhulia msiba huo au hata kutuma salamu za pole kutokana msiba wa Boniface? Ieleweke wazi kuwa tangu Kikwete apishwe kuwa rais wa taifa hili Mei 21 mwaka 2005, serikali yake ndiyo imeandika historia ya kuwafikisha vigogo mahakamani kwa kesi mbalimbali na hatua hiyo ilitokana na kelele nyingi zilizokuwa zikipigwa na wananchi zilizotaka watuhumiwa wa ufisadi wa wizi wa fedha za EPA,Richmond,UDA,Shirika la Ndege(ATCL) wafikwe mahakamani haraka.Na walifikishwa mahakamani na DPP-Dk.Feleshi na Boniface na wenzake ndiyo waliokuwa wakiziendesha kesi hizo kwa nguvu zao zote hadi kufikia hatua ya kutishiwa usalama wao na watu wasiojulikana mara kwa mara. Ni huyu Rais Kikwete Pinda na huyo Nnauye na wabunge wengine wa ccm kwa mara kadhaa tumekuwa tukiwashuhudia katika majukwaani wakijinasibu kuwa serikali ya awamu ya nne imefanya mengi ikiwemo kuwafikisha mahakamani vigogo. Ni kweli serikali hiyo hilo imelifanya lakini cha kushangaza viongozi hao kupitia wasaidizi wao wameshindwa hata kuandika taarifa kwa umma kwamba wameupokeaje msiba huo.Ni ajabu sana. Uenda Boniface aina ya mchango wake kwa taifa hili ulikuwa hauthamini na hautiliwi maanani sana na makundi hayo kuliko mchango uliokuwa ukitolewa na watanzania wenzetu kama wasanii na wanasiasa waliotangulia mbele za haki ambao vifo vyao vilisababisha CCM na serikali yake vilijifanya kuonyesha kutaharuki hadi rais Kikwete,Dk.Bilal kwenda kwa zaidi ya mara mbili kwenye msiba mmoja.Katika msiba mmoja ambao sitalitaja jina la marehemu hao, Rais Kikwete na viongozi wenzake licha marehemu hao hata hawakuwa watumishi wa serikali waliofariki mwaka huu waliudhulia tena hadi usiku lakini viongozi hao wakashindwa kutenga hata siku moja kuja kuudhuria msiba wa Boniface. Niwe mkweli kabisa tabia hii imeanza kuwafanya baadhi ya watu kuamini kuwa viongozi wetu wa kisiasa wanachagua misiba ya kwenda.Wakifikiri msiba fulani kama wa Boniface ambao ulisheheni wasomi wa sheria hawatapa upenyo wa kujigenga kisiasa hawaudhurii wala kutoa salamu za pole na msiba fulani wakishapiga hesabu wakabaini wakiudhulia msiba huo watapata upenyo wa kujitangaza kisiasa basi haraka sana wanaudhuria msiba huo na kutoa salamu za pole. Hii ni tabia isiyopendeza na kukatisha tamaa watendaji hususani wale wa serikali ambao ni waadilifu na wachapakazi kwa viongozi hao kwani miongoni mwao waliniuma sikio msibani wakisema msiba wa Boniface ndiyo ungekuwa ni msiba wa msanii basi Ikulu ingeamia katika msiba huo na kutoa misaada mingi.Kauli kama hizi hazipendezi kwani zinaonyesha kutolewa na wafanyakazi wa serikali walioanza kukatishwa tamaa na viongozi wao.Badilikeni. Hivi katika hali ya kawaida leo nyie viongozi hao nyie vyama vya upinzani,CCM na wanaharakati na nyie baadhi ya wabunge mliokuwa mmejipambanua kupambana na ufisadi mnaweza kuwa na jeuri ya kusimama majukwaani na kutuleeza nini kuhusu kesi za ufisadi, wakati hata kutoa salamu za pole kwa marehemu Boniface aliyekuwa akiongoza dawati la kuendesha kesi zilizokuwa na maslahi ya umma mmeshindwa?Kutwa kutoa matamko kuhusu ufisadi, maandamano na kupikiana majungu na kufukuzana kazi na kusuka makundi ya kugombea urais mwaka 2015. Ndiyo maana kuna baadhi ya majaji ,maofisa wa serikali waliniuma sikio wakiambia kuwa miongoni mwao muda mrefu walichaacha kuudhulia sherehe za kitaifa kwani wao wakifa vingozi hao wa juu wa serikali hawaudhulii madhishi yao. Boniface alipenda sana kazi ya Uwakili wa Serikali na hasa kuendesha mashtaka.Alikuwa tayari kuendesha kesi yoyote bila woga.Alikuwa msaada kwa mahakama katika kufikia maamuzi ya haki. Hii inadhiirika kwa kusoma hukumu na maamuzi ya mahakama ya mashauri ambayo aliiwakilisha serikali. Mfano mzuri ni hukumu ya Mahakama ya Rufaa Na. 250/2006 katika kesi ya Silivester Hillu Dawi na wenzake dhidi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ambapo jaji Edward Rutakangwa alimwelezea Boniface aliyekuwa akiiwakilisha serikali katika shauri hilo kuwa ni mkweli na mpenda haki. Jaji Rutakangwa aliweka kanuni ya washitakiwa wanaokabiliwa na shitaka kuchangia nusu ya thamani ya mali inayohusika shtaka husika ili kupata dhamana badala ya kila mshitakiwa kutoa nusu ya thamani hiyo. Kesi nyingine ni ya Mwenyekiti wa Timu ya Simba, Ismail Aden Rage dhidi ya Jamhuri katika Mahakama ya Rufaa Na. 286/2005, ambapo Jaji Mroso alieleza wazi kuwa Jamhuri iliyokuwa ikiwakilishwa na Boniface,ilikuwa imewakilishwa na mtu mwenye uwezo na msaada pale alipotamka. Kwa hukumu hizo mbili,ni wazi zimeuthibitishia umma kuwa hata Mahakama ya Rufaa Tanzania ilikuwa ikiheshimu na kumtambua Boniface kuwa ni wakili mahiri wa serikali.Na sisi watu tunaofikiri sawa sawa na wale wasomi wa sheria tutaendelea kuuenzi mchango wa marehemu na kumkumbuka daima katika tasnia ya sheria nchini. Mungu ailaze roho ya Boniface mahali pema peponi.Amina. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika 0716 774494 www.katabazihappy.blogspot.com Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Juni 3 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.