MAHALU ANA HATIA-SERIKALI
Na Happiness Katabazi
UPANDE wa Jamhuri katika kesi wizi wa Euro milioni mbili inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Grace Martin wamiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, iwaone washitakiwa hao wana hatia kwa sababu washitakiwa wameshindwa kuleta ushahidi mathubuti ambao unaonyesha hawakutenda makosa hayo.
Ombi hilo la upande wa Jamhuri limewasilishwa kwa maandishi na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Ben Lincoln na mawakili wa serikali Vicent Haule na Ponsian Lukosi ikiwa ni utekelezaji wa amri ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Ilvin Mugeta aliyoitoa kwa pande zote katika kesi hiyo Mei 16 mwaka huu, ambapo alizitaka pande zote ziwasilishe maombi hayo ya kuwaona washitakiwa wana hatia au la.
Kwa mujibu wa ombi hilo la upande wa Jamhuri ambalo gazeti hili inayo nakala yake, wakili Lincoln anaiomba mahakama hiyo iwakute na hatia washitakiwa wote wawili yaani Mahalu na Grace Martin kwasababu upande wa jamhuri umeweza kuleta mashahidi saba, vielelezo ambavyo ni nyaraka mbalimbali ambavyo vimethibitisha washtitakiwa hao wanaokabiliwa na makosa sita ilikiwemo kosa la kula njama, wizi wa Euro milioni mbili ,kugushi vocha za manunuzi ya jengo la Ubalozi,kutumia risiti za manunuzi kuidanganya serikali,kuisababishia serikali hasara ya Euro milioni tatu kuwa walitenda makosa hayo.
Wakili Lincoln alidai kuwa wakati Mahalu akitoa utetezi wake alishindwa kutoa ushahidi mbadala ambao ungeonyesha ni kweli serikali ya Tanzania ilimruhusu anunue jingo la Ubalozi kwa njia ya mikataba miwili na kwa maana hiyo ameshindwa kuipangua hoja ya upande wa jamhuri ambayo inadai kuwa serikali haikuwa ikifahamu wala haikumpa idhini Mahalu ya kununua jengo hilo kwa njia ya mikataba miwili kitendo ambacho kina kwenda kinyume na Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2001 ambayo inakataza mali yoyote ya serikali isinunuliwe kwa njia ya mikataba miwili na endapo kutakuwa na ulazima wa kununua mali ya serikali kwa njia mikataba miwili ni lazima ipatikane kwanza idhini toka katika mamlaka husika.
Wakili Lincoln alidai kwa mujibu wa shahidi wa pili wa upande wa Jamhuri ambaye ni wakili wa Italia ambaye ndiye asiyesaini mkataba wa manunuzi wa jengo hilo Marco Papi ambao mkataba huo ulionyesha jengo hilo lilinuliwa kwa thamani ya Euro milioni moja na kwamba huo mkataba ndiyo unatambuliwa kisheria na ule mkataba wa pili ambao unaonyesha jengo hilo limenunuliwa kwa jumla ya thamani ya Euro milioni tatu autambuliki kisheria na endapo mtu atanunulia kitu au jengo kwa mtindo wa mikataba miwili serikali ya Italia itamhesabu mtu huyo amekwepa kodi.
“Na katika utetezi wao washitakiwa hao wawili wameshindwa kutoa ushahidi mbadala unaopinga ushahidi huo wa Papi pamoja na kutoa vielelezo vinavyoonyesha mamlaka au sheria za Tanzania ziliwaruhusu kutenda tendo hilo la kununua jengo hilo kwa njia ya mikataba miwili na kwa sababu hiyo ndiyo maana tunaiomba mahakama iwaone wanahatia”alidai wakili Lincoln.
Wakili Lincoln akiuchambua ushahidi wa shahidi wa pili wa upande wa utetezi, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ,wakili huyo alidai Mkapa alieleza kuwa yeye aliruhusu jengo hilo linunuliwe na kwamba malipo yalipwe kupitia akaunti mbili tofauti lakini Mahalu alishindwa kumweleza Mkapa kuwa jengo lile litanunuliwa kwa njia ya mikataba miwili.
“Kwa sababu hizo tulizozitaja hapo juu, tunaiomba mahakama hii tukufu iwaone washitakiwa hao wanatia na iwahukumu vifungo kama sheria inavyosema na wairudishie serikali jumla ya Euro milioni mbili ambazo waliziiba kwa kisingizio cha kununua jengo la ubalozi kwa njia ya mikataba miwili”alidai Lincoln”alidai Lincoln.
Kesi hiyo itakuja kutolewa hukumu na Hakimu Mfawidhi Mugeta, Julai 11 mwaka huu.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Julai 13 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment