HUKUMU KESI YA ARCADO NTAGAZWA OKTOBA 17, 2013
Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi
Kisutu Dar es Salaam, imesema Oktoba 17 mwaka huu, ndiyo siku itakayotoa hukumu
ya kesi ya kujipaia kofia ,fulana zenye jumla ya thamani ya Sh.milioni 74.9 kwa
njia ya udanganyifu inayomkabili Waziri wa zamani Arcado Ntagazwa na wenzake.
Hayo yamesemwa na Hakimu
Mkazi Gene Dudu muda mfupi baada ya wakili wa utetezi Alex Mushumbusi kuiambia
mahakama upande wa utetezi umefungua utetezi baada ya washitakiwa wote kumaliza
kujitetea.
Hakimu Dudu alisema baada ya
washitakiwa wote kumaliza kujitetea anautaka upande wa jamhuri na utetezi
kuwasilisha kwa maandishi majumuisho yao ya mwisho ya kuiomba mahakama iwane
washitakiwa wana hatia au la Oktoba 3 mwaka huu, na kwamba hukumu ya kesi hiyo
ataitoa oktoba 17 mwaka huu.
Mbali na Ntagazwa ,
washitakiwa wengine ni mtoto wa Ntagazwa, Dk. Webhale Ntagazwa na mshitakiwa wa
kwanza Senetor Mirelya (60) alishamaliza kutoa utetezi wake.
Aprili 23 mwaka 2012,
ilidaiwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Ladslaus Komanya kuwa Oktoba 22 mwaka 2009 huko Msasani
Mikoroshini washtakiwa hao kwania ovu walijipatia fulana 5000 na kofia 5000
zenye jumla ya thamani ya Shilingi milioni 74.9 toka kwa Noel Sevele kwa
makubaliano kuwa wangemlipa Sevele kiasi hicho cha fedha katika kipindi cha
mwezi mmoja tangu walipochukua vifaa hivyo lakini hata hivyo walishindwa
kumlipa na washtakiwa walikana shtaka na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado
haujakamilika.
Ntagazwa ambaye kwa sasa ni Kada
wa Chadema , kabla ya kujiunga na chama hicho miaka minne iliyopita, akitokea
chama cha Mapinduzi (CCM).Akiwa mwanachama wa CCM, aliwahi kuteuliwa na rais wa
Serikali ya awamu ya pili na ya tatu, Ally Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa
kushika nyadhifa za uwaziri katika wizara mbalimbali hadi ilipofika mwanzoni
mwa mwaka 2006, Rais Jakaya Kikwete alipounda baraza lake jipya la mawaziri na
kuamuacha nje ya baraza hilo.
Ntagazwa ambaye aliwahi kuwa
mbunge wa muda mrefu wa Jimbo la Mhambwe kwa tiketi ya CCM, hadi sasa
nakumbukwa kwa msemo wake mmoja maarufu aliowahi kuutoa bungeni akiwa Waziri
Nchi ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira alisema ‘Ipo siku
wajukuu zetu watafukua makaburi yetu wachunguze ubongo wetu kama tulikuwa na
akili timamu’. Ntagazwa alitoa msemo huo kutokana na kutoridhishwa na baadhi ya
maamuzi yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya watendaji waliopewa dhamana.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Septemba 25 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment