Header Ads

VURUGU ZALINDIMA MAHAKAMA YA KISUTU




Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilikuta ikipata taharuki kufuatia patashika iliyotokea baina ya askari polisi na waliokuwa washitakiwa wanne katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha iliyokuwa ikimkabili Fredy Peter ‘Chege’ na wenzake wanne ambao walikuwa wakipambana na polisi ili waweze kutoka chini ya ulinzi warejee uraini kwasababu mahakama ilikuwa imewaachiria huru.

Vurugu hizo zilizodumu kwa dakika 15 zilitokea jana saa tano asubuhi ndani ya selo ya mahakama hiyo ikiwa ni dakika chache baada ya Peter na Hakimu Chilumba ‘Chinga’,Boniface Steven ‘Bukuku’,Nsajigwa Steven ‘Bukuku’ waliokuwa wakikabili na kesi Na.128/2013 ya unyang’anyi wa kutumia silaha kinyume na kifungu cha  287 A  cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 ambayo haina dhamana ambayo ilifunguliwa rasmi mahakamani hapo  Julai 30 mwaka huu.

Kesi hiyo ambayo jana ilikuja kwaajili ya kutajwa ambapo hakimu Nyigulila Mwaseba alisema Septemba 12 mwaka huu, mshitakiwa wa nne aliambia mahakama kuwa kesi hiyo waliyoshtakiwa nayo katika mahakama hiyo ni kesi inayofanana ambayo walifutiwa kesi ya shtaka linalofanana na kesi iliyombele yake  ambayo ilifutwa na  hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Kalli, Julai 29 mwaka huu , na hivyo akaiomba mahakama yake iwafutie kesi hiyo  na iwaachiri huru na kwamba siku hiyo mahakama yake ilimtaka mshitakiwa huyo alete nakala ya uamuzi wa mahakama ya Temeke unaonyesha mashitaka yaliyofutwa katika mahakama ya Temeke yanafanana na yaliyofunguliwa katika mahakama ya Kisutu.

Hakimu Mwaseba alisema washitakiwa hao walileta nakala ya uamuzi huo  uliotolewa na hakimu wa wilaya ya Temeke Julai 29 mwaka huu, ambapo Hakimu Kalli katika nakala ya uamuzi wake ambao gazeti hili limefanikiwa kuiona nakala hiyo, hakimu Kalli alisema anawafutia washitakiwa kesi hiyo chini ya kifungu cha 98B cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 licha washitakiwa watatu walikuwa wameishatoa utetezi wake na siku hiyo kabla ya kuifuta kesi hiyo ilikuja kwaajili ya mshitakiwa wa nne aanze kujitetea lakini wakili wa serikali aliwasilisha ombi mahakamani hapo la kuomba kuwafutia washitakiwa wote kesi hiyo chini ya kifungu chja 91(1)  cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, ombi ambalo lilikubaliwa na hakimu huyo na akaawachiria huru washitakiwa hao.

“Nimeridhika nakala hiyo ya uamuzi wa mahakama ya Temeke na nakala hiyo inaonyesha wazi shitaka waliloshtakiwa nayo Temeke na wakafutiwa na mahakama baada ya upande wa jamhuri kuona hawana haja ya kuendelea kuwashitaki na shitaka hilo hilo ndilo wameshitakiwa nalo katika mahakama hii ya kisutu…kwa kauli moja mahakama yangu inasema haina mamlaka ya kusikiliza kesi hii na inawaachiria huru washitakiwa wote”alisema Hakimu Mwaseba.

Baada ya kuwaachiria huru askari magereza waliwarudisha sero ya mahakamani hapo na washitakiwa walipokuwa wanataka kutoka mikononi mwao ,askari polisi waliwadaka huku waliokuwa washitakiwa hao wakibambana na polisi ili waweze kutoka mikononi mwa polisi hali iliyosababisha polisi kujaa kwa wingi ndani ya sero hiyo na kuanza kupambana na waliokuwa washitakiwa hao kwa kuwapiga na kuwazuia wasitoke ndani ya sero hiyo huku washitakiwa wakipiga may owe na kuangua vilio kwa sauti ya juu hali iliyosababisha taaruki mahakamani hapo na baadhi ya askari polisi wakiwalaumu askari polisi wenzao walioenda kuwakamata watu hao kwa madai kuwa huo ni uonevu wa hali ya juu na kwamba kuna watuhumi wangapi wanakesi kubwa wameachiliwa huru na mahakama lakini polisi hao hawawakamati.

“Polisi mmetubambikia kesi, na hao mawakili wa serikali ndiyo hao hao waliotufungulia kesi na kisha wakatufutia na mahakama ikatuachia kule Temeke na muda mfupi baada ya kuachiwa na mahakama ya Temeke askari mmoja akatukamata akatupeleka mahakama ya Kisutu na kisha kutushitaki kwa kosa lilele….huu ni uonevu wa hali ya juu na ni matumizi mabaya ya muda wa mahakama na kutunyanyasa…..tuachieni tutoke kwanza nyie polisi mnatuzuia tusitoke wakati hata hamjui kesi huko mahakamani leo kimeamriwa kitu gari…tumechoshwa na uonevu tuachieni’alisikika mmoja wao ambaye alichaniwa shati katika vurugu hizo baina yao na askari polisi.

Hata hivyo polisi walifanikiwa kuwadhibiti waliokuwa watuhumiwa hao na kisha kuwaweka selo na hadi gazeti hili linaondoka mahakamani hapo ,haikuweza kujulikana mara moja watafunguliwa mashitaka gani mengine.

Julai 31 mwaka huu, ilidaiwa mahakamani hapo na wakili wa serikali kuwa washitakiwa huo kuwa Desemba 1i 5 mwaka 2012  huko eneo la Zanapa huko Temeke, waliiba simu mbili za mkononi aina ya Nokia  zenye thamani ya Sh. 300,000, waleti yenye thamani ya Sh 200,000, pochi moja ya mkononi yenye thamani ya Sh. 150,000 na saa ya mkononi yenye thamani ya Sh, 180,000 .vitu vyote vyenye thamani ya Sh.1,470,000 mali ya  John Luanda na kabla ya kujipatia vitu hivyo  walimkata kwa Panga ,Luanda na washitakiwa walikanusha mashitaka hayo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Septemba 17 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.