SHAHIDI AZIDI KUMCHOMOA MRAMBA KWENYE KESI
Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imeelezwa kuwa mwaka 2002 wakati Benki Kuu ya Tanzania kwaniaba ya serikali inaingia mkataba na kampuni ya Alex Stewart ya kukagua dhahabu nchini, Tanzania ilikuwa haifahamu nchi ina kiasi na thamani gani ya dhahabu hapa nchini.
Hayo yalielezwa jana na shahidi anayemtetea aliyekuwa waziri wa Fedha, Basil Mramba,Clecensia Mbatia mbele ya jopo la majaji watatu John Utamwa, Sam Rumanyika na Hakimu Mkazi Saul Kinemela wakati akijibu swali aliloulizwa na Hakimu Kinemela kuwa ni kwanini Timu ya majadiliano ya kuitafuta kampuni hiyo ilipendekeza kampuni hiyo ichukue asilimia 1.9 ya dhahabu yote atakayoikagua wakati serikali wakati huo ilikuwa haifahamu Tanzania ina kiwango gani cha dhahabu.
“ Waheshimiwa majaji, Marehemu Daud Balali ndiye aliyeteua kamati yetu ya kutafuta kampuni ya kukagua dhahabu na mwisho wa siku tukaipata kampuni ya Alex Stewart…na tulipoipata kampuni hiyo ilitaka ilipwe asilimia 1.9 ya dhahabu yote ambayo watakuwa wameishaikagua…sisi kama Kamati asilimia hiyo hatukufurahishwa nayo kwani tuliona ni asilimia kubwa sana na tulimweleza Gavana kuwa sisi timu yetu inapendekeza kampuni hiyo ilipwe asilimia 1.8 ndani ya miaka miwili lakini kampuni hiyo ilikataa pendekezo letu na kusema ingekubalina na bei ya asilimia 1.8 endapo serikali ingekubali kuingia nao mkataba kwa miaka mitano…..na gavana mwisho wa siku alisema kwakuwa jambo hilo ni la haraka sana mkataba usainiwe kwa kampuni hiyo ilipwe asilimia 1.9 ya dhahabu yote watakayokuwa wameikagua na wakati huo dhahabu iliyopo nchini ilikuwa haijulikani ipo kiasi gani hivyo kampuni hiyo ilikuwa ni ya kwanza kuanza kufanya kazi hiyo ya ukaguzi hapa nchini”alidai
Mbatia.
Akijibu maswali aliyokuwa akihojiwa na mawakili waandamizi wa serikali Shadrack Kimaro na Oswald Tibabyekomya alieleza kuwa kila jambo lilokuwa likifanywa na timu yake na nyaraka zote za kufanikisha mchakato wa kuitafuta kampuni hiyo walikuwa wakizepeleka BoT kwa gavana hivyo nyaraka zote kuhusu mchakato huyo kama zinatafutwa basi wakuulizwa na BoT.
Mbatia alidai kuwa wakati wakiendesha mchakato huo wa kutafuta kampuni hiyo na hatimaye kufanikisha kuipata, timu yake haikutangaza tenda ya kutafuta kampuni hizo kwani Gavana ndiye aliyeiteua timu yake na katika majukumu ya timu hiyo halikuwepo jukumu la kutangaza tenda ya kupatikana makampuni hayo na kwani wakati huo wa mwaka 2002 ,Sheria ya Manunuzi ya Umma ilikuwa haipo na kwani sheria hiyo ilitungwa mwaka 2004 .
Aidha akijibu swali la wakili wa Mramba, Hurbbet Nyange, lilokuwa likimuuliza kuwa gavana wa Benki Kuu anayomamlaka ya kusamehe kodi kampuni ,Mbatia alijibu kuwa hana mamlaka hayo na kwamba BoT ndiyo iliingia mkataba na kampuni hiyo kwaniaba ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jaji Utamwa alisema shahidi huyo amemaliza kutoa ushahidi wake na kwamba anaiarisha kesi hiyo hadi leo ambapo shahidi wa tatu wa Mramba ambaye juzi na jana alifika mahakamani hapo kwaajili ya kutoa ushahidi wake bila mafanikio kwasababu ya ufinyu wa muda wa mahakama, hivyo leo anatarajiwa kaunza kutoa ushahidi wake.
Mbali na Mramba washitakiwa wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Daniel Yona na Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Fedha Gray Mgonja ambao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Nyange, Elisa Msuya na Profesa Leonard Shaidi .
Novemba 2008 ilidaiwa mahakamani hapo na mawakili wa upande wa jamhuri kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa ya matumuzi mabaya ya madaraka na kuisasababishia serikali hasara ya Sh.bilioni 11.7.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa Septemba 20 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment