MKENYA WA DK.ULIMBOKA JELA MIEZI SITA
Na
Happiness Katabazi
HATIMAYE
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imemhukumu kwenda jela miezi
sita au kulipa faini ya Sh.1,000 ,raia wa Kenya, Joshua Mulundi ambaye
alikuwa akikabiliwa na kosa moja la kutoa taarifa za uongo kwa ofisa wa polisi
katika Kituo cha Polisi Oystebay ambapo
alimweleza ofisa huyo wa polisi yeye na wenzake ambao waliokodiwa kwenda
kumteka na kumjeruhi Dk.Steven Ulimboka.
Hukumu
hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Alocye Katemana alisema kesi hiyo ilikuja jana kwa ajili ya upande
wa jamhuri kumsomea maelezo ya awali mshitakiwa huyo ambapo Wakili Mwandamizi wa Serikali Tumaini
Kweka alimsomea maelezo ya awali mshitakiwa
na baada ya kumaliza kusomea maelezo hayo , mshitakiwa huyo alikiri
kutenda kosa hilo la kutoa taarifa za uongo polisi kinyume na kifungu cha 122 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu
ya mwaka 2002.
Kabla
ya Hakimu Katemana kutoa adhabu yake aliutaka upande wa jamhuri uzungumze
lolote kama wanalo, ambapo wakili Kweka alidai kuwa anaiomba mahakama itoe
adhabu inayostahili kwasababu kwa mazingira ya kesi hiyo , hali iliyojengeka
katika jamii kuhusu sakata la kutekwa na kuteswa kwa Dk.Ulimboka ni tetete na
kwamba ni kwamba si vyema kwa mtu mzima kama mshitakiwa kwenda kutoa taarifa za
uongo polisi ambazo zilipelekea jamii kuwa na hisia tofauti kuhusu utekwaji wa
Dk.Ulimbo na kuomba mahakama itoe adhabu kali.
Aidha
kwa upande wake Mulundi alieleza kuwa yeye ni raia wa Kenya na kwamba lengo na
madhumuni ya kuja Tanzania, ni kuja kufanyabiashara ya kuuza nguo. Juni 27 mwaka jana akiwa Arusha, alitekwa na mtu
asiyemfahamu na wakati ametekwa huyo mtu alimwamuru afanye kila jambo
atakalomtaka alifanye na kwamba yeye alikubali kufanya yote aliyokuwa akiamriwa
na mtu huyo ambaye alikuwa akimpa maelekezo huku akiwa ameshika silaha.
“Mheshimiwa
hakimu kwa kuwa nilikuwa naogopa vitisho
hivyo nilifanya kama alivyokuwa
akinielekeza na baadae mtu huyo aliyekuwa ameniteka akanipeleka hadi Tanga,
sehemu ambayo sikuwa nimewahi kufika na kwamba mtu huyo akanieleza kuwa yeye ni
mkristo na kwamba ananituma kwa mkristo mwenzie
na akanipa taarifa hizo nizipeleke kwa mkristo mwenzake na taarifa hizo ndizo zilizosomwa hapa
mahakamani na mwendesha mashitaka wakati akinisomea maelezo ya awali.
“Nilienda
hadi katika kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo Kawe Tanganyika Parkers na kumkuta mchungaji Joseph Marwa Kiliba
ambaye yule mtekaji aliniambia nimfikishie taarifa hizo na nilimfikishia kwani
nilikuwa naogopa vitisho vile kwani yule mtekaji aliniambia endapo sitafikisha
zile taarifa za ungamo langu niloungama polisi na kwa mlinzi wa amani atapewa
taaarifa kwani huyo mchungaji ni mtu wao pia . Nikampatia taarifa zile kama
nilivyoelekezwa baada ya hapo nikajikuta nakamatwa na pelekwa kituo cha polisi
Oystebay kishwa kwa mlinzi wa amani katika Mahakama ya Mwanzo Kawe ambapo
nilitoa taarifa hizo ambazo mwisho wa siku zilisababisha nifunguliwe kesi hii
ya kutoa taarifa za uongo”alidai Mulundi.
Mapema
jana asubuhi wakili Kweka akimsomea maelezo ya awali mshitakiwa huyo, alidai
kuwa mshitakiwa ni Raia wa Kenya na kwamba alifika katika kanisa na Ufufuo na
Uzima Kawe , mbele ya mchungaji
Kiliba na kuungama na kusema kuwa
yeye na wenzake ambao hawapo mahakamani ndiyo waliousika kumteka na kumtesa
Dk.Ulimboka na kisha kwenda kumtupa katika Msitu wa Magwepande Dar es Salaam.
Baada
ya kumaliza kuungama mbele ya mchungaji huyo, Mulundu alijikuta akikamatwa na
wanausalama na kupelekwa kituo cha polisi Oystebay mbele ya Sajenti Nyagea
ambapo mshitakiwa huyo mbele ya askari huyo alisema kuwa yeye ndiye
aliyeusika kumteka na kumtesa Dk.Ulimboka na baada ya hapo askari polisi huyo
alimpeleka Mulindi kwa mlinzi wa amani katika mahakama ya mwanzo Kawe na
mshitakiwa huyo alikiri kutenda kosa hilo.
Akitoa
adhabu yake baada ya kusikiliza maombi ya pande zote mbili Hakimu Katema
alisema kwakuwa mshitakiwa amekiri kosa kabla hata mashahidi wa jamhuri
hawajaletwa kuja kutoa ushahidi wa kesi hiyo, mahakama yake inamhukumu kwenda
jela miezi sita au kulipa faini ya Sh.1,000. Hata hivyo Mwandishi wa habari wa
Redio Times, Chipangula Nandule aliyekuwepo mahakamani hapo alijitolea
kumlipia faini hiyo ya Sh.1,000 na sekunde chache baadaye askari polisi
walimkamata Mulundi na askari hao kwa masharti ya kutotajwa majina yao gazeti
kwa maelezo kuwa wao siyo wasemaji wa jeshi, walisema kuwa Mulundi ni raia wa
Kenya, hivyo wanamshikilia ili waweze kuandaa taratibu za kumrejesha nchini
kwao Kenya.
Agosti
6 mwaka huu, Mkurugenzi wa Mashitaka
nchini(DPP), Dk.Eliezer Feleshi alimfutia kesi ya kujaribu kumuua na kuteka
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini Steven Ulimboka, raia wa Kenya Joshua
Mulundi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, baada ya kuona
hana haja kuendelea kumshitaki kwa makosa hayo ambayo yalikuwa hayana dhamana
na kisha siku hiyo akamfungulia kesi mpya ya kutoa taarifa za uongo Polisi.
Wakili
Kweka mbele ya Hakimu Katema alimsomea shitaka hilo mshitakiwa ambapo Julai 3
mwaka jana, katika Kituo cha Polisi Oystebay mshitakiwa huyo alitoa taarifa za
uongo kwa ofisa wa polisi ambapo alimweleza ofisa huyo wa polisi yeye na
wenzake ambao waliokodiwa kwenda kumteka na kumjeruhi Dk.Ulimboka jana ambalo
si kweli kosa ambali ni kinyume na kifungu cha 122 cha Sheria ya Kanuni ya
Adhabu ya mwaka 2002 na kuongeza kuwa upelelezi wa kesi hiyo mpya umekamilika.
Wakili
Kweka alidai licha kosa hilo lina dhamana kwa mujibu wa sheria lakini upande wa
jamhuri unaomba asipewe dhamana kwaajili ya usalama wake,kesi hiyo ina maslahi
kwa taifa hoja ambayo ilimlazimu hakimu Katemana aairishe kesi hiyo kwa muda na
kisha kuutaka upande wa jamhuri uende ukalete kwa maandishi hati ya kumfungia
dhamana mshitakiwa huo.
Julai
13 mwaka 2012, Mulundi (21), alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya
kwanza akikabiliwa na makosa mawili, kosa la kwanza ni la kutaka kuua
Dk.Ulimboka na kosa la pili ni la kumteka,ambapo makosa hay ohayo kwa mujibu wa
sheria hayana dhamana na yanasikilizwa na Mahakama Kuu peke yake na kwamba
mahakama ya Kisutu ilikuwa haina mamkala ya kusikiliza kesi hiyo hiyo na hivyo
kusababisha kukaa gerezani tangu siku hiyo.
Wakili
wa serikali, Ladslaus Komanya, mbele ya Hakimu Agnes Mchome, alidai kuwa
Mulundi ambaye mkazi yake ni Murang’a nchini Kenya, anadaiwa kuwa Juni 26
mwaka jana, akiwa eneo la Leaders Club alimteka Dk. Ulimboka.
Katika
shtaka la pili, Komanya alidai kuwa Juni 26 mwaka huu, akiwa katika eneo la
Msitu wa Mwabepande Tegeta, Dar es Salaam, kinyume cha sheria, mshtakiwa huyo
alijaribu kumsababishia kifo Dk. Ulimboka.
Hakimu
Mchome alisema mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo
haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, kwani Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka
ya kusikiliza kesi hiyo.
Juni
27 mwaka 2012, Dk. Ulimboka aliokotwa na msamalia mwema katika msitu huo wa
Mwagwepande akiwa amejeruhiwa vibaya na kisha akafikishwa katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili akiwa na maumivu makali na kuanza kutibiwa na kisha
kupelekwa afrika Kusini kwaajili ya matibabu zaidi na kisha kurejeshwa nchini
akiwa amepona.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Oktoba Mosi mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment