Na Happiness Katabazi
 
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,jana ilishindwa kusikiliza utetezi wa aliyekuwa Kaimu Mhariri Mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communication, Theophil Makunga kama ilivyokuwa imepangwa kwasababu mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo ambaye alikuwa ni mhariri Mtendaji wa gazeti la Tanzania Daima ,Absalom Kibanda amekwenda Afrika ya Kusini kwaajili ya matibabu.
 
Wakili wa Serikali Inspekta Hamis  mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema aliikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo ya kuchapisha makala ya uchochezi ilikuja kwaajili ya kuendelea kwa washitakiwa kujitetea hivyo haitawezekana kwasababu Kibanda na wakili wa serikali Prosper Mwangamila hawapo na Mwangamila  yupo safarini kikazi.
Hakimu Lema aliarisha kesi hiyo hadi Oktoba  23 mwaka huu, kwaajili ya washitakiwa kuendelea kuitetea.
Katika hatua nyingine ,kesi ya wizi wa Sh.bilioni sita inayowakabili ndugu wawili Johnson Lukaza na Mwesigwa Lukaza jana ilijatajwa na kuarishwa hadi  Oktoba 23 kwa sababu jarada la kesi hiyo limeitwa Mahakama Kuu.
 
Wakati huo huo  mahakama hiyo imeairisha kesi ya kukutwa na simu gerezani inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba hadi Oktoba 16 mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Septemba 24 mwaka 2013.