Header Ads

MKE NA MUME JELA KWA FEDHA ZA EPA

Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imewahukumu kwenda jela miaka tofauti wafanyabiashara  watatu waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya wizi wa Sh.bilioni 1.1 katika akaunti ya Madeni ya Nje(EPA), katika Benki Kuu ya Tanzania, baada ya kuwakuta na hatia katika makosa mbalimbali likiwemo kosa la kughushi hati ya kuamisha deni toka kampuni ya Kampuni ya Marubeni ya Japan kwenda kampuni ya Changanyikeni Residential Complex ya nchini.
Hukumu hiyo ya kesi hiyo ya jinai Na.1158/2008 iliyokuwa ikimkabili Bahati Mahenge, Manase Makalle,Davis Kamungu, Geofrey Mosha na Edda Mwakale ambaye ni mke wa mshitakiwa wa pili(Manase).
Hukumu hiyo ilitolewa na jopo lilokuwa likiongozwa na Jaji Sekela Mushi, Jaji Sam Rumanyika na Hakimu Mkazi Lameck Mlacha na ilisomwa kwaniaba yao na Mlacha.

Hakimu Mlacha alisoma hukumu hiyo kwa kuanza kuikumbusha mahakama kuwa hati ya mashitaka  ilikuwa na jumla  ya mashitaka tisa na kwamba kosa la kwanza ni la kula njama kinyume na kifungu cha 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002  kwamba washitakiwa hao walitenda kosa hilo la kula njama kati ya Desemba 23 mwaka 2003 na  Oktoba 26 mwaka  2005 ,kuwa washitakiwa na watu wengine ambao hawapo mahakamani walitenda kosa hilo na kuiibia BoT , na kwamba   kosa hilo lilikuwa likiwakabili washitakiwa wote.

Hakimu Mlacha alisema baada ya kupitia ushahidi na vielelezo vyote mahakama yake inamshia hatiani mshitakiwa wa kwanza na wa pili(Mahenge na Manase) katika kosa la kwanza ambapo na kwamba mahakama inawaachulia huru washitakiwa wengine katika kesi hiyo kwasababu hakuna ushahidi wa kuonyesha walitenda kosa hilo na kwamba washitakiwa watakwenda jela miaka mitano.
Hakimu Mlacha alililitaja kosa la pili kuwa ni la kuwasilisha nyaraka za kutaka kampuni yao ya Changanyikeni isajiliwe na Brela  na kwamba katika nyaraka hizo walionyesha  jina la kufikirika la  Samson Mapunda ndiye Mkurugenzi wa kampuni hiyo wakati wakijua wazi hakuna mtu anayeitwa Mapunda na jina hilo ni la kufikirika na waliwasilisha nyaraka hizo Brela Desemba 23 mwaka 2003 na kuwa mahakama yake imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa jamhuri uliokuwa ukiuongozwa na Wakili Kiongozi wa Serikali ambaye hivi sasa ni marehemu Stanslaus Boniface kuwa mshitakiwa wa kwanza na wapili(Mahenge,Manase) walitenda kosa hilo na hivyo mahakama yake inawahukumu kwenda jela miaka mitano.

Alilitaja kosa la tatu ni la kutoa nyaraka hizo za uongo za kuomba usajili wa kampuni zinazaoonyesha Mapunda ndiye Mkurugenzi wa Kampuni ya Changanyikeni kumbe ni jina la kufikirika kwa kampuni ya Brela na kampuni hiyo ikapewa usajili na Brela ambapo kosa hilo lilikuwa linamkabili Mahenge peke yake na kwamba mahakama imeliridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa jamhuri na kwamba mahakama yake inamhukumu Mahenge peke yake kwenda jela miaka saba.

Hakimu Mlacha alilitaja kosa la nne ni la kampuni ya Changanyikeni Residential Complex ya washitakiwa kujipatia usajiliwa kampuni toka Brela kwa nia ya udanganyifu kwa kutumia jina la kufikirika  ambapo mahakama yake katika kosa hili linamtia hatiani mshitakiwa wa kwanza na pili ambao watakwenda jela mwaka mmoja.
Katika kosa la tano ambalo ni la kughushi ambalo linawakabili washitakiwa wote , hakimu huyo alisema katika maelezo ya onyo aliyoyaoa wachunguzi wa kesi hii, Mahenge alikiri kuwa yeye alikuwa akitumwa kuchukua hundi za malipo ya kampuni hizo mbali na kwamba yeye ndiye aliyekwenda kupeleka fomu Brela za kusajili kampuni yao ya Changanyikeni na alikuwa akisaidiana kufanya kazi hizo na mshitakiwa wa pili , hivyo mahakama hiyo imemtia hatia mshitakiwa wa kwanza(Mahenge) na mke na Mume(Manase na Edda),  na kwamba watakwenda jela miezi 18.  

Kosa la sita ,Mchala alisema ni kwaajili ya   washitakiwa wote ambalo ni la kughushi hati ya kuamisha deni  iliyokuwa ikionyesha kampuni ya Marubeni ya Japan imeridhia kampuni ya Changanyike idai deni lake jambo ambalo si kweli.
“Licha upande wa utetezi ulidai hati hiyo ya kuamisha deni ilikuwa ni halisi lakini sisi kama mahakama tulipata wasaa tukaikagua kwa makini hiyo hati ya kuamisha deni tukabaini hata hiyo kampuni ya marubeni haikutia saini katika hati hiyo, na kampuni ya Changanyikeni aliyesaini hati hiyo alisaini bila kuwepo shahidi wa kushuhudia tukio hilo na kwamba na hati hiyo inaonyesha isainiwa katika mgahawa wa City garden Dar es Salaam, na tulijuiliza Marubeni ni kampuni kubwa kwani hakutia saini katika hati hiyo na mwisho wake mahakam hii ikakubaliana na upande wa jamhuri hati hiyo ya kuamisha deni ilikuwa imeghushiwa Mahenge ambaye katika maelezo yake ya onyo alikiri kuwa ni yeye ndiyo aliyepeleka hati hiyo na nyaraka hizo ambazo mahakama imeridhika kuwa zilighushiwa Brela na BOT na kwasababu hiyo mahakama hii inamtia hatiani mshitakiwa wa kwanza na wa pili katika kosa hilo na hivyo wataenda jela miezi 18.

Aidha  alilitaja shitaka la saba kwaajili ya washitakiwa wote ambalo ni la kuwasilisha hati hiyo ya kuamisha deni iliyoghushiwa na kwamba mahakama yake imemtia hatiani mshitakiwa wa kwanza katika kosa hilo ambapo atakwenda jela  mwaka mmoja tu.
Kuhusu shitaka la nane  ambalo ni wizi na shitaka la tisa lilikuwa ni la kujipatia kiasi hicho cha fedha toka BoT, hakimu Mlacha alisema mahakama yake inawaachiria huru katika makosa hayo mawili kwani mahakama yake imeyafuta makosa hayo kwasababu tangu hapo awali mahakama yake ilitoa amri kwa upande wa jamhuri kwenda kuyafanyia marekebisho makosa hayo lakini upande wa jamhuri ulishindwa kufanya hivyo hadi jana mahakama yake ilipofikia hatua ya kutoa hukumu hiyo hivyo mahakama yake ikatamka kuwafutia mashitaka hayo mawili kwa washitakiwa wote.

Hata hivyo alisema kwa mujibu wa ushahidi ulioletwa  na upande wa jamhuri, ushahidi huo umeshindwa kuishawishi mahakama imuone mshitakiwa wa tatu(Davis Kamungu) na wanne (Mosha)wana hatia katika kesi hiyo na kwasababu hiyo mahakama yake ikawaachilia huru washitakiwa hao na mahakama hiyo ikawatia hatiani jumla ya washitakiwa watatu.
Badaa ya hakimu Mlacha kuwatia hatiani washitakiwa hao wakili Mwanadamizi wa serikali Shadrack Kimaro alidai upande wa jamhuri hauna rekodi za uhalifu za washitakiwa waliotiwa hatiani ila wanaiomba itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine na kwamba mahakama itumie 384(1) na 358(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 , kuwaamuru washitakiwa waliotiwa hatiani kurejesha kiasi hicho cha fedha serikalini.

Kwa upande wake wakili wa washitakiwa Tarimo, aliomba mahakama iwapatie adhabu ndogo kwani hii ni mara yao ya kwanza kukutwa na hatia, na kwamba Manase na Edda ni mke na mume wanafamilia inawategemea na kwamba Edda anasumbuliwa na maradhi ya uzazi hivyo anaomba wapewe adhabu ndogo.
Aidha hakimu Mlacha alisema amesikiliza maombi ya pande zote mbili na kwamba mahakama hiyo inaamuru Mahenge na Manase warejeshe kiasi hicho cha fedha na kwamba adhabu hiyo itakwenda pamoja.
Kwa maana hiyo Mahenge peke yake atakwenda jela jumla miaka saba, Manase anakwenda jela miaka mitano na Edda atakwenda jela miezi 18 tu.

Baada ya hukumu hiyo kumalizika kusomwa baadhi ya ndugu na jamaa washitakiwa hao waliangusha vilio mahakamani hapo na wanausalama waliwachukua wafungwa hao na kuwapeleka gerezani.

Novemba 2008, Wakili Kiongozi wa Serikali marehemu Stanslaus Boniface alidai washitakiwa hao walitenda makosa hayo.

Hii ni kesi ya tano sasa  ya EPA kati ya kesi 12 za EPA zilizofunguliwa mahakamani hapo Novemba 2008 na Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi kufuatia kumalizika kwa uchunguzi wa Tume ya rais jakaya Kikwete ya kuchunguza wizi katika akaunti ya EPA, kutolewa hukumu, kesi tatu za EPA zinazomkabili Kada wa CCM ,Rajabu Maranda kutolewa hukumu na kesi mmoja ya EPA iliyokuwa ikiwakabili wafanyab iashara na maofisa wa BOT nayo kutolewa hukumu ambapo walipatikana na hatia.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Septemba 28 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.