Header Ads

SHAHIDI WA MRAMBA AWEKEWA PINGAMIZI


Na Happiness Katabazi
 
SHAHIDI wa tatu anayemtetea aliyekuwa Waziri wa Fedha,Basil Mramba ambaye ni Naibu Kamishna wa Income Tax , Felisian Busigala (67), jana alijikuta akishindwa kuendelea kutoa ushahidi wake katika kesi hiyo  ya matumuzi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh.bilioni 11.7 inayomkabili Mramba na wenzake kwasababu upande wa jamhuri kumuwekea pingamizi la kwamba hastahili kuwa shahidi katika kesi hiyo kwasababu ushahidi alioanza kuutoa anaonyesha amefika mahakamani hapo kama mtaalamu wa masuala ya kodi na siyo shahidi ambaye anastahili kuzungumzia mashitaka yanayomkabili Mramba.
 
Pingamizi hilo liliwasilishwa na mawakili wa serikali waandamizi Shadrack Kimaro na Oswald Tibabyekomya mbele ya jopo la majaji watatu John Utamwa ,Sam Rumanyika na Hakimu Mkazi Saul Kinemela ikiwa ni saa chache tu tangu shahidi huyo wa tatu wa Mramba ambaye pia ndiye Kamishna wa kwanza nchini wa  Costumes   Exercise wa TRA ,kupanda kizimbani na kuanza kutoa ushahidi wake huku akiongozwa na wakili wa Mramba, Hurbbet Nyange kutoa ushahidi wake.
 
Wakili Tibabyekomya aliomba akiwasilisha pingamizi hilo aliomba shahidi huyo asiendelee kutoa ushahidi wake kwasababu ushahidi aliokuwa ameanza kuutoa jana asubuhi unaonyesha Busigala amefika mahakamani hapo kutoa ushahidi wa kitaalamu na siyo kutoa ushahidi unaohusu mashitaka yanayomkabili Mramba  na kwamba mawakili wa upande wa utetezi wamekiuka utaratibu wa kumleta shahidi huyo kwani wamemleta shahidi kama mtaalamu badala ya shahidi.
 
Baada ya kusikiliza ombi hilo la upande wa jamhuri, Jaji Utamwa alisema shahidi huyo kwa jana hataweza kuendelea kutoa ushahidi wake kwasababu upande wa jamhuri umewasilisha pingamizi hilo, na akautaka upande wa utetezi uwasilishe majibu ya pingamizi hilo Oktoba 14 , upande wa jamhuri ujibu Oktoba 21   na uamuzi wa pingamizi hilo utatolewa Oktoba 25  na kesi hiyo itaendelea kusikilizwa kuanzia tarehe hiyo ya Oktoba 25 hadi 29 mwaka huu, na akamtaka shahidi huyo asije mahakamani hadi pale mahakama hiyo itakapotoa uamuzi wa pingamizi hilo na akasema kesi hiyo itatajwa Oktoba 18 mwaka huu na akapatia kibali cha kusafiri nje ya mkoa washitakiwa wote.
 
Mapema jana asubuhi Busigala akiwa kizimbani akijibu maswali ya wakili Nyange ambayo yalimtaka shahidi huyo afafanue maana ya ‘Net of all taxes’ kwasababu kwa mujibu wa mkataba ulioingiwa na Benki Kuu na kampuni ya Alex Stewart inaonyesha BoT kwaniaba ya serikali iliridhia kampuni hiyo ichukue asilimia 1.9 ya dhahabu yote atakayokuwa ameishaikagua.Na aieleze mahakama kuwa je  Mramba alikosea au alikuwa sahihi kwa hatua yake ya kutoa msamaa wa kodi kwa kampuni ya Alex Stewart? Na je Waziri wa Fedha anayo mamlaka ya kusamehe kodi kampuni?
 
Busigala alianza kufafanua kuwa ‘Net of all taxes’ katika mkataba ule maana yake kampuni ya Alex Stewart  ataondoka na asilimia 1.9 baada ya kumaliza ukaguzi wa dhahabu  na hiyo asilimia 1.9 ni baada ya  kodi yote kukatwa na serikali na kwamba kama kisingekuwepo hicho kipengele kwenye ule mkataba ni kwamba kampuni ya Alex Stewart  angelipwa fedha zaidi na serikali ili mwisho wa siku kampuni hiyo iweze kuja kulipa kodi husika kwa serikali na tatizo hapo siku zote kodi zimekuwa zikibadilika badilika kwani zinapanda na kushuka  na hivyo ingelikuwa ni vigumu kwa serikali  kuweza kutekeleza matakwa ya mkataba ambao usingekuwa na kipengele hicho cha kumlipa moja kwa fedha kampuni na kisha kampuni ije ilipe kodi husika kwa serikali.
 
Maelezo hayo ndiyo yalisababisha mawakili wa upande wa jamhuri kuwasilisha pingamizi hilo ambalo lilisababisha mahakama kumtaka shahidi huyo asindelee kutoa ushahidi wake hadi watakaposikiliza pingamizi hilo kwa njia ya maandishi na watalitolea uamuzi Oktoba 25 mwaka huu.Kesi hiyo ambayo ilianza kusikilizwa mfululizo rasmi Jumatatu ya wiki hii na kumalizika jana. 
 
Novemba 2008 ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Mramba na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Daniel Yona na Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Mipango na Uchumi Gray Mgonja wanakabiliwa na makosa mbalimbali ya matumizi mabaya na kuisababishia serikali hasara ya Sh.bilioni 11.7.
 
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi ,Septemba 21 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.