WAPAKISTANI KORTINI KWA KUUA TEMBO,NYATI
Na Happiness Katabazi
RAIA wa nne Raia wa nchini Pakistani jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es
Salaam, wakikabiliwa na mashtaka
ya uhujumu uchumi kwa kusafirisha nyara za serikali zenye thamani
ya zaidi ya Sh milioni 52.6 kwenda jiji la Guangzhou China, kuwinda
wanyama na kuwaua bila kibali.
Mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo, wakili wa serikali Mwandamizi,
Faraja Nchimbi aliwataja washtakiwa hao kuwa mfanyabiashara na mkazi wa Mount
Meru View Arusha, Kamran Ahmed (32), Wafanyabiashara na wakazi wa
Mtaa wa Mkunguni Kariakoo, Usman Afzal(32), Shekh Mohammad (30) pamoja na
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Paktan Company Limited, Mohammad Sufian (27).
Wakili Nchimbi alidai washitakiwa
hao walitenda makosa hayo kati ya Januari Mosi, mwaka 2005 na Septemba
14, mwaka 2013. Na kuwa washtakiwa wote kwa pamoja hao walisafirisha
meno ya Tembo yenye mng’ao mweupe 50 yenye thamani ya Sh 6,480,000 kwenda jiji la Guangzhou nchini China.
Wakili Nchimbi alidai kuwa shitaka jingine
ni la washitakiwa waliwinda na kuua
wanyama akiwamo Tembo mmoja mwenye thamani ya dola za Kimarekani 15,000, Chui
mwenye thamani ya dola za Kimarekani 3,500 na Duma mmoja mwenye thamani
ya dola za Kimarekani 4,900.
Pia washtakiwa hao wanadaiwa kuwawinda
na kumuua Nyati mmoja mwenye thamani ya dola za Kimarekani 1,400,
Pundamilia mwenye thamani ya dola za Kimarekani 1,200, Swala mwenye
thamani ya dola za Kimarekani 320 pamoja na Eland mmoja mwenye thamani ya dola
za Kimarekani 1,700 wote wakiwa na jumla ya Sh 46,202,400 mali ya
Serikali na akadai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Baada ya wakili Nchimbi kumaliza kuwasomea mashitaka
hayo, hakimu Fimbo aliwataka washitakiwa hao wasijibu chochote kwasababu mahakama yake haina mamlaka ya
kusikiliza kesi hiyo na akaiarisha kesi hiyo hadi Septemba 30 mwaka huu,
itakapokuja kwaajili ya kutajwa na akaamuru washitakiwa wapelekwe gerezani.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Septemba 17 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment