Header Ads

AMATUS LIYUMBA ATOKA GEREZANI

Na Happiness Katabazi
HATIMAYE aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba (63) ametoka jela katika gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam , alikokuwa akiishi baada ya kumaliza kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka miwili gerezani.


Kwa mujibu wa taarifa za kuaminika toka ndani ya familia ya Liyumba, zililiambia Tanzania Daima jana kuwa Liyumba alitoka gerezani hapo jana saa 3:30 asubuhi bila ya kuwepo kwa vikwazo vyovyote.

Vyanzo hivyo ambavyo havikutaka kutaja majina yao gazetini kwa madai kuwa wao siyo wasemaji wa familia Liyumba, vilisema kuwa ndugu zake wachache walifika saa mbili asubuhi katika gereza la Ukonga kwaajili ya kumchukua ndugu yao na ilipofika saa 3:30 asubuhi, uongozi wa Gereza la Ukonga ulimruhusu Liyumba kutoka gerezani hapo baada ya mfungwa huyo na uongozi huo wa gereza kukamilisha taratibu zote za kumuachilia huru mfungwa anayekuwa amemaliza muda wake wa kutumikia kifungo na wakafanikiwa kuondoka naye.

“Tunamshukuru mungu ndugu yetu Liyumba leo katoka gerezani baada ya kumaliza kutumikia kifungo cha miaka miwili jela na hivi tunayofuraha kwani amerudi uraiani kurejea na familia yake…kwakweli tunafuraha na yote yaliyompata ndugu yetu tunamwachia mungu”kilisema chanzo hicho.

Hata hivyo juhudi za gazeti hili za kumpata Liyumba ili azungumzie kumalizika kwa adhabu yake, zilishindikana kufuatia ndugu zake wa karibu kueleza kuwa hivi sasa ndugu yao hayupo tayari kuzungumza na vyombo vya habari kwani anaitaji kupumzika pamoja na familia yake.

Septemba 8 mwaka huu, Liyumba anayetetewa na mawakili wa kujitegemea Hudson Ndusyepo na Onesmo Kyauke alifikishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Stewart Sanga akikabiliwa na kesi mpya ya kukutwa simu gerezani hata hivyo alipata dhamana baada ya kujidhamini kwa bondi ya Sh 50,000. Na wakili wa Serikali Elizabeth Kaganda alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo mpya umekamilika na kwamba Septemba 29 mwaka huu, watakuja kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa huyo.

Desemba mwaka jana , Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Emilian Mushi alitupilia mbali rufaa iliyokatwa na Liyumba iliyokuwa ikiiipinga hukumu ya Mahakama ya Kisutu iliyomuhukumu kwenda jela miaka miwili baada ya kumtia hatiani kwa kosa moja la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma ambapo jaji huyo alisema akubaliana na hukumu ya Kisutu kwani ilikuwa sahihi kisheria.

Mei 23 mwaka 2010, Mahakimu wawili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa walitoa hukumu ya kumtia hatiani Liyumba kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya umma, na hakimu mkazi mmoja Edson Mkasimongwa ambaye ndiye aliyekuwa akiliongoza jopo hilo kusikiliza kesi hiyo alitofautiana na mahakimu hao wawili na akatoa hukumu ya peke yake ambayo ilimwachiria huru mshtakiwa huyo.

Lakini hata hivyo hukumu iliyotolewa na mahakimu hao wawili ndiyo ilibaki kuwa ni hukumu ya mahakama ya Kisutu na hukumu ya Hakimu Mkasimongwa ikabaki kwenye kumbukumbu za mahakama na haikutumika kwaajili ya kumpatia adhabu Liyumba

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Septemba 24 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.