Header Ads

SHAHIDI KESI YA MTIKILA AISHANGAZA MAHAKAMA

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa pili wa upande wa Jamhuri katika kesi ya kumkashfu Rais Jakaya Kikwete kuwa anakumbatia waislamu inayomkabili Mchungaji Christopher Mtikila, Daniel Kikunile(34) ameshindwa kumtambua mshtakiwa huyo ambaye alikuwepo mahakamani hapo wakati kesi hiyo inayomkabili ikiendelea jana.


Kikunile ambaye ni Mchungaji wa Kanisa Groly Of Christ Tanzania mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo alikuwa akiongozwa na wakili wa serikali Elizabeth Kaganda kutoa ushahidi wake ambapo alieleza kuwa Mwishoni mwa Machi 2010 asubuhi alikuwepo ndani ya kanisa hilo na alikuja mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mchungaji Mtikila(mshtakiwa) na kumuulizia Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo Joseph Gwajima kama yupo.

Yafuatayo ni mahojiano kati ya Wakili wa Serikali Kaganda na shahidi:
Swali:Huyo mtu aitwaye Mtikila aliyekuja siku hiyo kanisani kwako na kukukuta unaweza kumtambua hapa mahakamani?
Jibu: Mtu huyo aitwaye Mtikila hayupo hapa mahakamani.(Watu wakaangua kicheko kwasababu Mtikila alikuwepo mahakamani.
Swali:Huyo mtu alikupatia ujumbe gani siku hiyo kanisani?
Jibu:Alinipatia barua ambayo alinitaka nimpatie Gwajima pindi atakaporudi na Gwajima aliporudi kanisani hapo nilimpatia barua hiyo na wala sikuwa nafahamu kilichokuwa kimeandikwa kwenye ile barua kisha nikaondoka kwenda kuendelea na kazi zangu.Na baada ya siku chache walikuja wageni wawili kanisani hapo na wakakutana na Gwajima na Gwajima akaniita na kunitambulisha kwa wale wageni kuwa mapolisi na kwamba wamefika pale kwasababu ya ile barua ya niliyokadhiwa na Mtikila ambayo Gwajima alikuja kunieleza kuwa ule ulikuwa ni Waraka wa kumkashfu Rais Kikwete kuwa anakumbatia waislamu hivyo wakristo waungane wamuweke mkristo Ikulu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Kwa upande wake Mtikila ambaye hana wakili aliambia mahakama kuwa hawezi kumhoji zaidi shahidi kwasababu tayari shahidi huyo wa Jamhuri ameshindwa kumtambua. Hakimu Fimbo akaiarisha kesi hiyo hadi Oktoba 3 mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Septemba 8 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.