Header Ads

MTIKILA AFUNGUA KESI KUZUIA MAHAKAMA YA RUFAA ISIUZWE

Na Happiness Katabazi

MWENYEKITI wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, amefungua kesi ya Kikatiba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana, akiitaka izuie kuuzwa kwa jengo la Mahakama ya Rufaa lililopo eneo la Kivukoni Front, kwa mmiliki wa Hoteli ya Kempinski.


Kwa mujibu wa hati ya madai ambayo tayari imeshapewa namba 23 ya mwaka huu, Mtikila anamshtaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Katiba na Sheria na Jaji Mkuu wa Tanzania kwa kuruhusu jengo hilo la mahakama ya juu nchini liuzwe.

Mtikila amefungua kesi hiyo chini ya ibara ya 27(1) ya Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inayosomeka: “Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.”

Anadai kuwa amefikia uamuzi wa kuwashtaki walalamikaji hao kwa sababu wadaiwa hao wana dhamana ya kulinda mali za umma zisifujwe lakini cha kushangaza ndiyo wamekuwa mstari wa mbele kwa kushindwa kulinda jengo hilo ambalo ni mali ya umma na matokeo yake wameshiriki kuharibu mali hiyo ambayo ni jengo la kihistoria.

Hatua hiyo ya Mtikila kufungua kesi, imekuja ikiwa ni siku chache toka Waziri wa Katika na Sheria, Celina Kombani, kuueleza umma kuwa taratibu za kisheria zimefuatwa za kuliuza jengo hilo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Septemba 9 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.