Header Ads

TANESCO MSIKATE UMEME MAHOSPITALINI


Na Happiness Katabazi
KWA TAKRIBANI miaka mitano sasa Watanzania waliobahatika kupata nishati ya umeme wamekuwa wakikabiliwa na ukosefu wa umeme wa uhakika.


Hali hiyo imekuwa ikisababisha baadhi ya watu kukosa ajira, uzalishaji viwandani kupungua, wagonjwa kupoteza maisha mahospitalini kwaajili ya ukosefu wa uhakika wa nishati hiyo na hata uchumi wa nchi yetu kusuasua kutokana nauzalishaji viwandani kupungua kutokana na ukosefu wa umeme.

Ijumaa iliyopita mwanangu Queen ‘Malkia’ (3) alilazwa kwa siku moja katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam, ambapo alililazwa kwa siku moja baada ya Daktari wa watoto Dk. Zubeda Kange na Dk. Saumu Mweli kumgundua anasumbuliwa na ugonjwa Tonsilite.

Kwanza nawashukuru madaktari na wauguzi wote wa wodi ya watoto katika Hospitali hiyo ya Jeshi Lugalo kwani walijitahidi kadri ya uwezo wao kuakikisha wanampatia huduma bora mwanangu na watoto wengine ambao walikuwa wamelazwa katika wodi hiyo.

Tangu asubuhi siku hiyo ndani ya hospitali hiyo kulikuwa na umeme lakini ilipofika saa 10-moja jioni umeme ulikatika hali iliyosababisha baadhi ya wananchi waliokuwa wakifika hospitalini hapo na kuonana na madaktari ambapo waliandikiwa vipo mbalimbali ili waende mahabahari kwaajili ya kupimwa na kugundulika na maradhi gani, lakini wagonjwa hao walipokuwa wakifika kwenye mahabara hiyo muda huo kwaajili ya kuchukuliwa vipimo.

Wataalamu wa mahabara walishindwa kuwachukua vipimo kwasababu ya umeme kukatika ndani ya hospitali hiyo.Kutokana na joto lilokuwa ndani ya wodi ya watato mimi na mwanangu tulitoka ndani ya wodi hiyo na kuketi kwenye viti ambavyo vimetazamana na mahabara hiyo na niliweza kuwashuhudia zaidi wananchi zaidi ya sita katika kipindi hicho wakifika katika mahabara hiyo kwaajili ya kuchukuliwa vipimo wakati umeme umekatika waliamua kwenda hospitali nyingine kupima na wengine waliamua kupima vipimo hapo na kuviacha mahabara ili umeme ukirudi muda usiofahamika warudi kuvichukua vipimo hivyo.

Hali hiyo ilinisikitisha sana licha halikuwa limeniathiri mimi binafsi.Kwani miongoni mwa watu hao waliokuwa wamefika katika kuchukuliwa vipimo walikuwa wanamaumivu makali katika mihili yao na walikuwa wakiitaji wapatiwe matibabu haraka lakini ndiyo ilikuwa haiwezekani kumpatia mgonjwa matibabu bila kujua amegunduliwa na vipimo vya mahabara kuwa anasumbuliwa na maradhi gani.

Niliishia kujiuuliza hivi kweli Shirika la Umeme(TANESCO) limeshindwa kabisa kuketi chini na kuorodhesha hospitali zote nchini kuwawekea ‘line’maalum ambazo zitafanya umeme katika hospitali hizo usikatike?

Kama ni Tanesco hii hii imeweza kutenganisha ‘line’ katika baadhi ya makazi watumishi wa Idara nyeti hayakatwi umeme, ni kwanini Tanesco hii inashindwa kuunganisha line maalum katika mahospitali yetu ili yasiwe yanakatiwa umeme?

Hivi Tanesco inajipendekeza nini kwa makazi hayo ya wafanyakazi wa idara nyeti za serikali kutowakatia umeme, halafu inaona fahari kukata umeme katika mahospitali ambayo wananchi wengine maskini tunaosumbuliwa na maradhi tunakwenda mahospitalini kwaajili ya kupata tiba halafu kisha tunajikuta tunakosa tiba kwa wakati eti kwasababu ya mgao wa umeme hadi mahospitalini?

Ikiwa ni mahospitali haya haya ya serikali kila kukicha yamekuwa yakikabiliwa na upungufu wa madawa, ufinyu wa vitanda vya kulazia wagonjwa, leo hii serikali hii kupitia Tanesco inaendelea kuzitumbukiza kwenye shimo hospitali hizo ambazo zinatumiwa na wananchi, kuziingiza kwenye mgao wa umeme ambao unasababisha hospitali hizo kuingia gharama ya kununua mafuta kila wakati kwaajili kuweka kwenye majenereta?

Mfano mzuri ni pale wodi ya wazazi ya Hospitali ya Mwananyamala, wanawake wanaosubiri kwenda chumba maalum kwaajili ya kujifungua wengine ujikuta wakilala chini kutokana na uhaba wa vitanda.Sasa katika hali kama hiyo ya msongamano ya wanawake wajawazito kulala chini, ongezea ukosefu wa umeme iwe mchana au usiku, hivi katika hali ya kawaida huyo mama mjazito anakuwa na hali gani ya kiafya?

Na mbaya zaidi Tanesco wakatapo umeme wala hawatoi taarifa kwamba dakika chache zijazo wanakata umeme, wanajikatia tu umeme wanavyojisikia wao na wakati wanakata kwa mtindo huo wa kutotoa taarifa mapema, kuna wananchi wenzetu wengine wanakuwa ndani ya vyumba vya upasuaji kwaajili ya kufanyiwa upasuaji na madaktari na wakati huo uenda majenereta ya baadhi ya mahospitali yanakuwa hayana mafuta, au yanahitilafu za ghafla hivyo uwezekano wa wananchi wenzetu kupoteza maisha wakiwa kwenye vyumba vya upasuaji kutokana na ukatikaji wa ovyo wa umeme ni mkubwa.

Imebidi tukubali kwamba Tanesco ndiyo mungu wa nishati ya umeme hapa Tanzania,kwani hadi sasa hajapatikana kiongozi mwenye maono na mwenye maamuzi ya kuweza kutupatia mbadala wa Tanesco ndiyo maana Tanesco inajiona ni mungu wa nishati ya Umeme.

Lakini katika hili la Tanesco kukata umeme katika mahospitali tunaomba likome mara moja, tunaamini wataalamu wale wale wa Tanesco waliweza kutenganisha line zinazokwenda kwenye makazi ya wafanyakazi wa idara nyeti za serikali ambazo hazikatwi umeme, pia ni wataalamu hao hao wanaweza sasa kutumia taaluma yao kutenganisha line zinazokwenda kwenye mahospitali ili umeme usiwe unakatika mahospitalini.

Kama Tanesco ipo kwaajili ya kulitumikia taifa hili bila ubagudhi wa makundi fulani, naamini wanaweza kuweka mpango mkakati wa kuakisha mahospitali yote hayakatiwi umeme, na hili linawezekana isipokuwa tu bado hatujapata viongozi wenye uchungu wa kwale wananchi wa taifa hili hasa wale wenye hali ya chini.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika
0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Septemba 16 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.