Header Ads

DOWANS HAIKAMATIKI

*Mahakama yatupa maombi yawanaharakati

Na Happiness Katabazi
HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeyafukuza maombi ya wanaharakati waliokuwa wakiongozwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC) ambao yaliyokuwa yakiomba mahakama hiyo ikatee kusajili tuzo iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa migogoro ya Kibiashara(ICC) kwa kampuni ya Dowans Holdings SA(Costa Rica) na na wenzake kwasababu wanaharakati hao hawana haki wala mamlaka ya kupinga hilo.


Sambamba na hilo, Jaji Emilian Mushi ambaye ndiye ametoa uamuzi huo wa kesi hiyo ya madai Na.8/2011iliyofunguliwa na LHRC, Chama cha Wanasheria wa Mazingira(LEAT),Kampuni ya Sikika Limited(SCL), na mwandishi wa habari Timothy Kahoho wanaotetewa na Dk.Sengondo Mvungi dhidi ya Dowans Tanzania,Dowans Holdings SA(costa rica) na Tanesco alisema uamuzi wa kusajiliwa au kutosajiliwa kwa tuzo ya Dowans ataitoa baadaye.

Jaji Mushi alianza kwa kuimbusha mahakama na kuwataka waandishi wa habari ufahamu kuwa uamuzi alioutoa jana ni mapingamizi ya awali yaliyowasilishwa na wakili wa wadaiwa Kennedy Fungamtama dhidi ya walalamikaji(Wanaharakati) na kwamba mahakama hiyo imefikia uamuzi wa kukubalina na mapingamizi ya wakili huyo kuwa walalamikaji hawana haki ya kisheria ya kufungua kesi ya kupinga tuzo hizo isisajiliwe kwa niaba ya Watanzania na kwamba wanaharakati hao wameshindwa kuonyesha ushahidi kuwa wao wanahaki,maslahi kwaniaba ya umma ya kufungua kesi kupinga tuzo hiyo isisajiliwe.

Jaji Mushi alisema pia anakubaliana na pingamizi la pili la wakili wa Dowans, Fungamtama kwamba walalamikaji hao hawakuwa wahusika kwenye kesi ya Dowans dhidi ya Tanesco iliyomalizika kwenye mahakama ya kimatiafa ya ICC hivyo kwakuwa hawakuwa wahusika katika kesi hiyo ni wazi hakuwa na mamlaka ya kufungua kesi ya kupinga utekelezaji wa hukumu ya ICC katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

“Katiba na Sheria za maamuzi mbalimbali ya mahakama yapo wazi nayametamka wazi kuwa mashauri ya madai yanayohusu nchi mwenye dhamana ya ulinzi na kufungua kesi za aina hiyo ni ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hivyo natupilia mbali ombi la wanaharakati hao ambao walidai kuwa wao ni watanzania wanahaki na wajibu wa kulinda mali za watanzania ndiyo maana wakafungua kesi hii ya kutaka Tuzo ya dowans isisajili, nalitupilia mbali ombi lao;

“Pia natupilia mbali maombi ya waombaji ‘wanaharakati’ kwasababu hayo maombi ya uwakilishi yakufungua kesi hiyo yameambatanishwa na mwenendo wa kesi iliyotolewa hukumu na mahakama ya kimataifa (ICC) na kwakushindwa kwao kafanya hivyo wakati Amri 1 Kanuni ya (8) ya Sheria ya Madai ya mwaka 2002 inawalazimisha wafanye hivyo, mahakama hii kwa mara nyingine inakubalina na pingamizi la wakili wa Dowans kuwa maombi hayo ya wanaharakati yanadosari ya kisheria na hivyo nayafukuza katika mahakama hii kwa gharama”alisema Jaji Mushi.

Sekunde chache baada ya Jaji Mushi kumaliza kusoma uamuzi wake mwombaji wa nne, Kahoho aliamka kwenye kiti alichoketi na kusema kuwa hajaridhishwa na uamuzi huo na kwamba atakarufaa katika Mahakama ya Rufaa na alipomaliza kusema maneno hayo jaji Mushi naye alimjibu maneno yafuatayo;

“Eeeh! Kahoho ni haki yako kusema hayo uliyoyasema naniaamini ukienda Mahakama ya Rufaa huko kuna wazee wazee ‘majaji’ watakusikiliza…lakini nataka utambue kuwa hata ukienda kukata rufaa hata sasa katika mahakama hiyo ya juu nchini, uamuzi wako huo hautanizuia mimi kutoa hukumu ya kesi ya Dowans dhidi ya Tanesco ambayo Dowans iliwasilishwa ombi lake hapa Mahakama Kuu lakuomba mahakama hii iisajili tuzo waliyopewa na mahakama ya ICC ”alisema Jaji Mushi na kusababisha watu kuangua vicheko mahakamani hapo.

Januari 25 mwaka huu, Dowans iliwasilisha ombi lake lakutaka Mahakama Kuu ya Tanzania iisajili tuzo waliyopewa na Mahakama ya ICC na siku chache baadaye wanaharakati hao wakawasilisha maombi ya kutaka tuzo hiyo isajiliwe kwasababu ni batili na ikisajiliwa Tanesco ambalo ni shirika la umma litajikuta likipoteza fedha nyingi kuilipa fidia ya bilioni 94 kampuni hiyo ya Dowans.

Mahakama ya ICC, ilitoa hukumu ya kesi ya Dowans dhidi ya Tanesco, Novemba 15 mwaka jana, ambapo mahakama ilitia hatiani Tanesco kwa kosa la kuvunja mkataba na Dowans na ikaimuru iilipe fidia ya shilingi bilioni 94.

Hukumu hiyo ya ICC, muda mfupi baada ya kutolewa ilizusha malumbano makali baina ya wananchi, wanaisiasa na kusababisha baadhi ya mawaziri na mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa kauli zinazopisha huku wachache wakitaka serikali iilipe Dowans huku wengine wakisema kulipwa fidia kampuni hiyo ni ufisadi.

Malumbano hayo ya nje ya mahakama yalisababisha pia Chama cha Mapinduzi(CCM), kuunda Kamati ya Wabunge kujadili hukumu hiyo na kisha wabunge watatu wa chama hicho Mbunge wa Kibakwe(CCM)George Simbachawe na Mbunge wa Karagwe(CCM), Gosbert Blandes na mbunge wa Viti Maalum,Angellah Kairuki na raia wengine wa nne kufungua kesi ya Kikatiba Na.5/2011 dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tanasco ambayo imeanza kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Njegafibili Mwaikugile, Agustine Shangwa na Projest Rugazia

Kwa mujibu wa hati ya madai ya walalamikaji hao wanaiomba mahakama itoe amri ya kuizuia serikali isiilipe kampuni ya Dowans na endapo malipo hayo yatafanywa kwa kampuni hiyo ni wazi wadaiwa hao ambao wanaiwakilisha serikali kwa ujumla watakiwa wamevunja ibara 26(2),27(1) na 27 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambazo mahakama hiyo ina wajibu wa kuilinda ibara hizo zisivunjwe.\

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Septemba 7 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.