Header Ads

LIYUMBA ASHITAKIWA TENA


Na Happiness Katabazi
ALIEYUKUWA Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania, Amatus Liyumba (63), ambaye Septemba 23 mwaka huu anamaliza kutumikia adhabu ya kifungu cha miaka miwili jela, jana alijikuta akipandishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam kwa kesi mpya ya kukutwa na simu gerezani.


Hata hivyo baada ya kuingizwa mahakamani saa 7:20 na wakili wa serikali, Elizabeth Kaganda, kumsomea shtaka moja linalomkabili, mawakili wake, Majura Magafu na Hudson Ndusyepo, waliibuka na hoja ya kutaka mteja wao asijibu chochote baada ya kusomewa shtaka hilo kwa hati yenye dosari.

Hali hiyo, ilisababisha Hakimu Mkazi, Stewart Sanga, anayesikiliza kesi hiyo kukubaliana na mawakili wa utetezi na akalazimika kutoa amri ya kuutaka upande wa Jamhuri uende ukaifanyie marekebisho hati hiyo na kisha muda kidogo baadaye urudi mahakamani hapo ikiwa na hati mpya ambayo imefanyiwa marekebisho.

Wakili wa serikali, Kaganda, akimsomea shtaka Liyumba kwa kutumia hati yenye dosari, alidai anakabiliwa na kosa la kukutwa na kitu kilichokatazwa gerezani chini ya kifungu cha 86 cha Sheria ya Magereza kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Alidai kuwa Liyumba ambaye ni mfungwa mwenye namba 303/2010, Julai, mwaka huu, ndani ya gereza la Ukonga, alikamatwa na simu aina ya Nokia Na.1280 nyeusi iliyokuwa na laini yenye namba 0653- 004662 na IMEI Na. 356273/04/276170/3 ambayo alikuwa akiitumia kwa ajili ya kufanya mawasiliano binafsi wakati ni kinyume cha sheria.

Baada ya Kaganda kumaliza kusoma shtaka hilo, wakili Magafu aliinuka na kudai kuwa hawaoni sababu ya mteja wao kukana au kukubali shtaka hilo kwa sababu tayari hati ya mashtaka ina makosa.

Magafu alidai kwa mujibu wa kifungu cha 86 cha Sheria ya Magereza, kifungu hicho kina vifungu vidogo vitatu yaani kifungu cha 86 (1, 2, 3) na kwamba hawaelewi Jamhuri inamshtaki mteja wao kwa kifungu cha 86 (1, 2, 3) au kipi na kuongeza kuwa ili mshtakiwa aweze kujibu mashtaka yanayomkabili ni lazima mashtaka yaliyo kwenye hati ya mashtaka yaeleweke yamefunguliwa chini ya kifungu kipi na si kama hivi ilivyofanya Jamhuri kwenye kesi hii.

Hivyo aliiomba Jamhuri ikaifanyie marekebisho hati hiyo ili mteja wake aweze kujibu kuhusu shtaka analoshtakiwa.

Akijibu hoja hiyo wakili wa serikali, Kaganda, alikiri kuwa ni kweli hati ya mashtaka inamshtaki kwa kifungu cha 86 cha Sheria ya Magereza lakini wanamaanisha kuwa anashtakiwa kwa kifungu cha 86 (1, 2, 3) cha Sheria ya Magereza na kuiomba hati hiyo ya mashtaka isomeke kuwa anashtakiwa chini ya kifungu hicho na vifungu vyote vidogo vilivyopo ndani ya kifungu hicho.

Hoja hiyo ilimlazimu tena wakili Magafu kudai kuwa wanasikitishwa na hoja hiyo ya Jamhuri kwani kifungu cha 86 (2) cha sheria kinatoa maana ya vitu vinavyokatazwa gerezani lakini hakiundi kosa.

Na pia kifungu cha 86 (3) kinataja vitu vilivyokatazwa gerezani na kinatoa mamlaka kwa Jeshi la Magereza kutaifisha kitu walichokikamata ndani ya gereza ambacho kimekatazwa na sheria hiyo.

“Tulitegemea tuusaidie upande wa Jamhuri kuweka vizuri hati yao ya mashtaka lakini ndiyo kwanza wanaenda njia potofu…sasa sisi tunasema haya mashtaka yameletwa kimakosa hapa mahakamani na mteja wetu hapaswi kujibu chochote hivyo tunaomba hati hiyo itupwe ili Jamhuri iende ikaifanyie marekebisho; mahakama hii ina mamlaka ya kuifuta hati hiyo au kuiamuru Jamhuri iende ikaifanyie marekebisho,” alidai Magafu.

Kufuatia malumbano hayo, Hakimu Sanga alisoma kifungu cha 86 cha Sheria ya Magereza, mstari kwa mstari, hivyo kukubaliana na hoja za wakili wa utetezi Magafu kuwa hati hiyo ina makosa na hivyo akauamuru upande wa Jamhuri uiondoe hati hiyo na iende ikaifanyiwe marekebisho na baada ya muda mfupi iletwe hati iliyofanyiwa marekebisho mahakamani hapo na kumsomea upya mashtaka mshtakiwa huyo.

Upande wa Jamhuri ulitii amri hiyo na ilipofika saa 8:22 mchana, Wakili Kaganda alirejea na kuiambia mahakama kuwa tayari ameishaifanyia marekebisho hati hiyo na kwamba hivi sasa itasomeka kuwa Liyumba anashtakiwa chini ya Kifungu cha 86 (1,2) cha sheria hiyo, ambapo mshtakiwa alikana shtaka huku wakili wa serikali akidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Wakili Magafu alidai kuwa kifungu cha 148 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 hakiikatazi mahakama kutoa dhamana kwa mfungwa anayekabiliwa na kesi mpya.

Aliongeza kuwa kwa vile Septemba 23, mteja wao anamaliza kutumikia adhabu yake gerezani na kwamba kosa linalomkabili hivi sasa lina dhamana, wanaiomba mahakama impatie dhamana, ombi ambalo halikupingwa na wakili wa serikali.

Hakimu Sanga alikubaliana na ombi hilo ambapo alisema ili mshtakiwa huyo apate dhamana, atatakiwa asaini bondi ya sh 50,000 na awe na mdhamini mmoja wa kuaminika.

Liyumba alitimiza mashtari hayo na kupatiwa dhamana kwa kesi hiyo lakini hata hivyo alirudi gerezani kwa ajili ya kutumia adhabu ya kesi ya matumuzi mabaya ya madaraka aliyohukumiwa nayo.

Hakimu aliahirisha kesi hiyo mpya hadi Septemba 29, mwaka huu, ambapo itakuja kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Mei 24 mwaka jana, Mahakama ya Hakimu Mkazi ilimtia hatiani kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kumhukumu kwenda jela miaka miwili lakini hata hivyo, Liyumba hakuridhika na hukumu hiyo akakata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Mbele ya Jaji Mushi, Desemba mwaka jana alitupilia mbali rufaa ya Liyumba kwa maelezo kuwa hukumu ya Mahakama ya Kisutu ilikuwa sahihi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Septemba 9 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.