Header Ads

DOWANS YAIBWAGA TANESCO


*ZITTO:NI MATOKEO YA SIASA CHAFU
Na Happiness Katabazi

JITIHADA za wanasiasa na wanaharakati kulizuia Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO), kulipa tuzo ya mabilioni ya shilingi kwa Kampuni ya kufua umeme, Dowans Tanzania, zimegonga mwamba baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam kutoa uamuzi wa kuiruhusu Dowans kusajili tuzo hiyo ili ilipwe.


Tuzo hiyo ya dola za Marekani milioni 65 (takriban sh bilioni 94) iliyotolewa Novemba 15, mwaka jana (2010); na Januari 25, mwaka huu, Dowans iliwasilisha ombi lake la kutaka Mahakama Kuu ya Tanzania iisajili tuzo waliyopewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa migogoro ya Kibiashara (ICC).

ICC iliitia hatiani TANESCO kwa kosa la kuvunja mkataba na Dowans, na ikaiamuru iilipe tuzo hiyo na riba ya asilimia 7.5.

Lakini wanaharakati kadhaa na wanasiasa hapa nchini wamekuwa wakipinga uamuzi huo wa ICC mahakamani. Jana Jaji Emilian Mushi alisema Mahakamu Kuu ya Tanzania haina mamlaka ya kutengua hukumu ya ICC.

Hatua hiyo ya wanasiasa na wanaharakati kuchelewesha malipo ya tuzo hiyo itaifanya TANESCO kulipa kiasi kikubwa zaidi kwani riba imekuwa inaongezeka. Hadi jana Dowans ilikuwa inastahili kulipwa sh bilioni 113 badala ya sh bilioni 94 kutokana na ucheleweshwaji huo.

Katika hukumu hiyo aliyoanza kuisoma kuanzia saa 3:31 asubuhi hadi 6:53 mchana, Jaji Mushi alisema kesi hiyo ya madai Na. 8/2011 iliyofunguliwa na TANESCO dhidi Dowans Tanzania, ilikuja kwake ili atoe hukumu ya ama kuiruhusu Dowans kusajili au kutokusajili tuzo hiyo. TANESCO katika pingamizi lake iliwasilisha sababu 12 za kupinga tuzo hiyo isisajiliwe.

Jaji Mushi alianza kwa kusema maneno yafuatayo:

“Kwanza, naishukuru TANESCO na zile taasisi nne za wanaharakati waliokuwa wakiongozwa na LHRC; walijitokeza mahakamani hapa kupinga tuzo ya Dowans isisajiliwe na kutumia muda wao kuchambua kesi mbalimbali na kuandaa mapingamizi yao, ambayo hata hivyo niliyatupilia mbali.

“Pili, nafahamu fika kuwa kesi hii ya Dowans ina sayansi nyingi sana za kisiasa, hivyo napenda niwafahamishe mapema kabisa kabla ya kuendelea kuwa hukumu yangu nitakayotoa leo haijatoa nafasi kwa sayansi hizo za kisiasa, kwa sababu imezingatia misingi ya sheria na haki.”

Jaji Mushi alisema miongoni mwa sababu zilizowasilishwa na mlalamikaji (TANESCO) za kutaka tuzo ya Dowans isisajiliwe ni pamoja na majaji wa Mahakama ya ICC kuipendelea Dowans, hukumu yake kuwa na upungufu wa kisheria, hukumu kutofuata sera na maslahi ya taifa na Mahakama Kuu ya Tanzania kutokuwa na mamlaka ya kuisajili tuzo hiyo. Dowans ilikuwa inatetewa na Wakili Kennedy Fungamtama, huku TANESCO ikitetewa na Kampuni ya uwakili ya Rex Attorney. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliwakilishwa na Naibu Mwanasheria Mkuu, George Masaju na Dk. Hawa Senare.

Jaji Mushi alisema baada ya kuipitia hukumu ya ICC amebaini kuwa haina makosa ya kisheria kama anavyodai mlalamikaji, na ndani ya hukumu hiyo alikuta kiambatanisho ambacho ni mkataba kati ya TANESCO na Dowans uliosainiwa Juni 23, mwaka 2006; na kufafanua kwamba pande zote mbili katika mkataba huo zilikubaliana kwamba uamuzi wa ICC ndiyo utakuwa wa mwisho, na utazibana pande zote mbili na hautaweza kukatiwa rufaa.

Jaji huyo alisema kifungu cha 14 (f) cha mkataba huo kinasomeka hivi: “The parties waive any right to challenge or contest the validity or enforceability of this arbitration agreement or any arbitration proceeding or award brought in conformity with this section.” Kwa tafsiri nyepesi, Fungamtama alisema kifungu hicho kinasema, TANESCO na Dowans katika mkataba wao walikubaliana kwa maandishi kuweka kando haki za kupinga au kuhoji mwenendo na tuzo zitakazotolewa na baraza la usuluhishi.

Jaji akasema: “Sasa kwa mujibu wa mkataba huo ni wazi kuwa TANESCO na Dowans walikubaliana kuwa endapo utatokea mgogoro baina yao utapaswa upelekwe ICC tu na ICC itakapotoa hukumu ya mgogoro baina yao, pande hizo mbili hazitakuwa na mamlaka ya kuikatia rufaa hukumu hiyo ya ICC.

“Kwa makubaliano hayo ya pande hizo mbili ndani ya mkataba huo wa POA ambao TANESCO hadi wanakwenda kujitetea ICC hawakuwa wameuvunja huo mkataba wa POA na kupitia mkataba huo ICC pia iliutumia kutolea uamuzi wake…ni wazi kabisa mahakama hii inakubaliana na hukumu ya ICC kuwa ilikuwa ni hukumu ya haki na iliyofuata sheria na ilizingatia pia masilahi ya sera za Tanzania na kwakuwa pande hizo zilikubaliana hukumu ya ICC hawataweza kuikatia rufaa basi ndivyo hivyo hivyo mahakama hii ya Tanzania haiwezi kutoa uamuzi wa kutengua hukumu hiyo iliyotolewa na ICC.”

Alisema anakubaliana na hoja ya wakili wa Dowans, Fungamtama, kuwa kifungu cha 3 cha jedwali la 3 katika Sheria ya Usuluhishi ya Tanzania, Sura ya 15 ya mwaka 2002 ambacho kinasomeka hivi: Kwa tafsiri rahisi, kifungu hicho utaona tayari nchi imejifunga mikono na utekelezaji wa hukumu zinazotolewa na mahakama za kimataifa kwa sababu ni nchi yetu yenyewe imeridhia sheria na mikataba ya kimataifa.

Jaji Mushi alisema kitendo cha TANESCO kuwasilisha ombi mbele yake likidai kuwa Mahakama Kuu haina mamlaka ya kusajili tuzo hiyo, halina ukweli na kwamba mwanasheria aliyefahamu vema Sheria ya Usuluhishi ya Tanzania ya mwaka 2002 Sura ya 15, Mikataba ya Kimataifa na Sheria ya Makosa ya Madai ya mwaka 2002 ataona wazi kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania imepewa mamlaka ya kusajili tuzo hapa nchini zinazotolewa na Mahakama za Kimataifa.

Jaji alisema hoja ya TANESCO kuwa mwenendo wa hukumu ya ICC ulikuwa na mapungufu ya kisheria, haikupaswa kupelekwa mbele yake kwani Tanasco walikuwa ni wadaiwa katika kesi iliyofunguliwa ICC na walipaswa kuiwasilisha hoja hiyo ICC kabla ya mahakama hiyo ya kimataifa kutoa hukumu yake na kuikumbusha TANESCO kuwa ni yenyewe iliyoingia mkataba wa POA na Dowans ambao kwa ridhaa yao waliridhia kuwa hukumu itakayotolewa na ICC haitakatiwa rufaa.

Kutokana na makubaliano ya pande hizo mbili, Jaji Mushi aliishangaa TANESCO kwa hatua yake ya kuwasilisha hoja hiyo ambayo ni wazi ilipaswa iwasilishwe kwenye mashauri ambayo yamekatiwa rufaa na kwamba shauri lilokuwa mbele yake halikuwa shauri la rufaa.

Hata hivyo Jaji Mushi alisema anatupilia mbali hoja ya TANESCO iliyodai kuwa hukumu ya ICC haikuzingatia sera za Tanzania kwa maelezo kuwa haina msingi na baada ya kuisoma hukumu ya ICC amebaini kuwa hukumu ya majaji wa ICC ilizingatia sera za Tanzania na kuitaka TANESCO itambue kuwa nchi yetu imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa na mahakama zote kote duniani zinatoa maamuzi yake kwa kufuata ushahidi uliowasilishwa mbele yake, sheria na haki na siyo vinginevyo.

Jaji Mushi alitupilia mbali hoja nyingine ya TANESCO iliyokuwa ikidai kuwa aliyekuwa mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, ndiye aliyekuwa akimiliki Dowans iliyokiuka taratibu za kupata tenda ya kuzalisha umeme kwa madai kuwa kesi iliyokuwa imefunguliwa ICC na Dowans dhidi ya TANESCO ilikuwa haihusiani kabisa na nani mmiliki wake, na akakubaliana na hukumu hiyo kuwa Rostam Aziz hausiki kwa namna yoyote ile kwenye kesi hiyo.

Jaji Mushi alikubali ombi la Dowans la kusajili tuzo waliyopewa na ICC isajiliwe na mahakama ya Tanzania. aidha, jaji aliiamuru TANESCO kulipa gharama zote za uendeshaji wa kesi hiyo, na Dowans ianze taratibu za kukazia hukumu ya Mahakama ya ICC.

Septemba 6 mwaka huu, Jaji Emilian Mushi alitoa uamuzi wa kuyatupilia mbali maombi ya wanaharakati waliokuwa wakiongozwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ambao waliiomba mahakama hiyo ikatae kusajili tuzo iliyotolewa na Mahakama ya ICC kwa kampuni ya Dowans Holdings SA(Costa Rica) na Dowans Tanzania kwa sababu wanaharakati hao hawana haki wala mamlaka ya kupinga hilo.

Katika uamuzi wake huo, Jaji Mushi alisema anakubaliana na pingamizi la wakili wa Dowans, Fungamtama kwamba walalamikaji hao hawakuwa wahusika kwenye kesi ya Dowans dhidi ya TANESCO iliyomalizika ICC, hivyo ni wazi hawakuwa na mamlaka ya kufungua kesi ya kupinga utekelezaji wa hukumu hiyo katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

“Katiba na sheria za maamuzi mbalimbali ya mahakama yapo wazi na yametamka wazi kuwa mashauri ya madai yanayohusu nchi mwenye dhamana ya ulinzi na kufungua kesi za aina hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hivyo natupilia mbali ombi la wanaharakati hao ambao walidai kuwa wao ni watanzania wenye haki na wajibu wa kulinda mali za watanzania ndiyo maana wakafungua kesi hii ya kutaka Tuzo ya Dowans isisajiliwe. Kwa msingi huo, nalitupilia mbali ombi lao,” alisema Jaji Mushi.

Mahakama ya ICC ilitoa hukumu ya kesi ya Dowans dhidi ya TANESCO, Novemba 15 mwaka jana baada ya kampuni hiyo kuishinda TANESCO katika kesi yake ya kudai fidia ya kuvunjiwa mkataba iliyokuwa imefunguliwa rasmi Novemba 20 mwaka 2008 na kupewa Na. 15947/VRO ambapo Mahakama ya ICC iliitia hatiani TANESCO kwa kosa la kuvunja mkataba na Dowans na ikaiamuru iilipe fidia ya dola za Marekani milioni 65 na riba ya asilimia 7.5.

Hukumu hiyo ya ICC, muda mfupi baada ya kutolewa ilizusha malumbano makali baina ya wananchi, wanaisiasa, mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa kauli zinazopishana huku wachache wakitaka serikali iilipe Dowans na wengine wakisema kulipwa fidia kampuni hiyo ni ufisadi.

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, ndiye aliyekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari kuhamasisha umma na serikali isiilipe Dowans. Kwa upande mwingine, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Fredrick Werema na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, walitaka Dowans ilipwe, hali iliyosababisha baadhi ya wananchi kuwashambulia kwa maneno makali wale wote waliokuwa wakitaka Dowans isajiliwe kisha ilipwe tuzo yao.

Malumbano hayo nje ya mahakama yalisababisha pia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuunda Kamati ya Wabunge kujadili hukumu hiyo na kisha wabunge watatu wa chama hicho, George Simbachawe (Kibakwe), Mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes, Mbunge wa Viti Maalumu, Angellah Kairuki na raia wengine wanne kufungua kesi ya Kikatiba Na. 5/2011 dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na TANESCO ambayo imeanza kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Njegafibili Mwaikugile, Agustine Shangwa na Projest Rugazia.

Kwa mujibu wa hati ya madai, walalamikaji hao wanaiomba mahakama itoe amri ya kuizuia serikali isiilipe Kampuni ya Dowans na endapo malipo hayo yatafanywa kwa kampuni hiyo ni wazi wadaiwa hao ambao wanaiwakilisha serikali kwa ujumla watakuwa wamevunja ibara 26(2),27(1) na 27 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambazo mahakama hiyo ina wajibu wa kuilinda ibara hizo zisivunjwe.

ZITTO KABWE ATOA MAONI:
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, ameupongeza uamuzi huo wa Mahakama Kuu akidai kuwa ni malipo ya maamuzi yanayotokana na siasa za kipuuzi na uzalendo pofu.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu Kabwe alisema tumeliingiza taifa hasara kubwa kwa sababu ya uongozi dhaifu na siasa za makundi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alisema TANESCO hawataweza kulipa fidia hiyo kwani walilazimishwa kuingia mkataba na kisha kuuvunja.

Kabwe alisema Kamati ya Mashirika ya Umma imeishaagiza kwamba deni hilo lisitokee katika hesabu za Shirika la TANESCO bali Serikali Kuu na kwamba hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amegoma kusaini hesabu za TANESCO za mwaka 2010 mpaka serikali ikubali kubeba mzigo huo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Septemba 29 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.