Header Ads

JAJI AZIONYA PANDE ZINAZOPINGANA CUF

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imewashauri mawakili wa pande mbili katika kesi ya kutaka mahakama itamke kuwa uamuzi wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi (CUF), uliomvua uanachama Mbunge wa Jimbo la Wawi, Hamad Rashid, kuwa ni batili iliyofunguliwa na mbunge huyo na wenzake 10, waachane na tabia ya kuleta pingamizi za awali kwani zinasababisha kesi hizo na zingine kutomalizika mapema.

Jaji Augustine Shangwa alitoa onyo hilo jana wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kuanza kusikilizwa, lakini ikashindikana baada ya mawakili wa Hamad, Fancis Stolla na Augustine Kusalika na Job Kyelalio anayetetea Bodi ya Wadhamini CUF kuiambia mahakama kuwa wamewasilisha pingamizi za awali hivyo wanaomba kesi hiyo isianze kusikilizwa.

“Januari mwaka huu tulivyokutana hapa tulikubaliana kwamba kesi hii hadi kufikia Machi iwe imeishatolewa hukumu…leo kesi hii ilikuja kwa ajili ya kuanza kusikilizwa lakini nimeshangaa kuona nyie mawakili wa pande zote mbili eti mmeibuka na pingamizi mkitaka kesi ya msingi isianze kusikilizwa kwanza.

Hizi pingamizi zenu mlizoleta leo mna haki ya kisheria kuzileta ila ninawashauri muachane na mchezo huu wa kuleta pingamizi mara kwa mara kwani husababisha kesi kushindwa kumalizika kwa haraka na mwisho wa siku mahakama inashindwa kueleweka mbele ya jamii,” alisema Jaji Shangwa.

Hata hivyo Jaji alizitaka pande zote kumweleza pingamizi hizo ni zipi ambapo kila wakili alieleza pingamizi lake na mwishowe Jaji akautaka upande wa mlalamikaji kuleta pingamizi lake kwa njia ya maandishi Februari 20 na upande wa mdaiwa kuwasilisha majibu yake Februali 24 na kwamba kesi hiyo itakuja kwa ajili ya kutajwa Februari 28, mwaka huu.

Wakili wa mlalamikaji, Francis Stolla, alisema kuwa wanaiomba mahakama ikitupe kiapo cha mdaiwa ambacho kiliapwa na wakili wake Twaha Tasilima kwa sababu ni batili kisheria kwa kuwa muapaji alipinga madai ya Hamad kuwa amri ya mahakama haikupelekwa katika ofisi za chama, Buguruni Januari 4 mwaka huu saa sita mchana na karani wa mahakama na kikakataliwa kupokelewa na mlinzi wa ofisi hiyo.

Pia aliomba mahakama hiyo ikatae pingamizi la wakili wa mdai lilotaka Hamad aitwe mahakamani hapo ahojiwe kuhusu maelezo aliyoyatoa kwenye kiapo chake ambacho alikitumia kufungulia kesi yake ya msingi kwa sababu ombi hilo limeletwa mapema mno kabla ya ombi la msingi halijaanza kusikilizwa.

Januari 4 mwaka huu saa nne asubuhi, Jaji Shangwa alitoa amri ya muda ya kuzuia Bodi ya Wadhamini wa CUF kuwavua uanachama Hamad na wenzake hadi kesi ya msingi iliyofunguliwa itakapokuja kusikilizwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania la Jumanne, Februali 15 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.