SI KILA MTU ANAFAA KUWA KIONGOZI
Na Happiness Katabazi
KWA muda mrefu miongoni mwa wasomi na wananchi wa kawaida wamekuwa na mawazo tofauti kuhusu viongozi wanapatikanaje na ni hasa anastahili kuwa kiongozi.
Wapo wanaoamini kwamba uongozi ni karama au kipaji anachozaliwa nacho mtu, lakini kuna wengine wanaamini mtu anaweza kufundishwa kuwa kiongozi.Kwa upande mwingine wapo wanaoamini kwamba akiwa na sifa za kuzaliwa na akapewa mafunzo ya uongozi huyo ndiye kiongozi anayefaa.
Lakini wote hawa ukubaliana na jambo moja kwamba si kila mtu hata asiyekuwa na sifa anaweza kuwa kiongozi. Kimsingi kiongozi lazima awe na sifa zinastahili ikiwa ni pamoja na uelewa wa mambo, maono, awe ni mfano bora kwa wanaowaongoza na asiyetanguliza maslahi yake binafsi.
Dunia imebahatika kupata viongozi wenye sifa za namna hii na mifano hao viongozi si ya kutafuta kwa maana ni wengi. Kule Afrika Kusini, kulikuwa na Nelson Mandela, alikuwa na uelewa wa mambo na msomi wa hali ya juu alitanguliza maslahi ya watu wa taifa lake weupe kwa weusi hata akafungwa gerezani miaka 27 kwa sababu hiyo
Tukirejea Tanzania tunaweza kumtaja Baba wa Taifa Julius Nyerere, ambaye alipenda na taifa na watu wake na hata muda mfupi ya kuaga dunia alitamka wazi atawaombea wananchi wa taifa hili kwa mwenyezi mungu. Nyerere aliwahi kusema Ikulu ni mahali patakatifu na pana mzigo mzito wa kuwatumikia wananchi waliona matatizo mbalimbali kama umaskini na kadhalika.
Nyerere alikuwa msomi mbobevu na mwenye shahada kadhaa za vyuo vikuu kadhaa.Mwenye maono, na mwenye msimamo dhabiti katika yale aliyoyaamini. Kiongozi huyu aliyeweza kuibua viongozi wengine wenye sifa kama za kwake na pengine ni za kipekee mathalani marehemu Moringe Sokoine, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa nchi hii.
Nyerere alijenga vyuo vya kuwafunza watu uongozi akijua kwamba anatengeneza uongozi wa baadaye wa taifa lake kwa bahati wanafunzi wake wengi , wamesaliti mafunzo aliyowapa. Taifa letu la Tanzania lilipata bahati kubwa wakati wa uongozi wa Nyerere, viongozi waliheshimika ndani na nje ya nchi.
Waliheshimika kwa sababu walijiheshimu, walifuata maadili, walikuwa na moyo wazalendo na kutanguliza maslahi ya taifa mbele na hawakuwa wabinafsi wala wasanii. Viongozi hawa walipokuwa wakitamka jambo au kutoa maelekezo kwa watendakazi chini yao, wananchi kwa ujumla walisikilizwa na maelekezo yalikuwa yakitekelezwa kwa vitendo bila kupuuzwa.
Leo hii viongozi wetu wengi wanatoa maelekezo wanaishiwa kukosolewa na wananchi na watalaamu mbalimbali.
Lakini kama alivyoimba mwanamuziki maarufu wa muziki wa kizazi kipya Lady J Dee, ‘Siku hazigandi’, enzi za uongozi na viongozi walio na uwezo wa kutupeleka kule kunakostahili hivi leo zinaoneka kama zimetoweka.
Sifa na vigezo vya mtu kuchaguliwa kuwa kiongozi leo hii si tena zile sifa njema, taifa hili sasa linashuhudia watu wakipata uongozi kwa sababu ya mahusiano yao na watu fulani wenye sauti katika jamii na nguvu ya fedha.
Wengine wanakuwa viongozi kwa sababu hapo zamani au hata sasa wana uhusiano wa kimapenzi na wenye mamlaka ya kuteua. Kwa upande mwingine wapo viongozi ambao madaraka yao yametokana na undugu na kiongozi fulani mkubwa, wengine kwa kisingizio cha kufuata nyayo za wazazi wao, waume zao au wake zao na kuwa mabingwa wa fitna.
Kwa kuwa hizi ndio zimeanza kuwa sifa za mtu kupata uongozi wa kiongozi katika taifa letu hii leo tunashuhudia uongozi uliolegalega kwa namna ambayo haijawahi kutokea katika historia ya nchi yetu.
Leo hii viongozi wetu hawasemi kitu kikasikilizwa na watendaji waliopo chini yao wala kikatekelezwa na wananchi ipasavyo. Viongozi wengi wanaonekana kupwaya katika nafasi zao, kwani wengi wanadaiwa hawana uwezo kuwashawishi utendaji kazi na wao wenyewe hawaonekani kumudu majukumu yao.
Cha kustaabisha zaidi baadhi ya viongozi hawaonekani kuwa na mvuto tena wa kusikilizwa na kupata utii unaostahili kutoka kwa wananchi. Hayo yote ni kwa sababu ya viongozi wetu kukosa sifa machoni pa jamii na katika baadhi ya viongozi kuanzia ngazi ya chini tulionao si viongozi wenye uelewa mpana wa mambo, maono, uzalendo na maadili.
Endapo tutaendelea kuwa na viongozi wanaopwaya kiasi hiki, taifa letu litasahau habari ya kutokomeza umaskini na kusonga mbele kimaendeleo sana sana tutapiga hatua kurudi nyuma siku hadi hadi siku.
Lakini hatima ya nchi hii katika suala la uongozi lipo mikononi mwa wananchi,wananchi ndiyo tunatakiwa tusimame sasa na kusema viongozi wasio na sifa sasa basi.
Tufike mahali ambapo hatutamchagua kamwe kiongozi mbinafsi, anayeandamwa na tuhuma za ufisadi, mlaghai, mbumbumbu, asiye na dira wa mwelekeo eti kwasababu tu kundi lake linanguvu kubwa ya kifedha na kutuhonga wapiga kula pilau.
Tena sasa hivi imeibuka mchezo mchafu wa baadhi ya wanasiasa wanautaka urais ,mwaka 2015 kujipitisha katika ,makanisa kuanza kujipigia kambeni na kuwarushia vijembe mahasimu wao.Nasisitiza tena viongozi wa aina hii hawatufai kwani wanamdhihaki mungu pia.
Kama wananchi hatutajali, tukumbuke kuwa dereva asiye na sifa za kuwa dereva akiendelea kupewa usukuni siku atakaposababisha ajali likawa janga la kitaifa, tutakaopoteza uhai ni sisi wananchi na dereva (kiongozi) huyo atatokomea kusikojulikana atakimbilia kule alikohifadhi fedha ambazo yeye na wenzake waliuibia umma.
Ni kweli jamii za wanadamu zinahitaji viongozi na viongozi hao lazima wawe watu. Hivyo ingawa viongozi wote ni watu lakini si kila mtu anafaa kuwa kiongozi.
Yule ambaye hawawezi kufikiri kwamba jamii anayokusudia kuiongoza atafanyia nini, bali anafikiri jamii imfanyie nini hatufai.
Yule ambaye yupo tayari kuuza mwili wake ili apate nafasi ya uongozi hatufai. Yule ambaye yupo tayari kutoa na kupokea rushwa ili apate uongozi hatufai.
Na yule aliyeanza kufanya usanii wa kampeni za kusaka urais wa mwaka 2015 leo hii katika makanisa hapa nchini hatufai kabisa.Yule ambaye anamsingizia uongo mwenzake ili kujipatia uhalali machoni pa wananchi hatufai.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika
0716 774494
www.katabazihappy.blogspot.com
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Februali 14 mwaka 2012
No comments:
Post a Comment