Header Ads

ADHABU MBADALA IAMASISHWE



Na Happiness Katabazi

FEBRUALI 3 mwaka huu, Tanzania ilikuwa ikiazimisha Siku ya Sheria(Law Day) ambayo kitaifa ilifanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam, ambapo Rais Jakaya Kikwete ndiye alikuwa mgeni rasmi ambapo mwenyeji wake alikuwa ni Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman.

Kauli mbiu ya sherehe hiyo ambayo ni ishara ya ufunguzi rasmi wa shughuli za mwaka mpya wa mahakama ni “Adhabu Mbadala katika kesi za jinai :Faida zake”.

Ambapo Rais Kikwete, Jaji Mkuu Othman, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju na Rais wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika(TLS), Francis Stolla ndiyo waliopata fursa ya kusoma hotuba zao ambazo zilijadili kauli mbiu hiyo kwa kina isipokuwa hotuba ya Rais Kikwete ambaye alikuwa wa mwisho kusoma hotuba yake ambayo ilikuwa fupi na alianza kwa kutoa neon la kujiami mapema kuwa yeye siyo mwanasheria kitaaluma kwahiyo hotuba yake haitazungumzia kwa undani masuala ya kisheria kuhusu kauli mbiu hiyo ila anaishauri mahakama itoe elimu na faida kuhusu matumizi adhabu mbadala ili umma uweze kuelewa faida zake.

Jaji Mkuu Othman katika hotuba yake siku hiyo ambayo gazeti hili inayo nakala yake alisema duniani kuna wafungwa na mahabusu milioni 9.8. Leo katika kila Watanzania 100,000 kuna takribani wafungwa na mahabusu 88. Mwaka 2008, walioongoza duniani ni Marekani ambapo kwenye kila watu 100,000 kulikuwa na wafungwa na mahabusu 756 .Hali nchini nyingine ilikuwa hivi:Rwanda 604,Afrika Kusini 335, Uingereza 153 na Kenya 130. Duniani nchi iliyokuwa na idadi ndogo kabisa ya mahabusu na wafungwa ni India ambayo kwa kila watu 100,000 ilikuwa na wafungwa na mahabusu 25 tu.

Alisema Desemba mosi mwaka jana, Tanzania ilikuwa na wafungwa na mahabusu 38,080 .Kati yao wafungwa walikuwa 18,978 na mahabusu 19,102. Uwezo wetu wa hifadhi magerezani ni nafasi 29,552. Matokeo ni wastani wa zaidi ya asilimia 29 ya msongamano pia uwiano kati ya wafungwa na mahabusu kwa muda mrefu umekuwa karibu nusu kwa nusu.

“Idadi kubwa ya mahabusu gerezani ambayo hairidhishi inachangiwa haswa na ucheleweshaji wa uchunguzi wa makosa ya jinai, upatikanaji wa mashahidi, mwendo mrefu wa kesi na mlundikano wa mashauri mahakamani, upatikanaji wa mwenendo wa mashauri na nakala za hukumu kuwezesha rufani kusikilizwa, masharti ya dhamana na uwezo wa watuhumiwa kutimiza masharti ya dhamana”alisema Jaji Othman.

Jaji Othman alisema pamoja na kupungua kwa wimbi kubwa la ujambazi lililotokea wakati serikali ya awamu ya nne ilipoingia madarakani, mwaka 2005 idadi muhimu ya wafungwa magerezani imechangiwa na matokeo ya uhalifu yaliyoainishwa kama adhabu kifungo cha miaka mitano hadi maisha, sheria zinazotoa kama sharti muda maalum wa kifungo(mandatory sentences), sheria zinazoainisha kama amri adhabu za chini za kifungo na mategemezi ya kupindukia ya adhabu ya kifungo kuliko adhabu zisizo kifungo.

“Suala si la idadi tu.Changamoto nyingine ni kwamba nafasi ya kuhifadhi wafungwa na mahabusu magerezani ni ndogo .Bado tuna tatizo sugu la msongamano haswa kwenye magereza ya mjini na usipodhibitiwa , unaweza kuwa adhabu ya pili.Kila mtu aliyetiwa hatiani kisheria na mahakama kwa kosa la jinai anastahili adhabu”anasema.

Jaji huyo alisema kwenye makosa ya jinai Sheria inaipa Mahakama busara ya uamuzi na uwezo wa kutoa kiwango cha adhabu stahili. Busara ya kutoa adhabu ina mipaka.Ikipindukia, mahakama za juu zina uwezo wa kuisahihisha ,aidha adhabu kali au ndogo sana iliyotolewa na mahakama za ngazi za chini na hivyo ndivyo wanavyowajibishana.

Aidha anasema kuna sheria nyingine kama Sheria ya Chini(Minimum Sentence Act,Cap 90), na Sheria Maalum ya Makosa ya Kujamiana(SOSPA) (Sexual Offences Special Provisions Act, 1998) ambazo zimeiondolea mahakama busara ya kutoa adhabu kwa kuainisha kama amri adhabu lazima za kifungo cha muda mrefu. Hilo linahusu makosa kama yale ya kijinsia, ujambazi na wizi wa mifugo.



“Kwa uzoefu wa nchi nyingi kuna njia mbili kuu za kuponyesha msongamano na kuhitimisha malengo ya adhabu.Ya kwanza ni kujenga na kuendelea kujenga magereza kwa kasi zaidi kila hapo idadi ya wafungwa na mahabusu itakapozidi nafasi za hifadhi.Na ukubwa wa magereza ya nchi unapimwa na mambo mawili; watu wangapi wanaoingia na wangapi wanaotoka kila siku”alisema.

Anasema njia zote hizo zina gharama. Kwa upande mmoja , ni zile za serikali kuwahifadhi na kuwailisha walio magerezani ambayo hapa nchini lishe ya kila mmoja wao ni takribani sh 2,300 kwa siku au sh bilioni 32 kwa mwaka na za usimamizi wa magereza. Kwa upande mwingine ni gharama za amani na usalama ambazo jamii itazibeba endapo mhalifu atatumikia adhabu mbadala kwenye jamii.Kwa vyovyote vile jamii ikumbuke kuwa sio kila mhalifu ana stahili adhabu ya kifungo , wengine wanastahili adhabu mbadala.



“Kwenye kutafuta jibu la kudumu inabidi serikali na jamii ipime gharama , madhara na lawama za kifungo gerezani na gharama, madhara na lawama za adhabu mbadala kwenye jamii. Ni ipi kati ya hizo njia mbili ina uwezo zaidi wa kurekebisha wafungwa,haswa wale wenye makosa madogo madogo warisudie tena uhalifu watakapo rejea uraiani,yenye uwezo wa kuwafidia waathirika wa kosa na kulinda jamii.Tukizingatia yote hayo njia muafaka ni kujenga suluhisho linaloweza kujihimili.Hoja siyo tu kuwa mkali wa uhali bali ni kuwa mwerevu wa uhalifu”alisema.

Adhabu mbadala ;alisema wanapozungumzia adhabu mbadala wanamaanisha ni adhabu yoyote ambayo siyo kifungo gerezani.Miongoni mwa malengo na faida za adhabu mbadala ni kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani, kushusha gharama za kuendesha magereza,kumuwezesha mtenda kosa kujiunga tena uraiani kwa urahisi, kumpa nafasi afidie jamii kwa kufanya kazi za maendeleo au za jumuiya na hatimaye kumpa nafasi aweze kuishughulikia familia yake.

Hivi sasa Tanzania inaitaji wafungwa walipa kodi,sio wawe mzigo kwa walipa kodi.

Adhabu mbadala :Amri ya Huduma ya Jamii ; Jaji Othman alisema moja kati ya adhabu mbadala yenye kipaji kikubwa kuhitimisha malengo adhabu humuwezesha mhalifu kujirekebisha na kufidia jamii kwa kosa alilotenda na vile vile kupunguza msongamano ni amri hizi za Huduma ya Jamii chini ya Sheria ya Huduma ya Jamii chini ya kifungu cha 3(1)(a)(b) cha Sheria hiyo, amri hizo hutolewa na mahakama kwa mtuhumiwa aliyetiwa hatiani kwa kosa la jinai ambalo adhabu yake haizidi kifungo cha miaka mitatu pamoja au bila ya faini au kifungo kinachozidi muda huo ambacho mahakama inaona kifungo cha miaka mitatu au chini pamoja au bila ya faini kinastahili amri ya huduma ya jamii.

Makosa hayo ni kama yale ya wizi wa maungoni , kupokea mali ya wizi ,kujipatia mali ay fedha kwa njia ya udanganyifu, kutumia lugha ya matusi ,kufanya fujo au kuvunja amri halali ya mahakama. Anawataka wananchi waelewe mahakama haina mamlaka ya kutoa adhabu mbadala kama hizi, kwenye makosa makubwa ya jinai kama yale ya ubakaji,ujambazi na kupatikana na madawa ya kulevya.

Kazi za jamii zilizoainishwa kisheria ni za kusafisha mazingira, usafi wa mabustani na maeneo ya ofisi za serikali,halmashauri na hospitali,ujenzi wa barabara au shule,kupanda miti na kuchimba mitaro ya maji na kazi hizo lazima ziwe kwa manufaa ya jamii pia kazi hizo hazi a malipo.

“Safari huanza kwa hatua, sheria hii ina upeo lakini bado haijatumiwa kikamilifu.Kwanza ,sheria hiyo inatumika kwenye mikoa 12 tu nayo ni Dar es Salaam, Mtwara,Dodoma,Kilimanjaro,Mwanza,Mbeya,Iringa,mArusha,Tanga,Mara,Kagera na Shinyanga.Pia tangu sheria ianze kufanya kazi mwaka 2005 hadi kufikia Oktoba 2011, ni wafungwa 3144 tu walioadhibiwa amri za huduma ya jamii”alisema.

Aidha anaeleza kuwa viungo muhimu katika utekelezaji wa sheria hiyo ni mahakimu, maofisa wa Huduma Jamii wa Mkoa na Wilaya, Maofisa Magereza,Halmashauri na wale wa serikali za mitaa pamoja na watendaji wa Kata na kuwa mafanikio ya kishindo yatapatikana ikiwa wote watashirikiana na kushikamana.

Kwa upande wake Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alisema kumekuwepo na falsafa nyingi siku hadi siku juu ya aina ipi ya adhabu ambayo inaweza kupunguza au kukomesha uhalifu katika jamii. Falsafa hizi zimegawanyika katika Nyanja mbili.Nyanja moja inasema adhabu ya kifungo jela inafaa zaidi kukomesha au kuzuia uhalifu.Nyanja nyingine inasema adhabu mbadala ndiyo inayofaa zaidi kuliko ile ya kumpeleka jela mhalifu.

Masaju alisema Nyanja hizo mbili uleta mvutano kwa wanafalsafa ,taasisi mbalimbali za serikali na jamii na hata kwa watu binafsi.Kwa ujumla hakuja jibu muafaka juu ya adhabu ipi inaifaa jamii katika kukomesha makosa ya jinai,kwani kila adhabu ina umuhimu na upungufu wake.Jambo la msingi la kuzingatia ni kwamba adhabu yoyote inayolengwa kutolewa ni budi iwe ndiyo yenye manufaa kwa jamii na kwa mhalifu husika kwa wakati huo kutegemeana na jinsi kosa lilivyotendeka.

Masaju alisema wafungwa wanaopelekwa gerezani ni wa makosa yenye aina na uzito mbalimbali.Kuna wafungwa wenye makosa makubwa ambao wamekuwa sugu na hawawezi kubadilika, lakini pia kuna wafungwa ambao ni mara yao ya kwanza kufanya uhalifu na makosa yao ni madogomadogo.Kwa kuyachanganya makundi haya gerezani kundi la mwisho huambukizwa mbinu za kutenda uhalifu wa makosa makubwa huko jela na wakitoka nje hutumia mbinu hizo katika kutenda uhalifu mkubwa katika jamii.Hivyo aina ya makosa yanayostahili kifungo cha jela isipoangaliwa vyema inayafanya magereza yetu kuwa viwanda vya kuzalisha wahalifu sugu.

“Matumizi sahihi ya adhabu mbadala yanaweza kupunguza madhara ya kifungo cha jela endapo adhabu mbadala itawekewa mfumo wa kutumika vilivyo katika jamii yetu.Faida ya adhabu hii kwa kifupi ni kama ifuatavyo huimarisha na kuboresha huduma za jamii, kumwezesha mfungwa kukaa na kuhudumia familia yake,kifungo cha nje huchochea wahalifu kuchukia uhalifu,kupunguza matumuzi ya serikali katika kuendesha kazi za magereza,kupunguza msongamano wa wafungwa gerezani,kuokoa rasilimali watu,kuwaepusha wahalifu wapya kujifunza tabia za uhalifu uliokubuhu”alisema Masaju na kushangiliwa.

Aidha alisema changamoto ambazo inakumbana nazo katika matumizi ya adhabu mbadala ni nyingi na miongoni mwake ni jamii kushahibikia zaidi mila na desturi zinzohusudu adhabu ya kifungo.

“Imekuwa ni desturi ya jamii yetu kuridhika na kung’ang’ania mfumo wa adhabu ya kifungo gerezani hivyo kutaka kila mhalifu apelekwe gerezani.Kutokana na mazoea hayo hata wapo wahalifu ambao nao wanajenga utamaduni wa kuthamini zaidi adhabu ya kifungo kuliko adhabu mbadala ambazo zimewekwa na sheria.Mtu akielewa kuwa akifanya kosa hatafungwa jela kwa mara nyingi haogopi kutenda kosa hilo.

Hiyo ni kwa sababu jela ndiyo mahala pekee panapowatisha watu wote ambao kwa mazoea wanapaswa kuishi kwa uhuru na kujitawala.Mtazamo huo huwafanya hata baadhi ya wadau wanaohusika na utoaji na usimamizi wa adhabu kuhimiza kutolewa kwa kifungo cha jela kuliko adhabu mbadala.

Hata hivyo Masaju alisema baadhi ya watendaji ambao hawana maadili wanatumia adhabu hii kinyume na madhumuni ya sheria.Wanatoa adhabu ndogo isiyostahili kwa minajili ya kutimiza malengo yao maovu ya kujinufaisha wenyewe kwa kupitia utoaji wa adhabu mbadala.Tabia hiyo kwa nyakati Fulani imechangia vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mikononi na kuwaadhibu wahalifu kwa mwamvuli wa watu wenye hasira kali.

Aidha Masaju alimaliza kwa kusema ni vyema umma uzingatie mifumo yote miwili ya adhabu ile ya kifungo na ile kifungo cha nje zina umuhimu wake kulingana na aina za makosa na mazingira ya jamii yetu.Kwa hali hiyo basi adhabu zote ziendelee kutumika kwa lengo linalokidhi mahitaji ya jamii na sheria za nchi ambayo ni kutokomeza uhalifu na kuwa na jamii salama na inayodumisha maridhiano katika Nyanja za kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika(TLS), Francis Stola alisema ni suala la mrundikano wa wafungwa na mahabusu magerezani ni jambo linalosumbua vichwa vya wengi hasa zile taasisi ambazo kimsingi zimebeba jukumu hilo.

Naye Rais Jakaya Kikwete aliita mahakama itoe elimu kwa umma kuhusu faida ya adhabu mbadala na kwamba hakuna ubishi kuwa msongamano magerezani upo, unakera na kwamba anaamini kuwa endapo adhabu mbadala ikianza kutolewa kikamilifu na mahakimu itasaidia kupunguza msongamano.

Rais Kikwete pia alipongeza jitihada za kimaendeleo zilizopigwa na mhimili wa Mahakama chini ya Jaji Othman na akawahidi kuakikisha atakikisha Mfuko wa Mahakama unaongezewa fedha ili mahakama iweze kufanyakazi zake kikamilifu kwani unaposema huru wa mahakama ni pamoja na mahakama hiyo kuwa na fedha za kujiendesha katika majukumu yake.

Sherehe hizo ziliitimishwa kwa Jaji Mkuu Othman kukagua gwaride maalum liloandaliwa na askari wa Jeshi la Polisi, ikiwa ni ishara ya ufunguzi rasmi wa shughuli za mahakama kwa mwaka huu.

0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Februali 5 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.