Header Ads

WASHTAKIWA KESI YA 'SAMAKI WA MAGUFULI'WATIWA HATIANI


Na Happiness Katabazi

FEBRUALI 23 mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,iliandika historia mpya ya kutoa hukumu katika kesi uvuvi haramu maarufu ‘kesi ya Samaki wa Magufuli’ katika ukanda wa bahari ya Hindi katika eneo la Tanzania kwa kutumia meli ya Tawariq 1,ambapo iliwahukumu kwenda jela jumla ya miaka 30 au kulipa faini ya jumla ya shilingi bilioni 22.


Waliotiwa hatiani ni Nahodha , Hsu Chin Tai na wakala wa meli hiyo Zhao Hanguin.Walioachiliwa huru ni ,Hsu Shang Pao, Ca’ Dong Li na Chen Rui Hai ambao walikuwa wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Ibrahim Bendera na John Mapunduzi.

Washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na jumla ya makosa matatu.Kosa la kwanza ni la kuvua samaki bila leseni kinyume na kifungu cha 18(1) cha Sheria Uvuvi katika kina kirefu cha bahari.Kosa la pili ni kuchafua bahari na kuathiri viumbe vilivyomo ndani ya bahari kinyume na kifungu cha 67 cha Sheria hiyo na kosa la tatu ni kusaidia kutendeka kwa kosa hilo hilo la kuchafua bahari.

Sambambamba na kuwapatia washtakiwa hao adhabu hiyo, pia mahakama hiyo ilikubali ombi la Wakili Mkuu wa Serikali Biswalo Mganga ambaye ndiyo aliyekuwa akiliongoza jopo la mawakili wa serikali katika kesi hiyo lilokuwa linaomba mahakama hiyo itoe amri ya serikali iitafishe meli hiyo.

Jaji Agustine Mwarija alisema nahodha na wakala amewatia hatiani katika kosa la kwanza ambalo ni la kufanya uvuvi bila leseni ambapo kila mmoja atalipa faini ya Shilingi Bilioni moja au kwenda jela miaka 20 kila mmoja:

“Katika kosa la pili nimetia hatiani mshtakiwa mmoja tu ambaye ni Nahodha wa meli ambapo atapaswa alipe faini ya Shilingi bilioni 20 au kwenda jela miaka 10, na katika kosa la tatu mahakama hii inawaachiria huru washtakiwa wote kwasababu jamhuri imeshindwa kuthibitisha kosa hilo la kusaidia kutendeka kwa kosa hilo na kwamba adhabu zote hizo zinakwenda pamoja”alisema Jaji Mwarija.

Nasema kesi hiyo ni ya kihistoria kwasababu kesi ya aina hiyo ni ya kwanza kufunguliwa katika mahakama zetu hapa nchini tangu taifa hili lipate uhuru wake mwaka 1961.

Binafsi nilikuwa ni miongoni mwa waandishi wa habari za mahakamani wachache hapa nchini ambao nimeiripoti kesi hii mfululizo tangu ilipofunguliwa kwa mara ya kwanza Machi 2009 pale Kisutu hadi juzi Jaji Mwarija wa Mahakama
Kuu alipotoa hukumu yake.

Na kupitia hukumu hiyo binafsi napenda kutoa pongezi kwa jopo la mawakili wa serikali lilokuwa likiongozwa na Biswalo Mganga kwa kuweza kuithibisha kesi na mwisho wa siku wameweza kuuthibitishia umma kuwa nayo serikali ina mawakili wanaoweza kupambana mahakamani kisheria na mwisho wa siku wakashinda.

Kwani kuna dhana ambayo imejengeka hapa chini kuwa mawakili wazuri ni wale mawakili wa kujitegemea na mawakili wa serikali kuna mawakili wasio wa kitaaluma na mwisho wa siku ndiyo maana wamekuwa wakishindwa kufurukuta katika baadhi ya kesi wanazozifungua mahakamani kwa kishindo.

“Hukumu hii imetufurahisha sisi watanzania kwani tunaamini hukumu hiyo imethibitisha kuwa Tanzania siyo shamba la bibi ambalo kila mtu anakuja anaiba samaki wetu na kuondoka …pia hukumu hii ni somo tosha kwa wale wezi wa samaki katika eneo la nchi yetu ambao wanaingia bahari kinyemela wanavua samaki wetu kwa kutumia meli za kisasa;

‘Na tunapenda kutoa pongezi kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka inayoongozwa na Dk.Eliezer Feleshi kwani kupitia mawakili wake wa serikali Biswalo Mganga, Dk.Deo Nangela, Prosper Mwangamila na Hamidu Mwanga kwani imethibisha bado serikali ina mawakili wenye uweledi wa kutosha katika tasnia ya sheria.

“Pia mashahidi na wapelelezi wa kesi hiyo kwani wamechangia kuuletea upande wa jamhuri ushindi katika kesi hiyo.Pia tunampongeza Waziri wa Ujenzi John Magufuli na mawaziri wenzake wa nchi za maziwa makuuu ambao walipokutana kwenye mkutano wakaazimia kuanza mapambano ya kuwasaka wavuvi haramu na hatimaye boti ya doria ya nchi rafiki iliweza kuwakamata washtakiwa hao wakiwa kwenye meli hiyo wakivua bila leseni:

Maneno hayo yaliyokuwa yakitolewa kwa nyakati tofauti na wananchi wa kada mbalimbali nje ya Mahakama ya Kuu Kitengo cha biashara ambapo hukumu hiyo ilisomwa ,ikiwa ni muda mchache baada ya Jaji Mwarija kumaliza kutoa hukumu yake.

Kwa wale ambao tulikuwa tukiudhuria kesi hii mwanzo mwisho, tutakubaliana kimsingi kuwa kesi hii ilikuwa na mlolongo mrefu wa taratibu kwani mashahidi, mawakili,jaji ,wazee wa baraza walipokuwa wakitoa hoja zao kwa lugha ya Kiswahili ama kiingereza, washtakiwa walikuwa hawaifahamu lugha hiyo, hivyo mahakama iliingia gharama ya kuwaleta wakalimani wa lugha zaidi ya nne kwaaajili ya kutafsiri kutoka lugha ya Kiswahili kwenda katika lugha ya Kiphilipino, Kichina,Kivietena na Kiingereza.

Hali ya mlolongo mrefu wa taratibu ilisababisha baadhi ya miongoni mwa waandishi wa habari wenzangu kuacha kuudhuria kesi hiyo kwa kile walichodai kesi hiyo inawachosha na kwamba wanasubiri siku ikija kutolewa hukumu ndiyo wataiandika.

Itakumbukwa kwamba mengi yalisemwa kuhusu kesi hii wapo waliosema Magufuli alikuwa akijitafuatia umaarufu wa kisiasa kupitia ukamatwaji wa meli hiyo, na wapo waliokuwa wakisema kuwa serikali itashindwa na mwisho wa siku itajikuta ikiwalipa washtakiwa hao fidia kubwa na kwamba fedha za walipa kinatumika kuwagharamia mahabusu hao ambao awali walikuwa 36 gerezani na mshtakiwa mmoja raia wa Kenya alifariki dunia baada ya kugoma kula kwa siku kadhaa.

Maneno hayo yaliyokuwa yakizungumza kichini chini na hata baadhi ya viongozi wa kubwa serikalini kwa njia moja au nyingine yalikuwa yakiwakosesha raha hata baadhi ya mawakili wa serikali waliokuwa wakiendesha kesi hiyo ambao binafsi nilikuwa napata fursa ya kuzungumza na mawakili hao lakini walikuwa wakiniakikishia kuwa wao watajitahidi kitaaluma katika kesi hiyo.

Kupitia hukumu hii serikali na watanzania kwa ujumla inapaswa tuamke na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali na nchi marafiki za kuwasaka wahalifu ambao wanatumia meli zao kuingia kwenye bahari yetu na kutuibia samaki bila sisi kufahamu na inaelezwa uhalifu huo uwaingizia kipata kikubwa sana.

Pia imekuwa ikielezwa kuwa kuna matajiri ambao wanamiliki meli zao kazi yao kubwa ni kujua msimu huu ni msimu wa kuvua samaki, basi matajiri hao uajiri vijana na kupeleka meli hizo bahari na kisha kuvua samaki wa aina tofauti bila kibali cha nchi husika na kisha uenda kuziuza samaki hizo katika mataifa tajiri na huko ujipatia fedha nyingi.

Kwangu mimi nawaona watu wa aina hiyo ni wahalifu kama walivyowahalifu wa makosa ya kuuza dawa za kulevya, unyang’anyi wa kutumia silaha na makosa mengine makubwa tu.Kwani kupitia uhalifu huo wa kuvua samaki bila kibali cha nchi husika ni wazi wanadhurumu rasilimali za nchi husika ambazo rasilimali hizo zikitumika vizuri zinaweza kusaidia kuongeza pato la nchi husika.

Ieleweke wazi kuwa hivi sasa ukitembelea mabucha yanayouza samaki , ule uhakika wa kupata samaki aina ya Sato kwa muda wote hakuna tena kwani aina hiyo ya samaki hivi sasa imeanza kuwa bidhaa hadimu tena bila ya kuwepo kwa taarifa zinazoeleweka.

Novemba 21 mwaka 2011, washtakiwa hao walimaliza kujitetea , ikiwa siku chache baada ya mahakama hiyo kuwaona washtakiwa hao watano wanakesi ya kujibu na kuwaachilia huru washtakiwa 31 kwasababu mahakama iliona hawana kesi ya kujibu.Kesi hiyo imekuwa ikiwahusisha wakalimani wa lugha zaidi ya nne tangu ilipofunguliwa katika mahakama hiyo ya chini hadi mahakama Kuu.

Machi 2009 washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kisha kesi hiyo ikahamishiwa Mahakama Kuu mbele ya Jaji Njegafibili Mwaikugile na kisha ikaamishiwa kwa jaji Razia Sheikh ambaye aliendesha kesi hadi mapema mwaka jana alipojitoa.

Baada ya washtakiwa kumtaka ajitoe kwasababu hawana imani na yeye kwakuwa jaji huyo alitupilia mbali ombi la lilotaka washtakiwa hao wapewe dhamana ambapo jaji huyo alitupilia mbali kwa maelezo kuwa kwa mazingira ya kesi hiyo hawezi kuwapatia dhamana washtakiwa kwasababu washtakiwa hao ni raia wa kigeni na endapo atawapa dhamana wataenda kuishi wapi haki iliyosababisha wakili wa utetezi John Mapinduzi kuwalisha ombi la kumkataa jaji huyo na jaji huyo mwishowe alijitoa na akasema ameamua kujitoa siyo kwasababu ya kukataliwa na wakili Mapinduzi.

Walikuwa wakikabiliwa na makosa ya kuvua samaki bila leseni, kuharibu mazingira katika kina kirefu cha ukanda wa Bahari ya Hindi eneo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusaidia kutendeka kwa kosa hilo.

Mungu ibariki Tanzania ,Mungu ibariki Afrika

0716 774494
www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzaia Daima la Jumanne, Februali 28 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.