Header Ads

SERIKALI ILIBARIKI UNUNUZI JENGO LA UBALOZI-MAHALU

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa serikali ilikuwa ikifahamu suala la ununuzi jengo na ndiyo ilikuwa ikimwagiza kutafuta na kununua jengo la ofisi ya Ubalozi mjini Rome nchini Italia.



Balozi Mahalu alitoa maelezo hayo jana mbele ya Hakimu Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo,Elvin Mugeta wakati alipokuwa akiongozwa kutoa utetezi wake na mawakili wake Alex Mgongolwa, Mabere Marando, Beatus Malima na Cuthbert Tenga ambapo kesi hiyo ikuja jana kwaajili ya mshtakiwa huyo kuendelea kujitetea mfululizo hadi kesho.

Awali kabla ya Mahalu kuanza kutoa utetezi wake wakili mwandamizi wa serikali Ponsian Lukosi, Ben Lincoln waliambia mahakama kuwa wamepata baadhi ya nyaraka za serikali ambazo ni mawasiliano kuhusu ununuzi wa jengo hilo yaliyokuwa yakifanywa na mshtakiwa huyo kipindi kile akiwa balozi nchini Italia na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa iliyokuwa ikiongozwa na Rais Jakaya Kikwete,waziri wa Ujenzi John Magufuri na Katibu Mkuu Kiongozi na serikali kwa ujumla wake ambazo ziliombwa na Mahalu ili aweze kuzitumia kujitetea na kwamba wamepata baadhi ya nyaraka halisi na zile ambazo ni vivuli na kwamba baadhi ya nyaraka ambazo mshtakiwa huyo anazo vivuli vyake wameshindwa kuzipata.

Itakumbukwa kuwa upande wa Jamhuri katika kesi hiyo mwaka juzi, uliambia mahakama hiyo kuwa wao siyo watunzaji wa nyaraka hizo na wala hauna hizo nyaraka ambazo Mahalu alikuwa akiwaomba awapatie hali iliyosababisha Oktoba mwaka jana , mahalu kuanza kujitetea kwa kutumia nyaraka vivuli na mahakama hiyo kuzikubali nyaraka hizo vivuli hali iliyosababisha wakili Lukosi kuiomba mahakama iarishe kesi hiyo ili wawende kuzitafuta nyaraka hizo na hatimaye jana upande wa jamhuri uliweza kuja na baadhi ya nyaraka za mawasiliano kuhusu ununuzi wa jengo hilo ambazo yaliyokuwa yakifanywa na Mahalu na serikali ambazo Mahalu alikuwa akizutumia jana kutolea ushahidi wake.

Alieleza mahakama kuwa kwa Mthamini wa majengo ya serikali M.Kimweli aliandika ripoti yake ya Julai 15 mwaka 2001 kwa serikali ambapo alisema baada ya kufanya ziara yake nchini italia na kufanya tathimini ya majengo matatu, anaishauri serikali ilinunue jengo la Villa kwani jengo hilo ni nzuri na kubwa kuliko majengo mengine yaliyopendekezwa kwani ni jengo la ghorofa moja juu ambalo likinunuliwa na serikali linaweza juu yakawa makazi ya maofisa wa ubalozi na chini ikawa ofisi ya ubalozi.

“Ni kiwa balozi Italia name nilipendekeza kwa serikali tena kupitia barua yangu moja ambayo nilimuandikia Katibu Mkuu Kiongozi, waziri wa wizara ya Mambo ya nje wakati huo alikuwa Kikwete na Wizara ya ujenzi iliyokuwa ikiongozwa na John Magufuli ambapo mwenye jengo aliandika tathimini yake iliyoonyesha jengo hilo lina thamani ya bilioni 11.117,ripoti ya Kimweli ilisema linathamani ya dola za kimarekani 3,000,000.
“Na ripoti ya ubalozi wetu nchini Italia iliandika ripoti yake iliyoonyesha jengo hilo linunuliwe kwa Euro 3,098.034 na kweli serikali ikalinunua jengo hilo kwa bei iliyotajwa sisi maofisa wa ubalozi na ililipa kwa njia ya mikataba miwili”alidai Profesa Mahalu.

Alidai kuwa wakati akiwa balozi aliwahi kufanya mawasiliano ya barua na aliyekuwa waziri wa Mambo ya Nje, Rais Kikwete kuhusu suala ya mikataba miwili ya ununuzi wa jengo hilo na Rais wa wakati huo Benjamin Mkapa alilizindua jengo hilo Februali 2003.

Aidha alidai kuwa Desemba 2001 Rais Kikwete alipokwenda mjini Rome kwenye mkutano wa nchi za SADC, ubalozi wa Tanzania kwa kushirikiana na wizara ya Mambo ya Nje ya Italia, ilimfanyia mpango wa kwenda kulitembelea jumba hilo sambamba na kumkutanisha na muuzaji wa jengo hilo ambaye ni mama wa makamu ambaye walifanya nae mazungu na mtoto wa mama huo ndiyo alikuwa mkarimani kwani mama huyo alikuwa hafamu lugha ya Kiingereza hivyo huyo mtoto ndiyo akawa anatafsiri mazungumzo yaliyokuwa yakizungumzwana Kikwete kwa lugha ya Kiingereza kwenda lugha ya kiitaliano.

“Mimi,maofisa usalama na rais Kikwete tuliudhulia mazungumzo hayo na nilimsikia Kikwete akimshukuru huyo mama kwa niaba ya serikali kuwa anamshukuru kwa kuiuzia jengo zuri kama lile na Yule mama alimweleza Kikwete kuwa jengo hilo ataliuza kwa mikataba miwili kwasababu serikali yetu tena kupitia Kikwete alimuahidi huyo mama kuwa ataakisha akifika Tanzania serikali itamtumia malipo ya awali Euro milioni moja na kwamba fedha hizo atatumiwa kabla ya mwishoni mwaka 2001:

“Baada ya kushukuru Kikwete alicheka na alimweleza mama huyo kuwa anamuarika Tanzania kuja kutembelea mbuga ya Ngorongoro na hiyo ndiyo shukrani yake kwa kwa Tanzania”alidai Mahalu.

Aidha aliendelea kujitetea huku akitumia nyaraka mbalimbali ambazo ni halisi na vivuli alidai na akazisoma nyaraka hizo ambazo zilikuwa zikisomeka na kuonyesha kuwa alikuwa akifanya mawasiliano kuhusu ununuzi wa jengo hilo na serikali ilimpa Baraka zote katika kulitafuta jengo hilo, kulinunua kwa bei hiyo lakini anashangaa serikali hiyo imekuja kumfungulia kesi ya uhujumu uchumi kuhusu ununuzi wa jengo hilo.

Hakimu Mugeta aliairisha kesi hiyo hadi leo ambapo Mahalu ambaye anashtakiwa na Grace Martin katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi anaendelea kujitetea.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Februali 29 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.