WAKILI KIBATALA AWA MAKAMU WA RAIS TLS
Na Happiness Katabazi
WAJUMBE wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika(TLS) kimemchagua kwa kura nyingi wakili wa kujitegemea Peter Kibatala(33) kuwa Makamu wa Rais wa chama hicho.
Wanachama wa chama hicho walimchagua Kibatala kushika wadhifa huo hivi karibuni katika mkutano wa mwaka wa chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa(ICC) mkoani Arusha ambapo Kibatala na wakili Mpare Mpoki ambaye alikuwa akitetea wadhifa wake wa umakamu wa rais waligombea nafasi hiyo na mwisho wa siku Kibatala aliibuka mshindi kwa kupata kura 374 na Mpoki akapata kura 295.
Sambamba na uchaguzi huo wa kiti cha umakamu wa Rais, pia ulifanyika uchaguzi wa kumchagua rais wa chama hicho ambapo aliyekuwa rais wa chama hicho ambaye alikuwa akitetea kiti chake Farancis Stolla alifanikiwa kuibuka mshindi kwa kupata kura za ndiyo 510 na kumshinda kwa mbali mpinzani wake ambaye Protase Ishengoma ambaye alipata kura 116.
Akizungumza na Tanzania Daima kuhusu ameupokeaje ushindi huo, wakili Kibatala ambaye anamtetea aliyekuwa Mgombea Ubunge Jimbo la Segerea(Chadema), Fred Mpendazoe katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ya jimbo hilo ambalo yalimtangaza Dk.Makongoro Mahanga (CCM) kuwa mshindi, alisema ameupokea kwa furaha ushindi huo na anawashukuru wajumbe waliompigia kura za ndiyo kwani kushinda kwake wadhifa huo kumeandika historia mpya katika chama hicho kuwa inashikiriwa na wakili kijana na kwamba anaamini atashirikiana na safu ya uongozi wa TLS kuchapa kazi kwa maslahi ya nchi kwa kutumia msaafu wa sheria.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Februali 23 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment