Header Ads

WASHTAKIWA 'KESI SAMAKI MAGUFULI' JELA MIAKA 30




Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana iliandika historia mpya kwa hatua yake ya kuwatia hatiani washtakiwa wawili wa kesi ya uvuvi haramu katika Ukanda wa Tanzania maarufu ‘Kesi ya Samaki wa Magufuli’ na kuwahukumu kwenda jela jumla ya miaka 30 au kulipa faini ya jumla ya Shilingi bilioni 22.



Sambamba na hilo mahakama hiyo imeridhia ombi Kiongozi wa jopo la mawakili wa serikali lilokuwa likiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Biswalo Mganga aliyekuwa akisaidiwa na Dk.Deo Nangela ,Prosper Mwangamila na Hamidu Mwanga aliloliwasilisha chini ya kifungu cha 351 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 , ambalo aliomba mahakama hiyo itoe amri ya meli hiyo kutaifishwa na serikali ya Tanzania


Washtakiwa katika kesi hiyo ambao walifika mahakamani hapo jana ni Nahodha wa meli hiyo Hsu Chin Tai na wakala wa meli hiyo Zhao Hanguin, Hsu Shang Pao, Ca’ Dong Li na Chen Rui Hai ambao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Ibrahim Bendera na John Mapunduzi.

Jaji Agustine Mwarija ndiye jana aliketi kwenye kiti cha enzi kuanzia saa 4:01-6:45 mchana na kuanza kuisoma hukumu hiyo ambayo ilikuwa
ikisubiriwa kwa shauku kubwa na watanzania wenyewe na mataifa mengine hususani taifa la China ambalo washtakiwa wake watano ndiyo walikuwa wakikabiliwa na kesi hiyo ambayo jana ilitolewa hukumu.

Jaji Mwarija ambaye alianza kusoma hukumu hiyo kwa mtindo wa kukumbusha mashtaka yanayowakabili wa shtakiwa hao, hoja zilizotolewa na mashahidi wa upande wa Jamhuri na mawakili wake na utetezi uliotolewa na washtakiwa wenyewe na mawakili wao ambao ni Ibrahim Bendera na John Mapinduzi na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na upande wa Jamhuri.

Jaji Mwarija alisema washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na makosa matatu:Kosa la kwanza ni la kuvua samaki bila leseni kinyume na kifungu cha 18(1) cha Sheria Uvuvi katika kina kirefu cha bahari.Kosa la pili ni kuchafua bahari na kuathiri viumbe vilivyomo ndani ya bahari kinyume na kifungu cha 67 cha Sheria hiyo na kosa la tatu ni kusaidia kutenda kosa.

Alisema ili mashtaka hayo yathibitishwe alijuliza maswali yafuatayo , je meli hiyo ya Tawariq 1 ilikuwa na leseni ya kuvua? samaki waliokutwa kwenye meli hiyo walikuwa wamevuliwa katika ukanda huo? na washtakiwa hao walivyokamatwa walikuwa ndani ya meli hiyo ambayo inadaiwa kuvua samaki bila leseni?

Jaji Mwarija alisema kwa mujibu wa maelezo ya onyo yaliyotolewa na Hsu Chin Tai (Nahodha) na Zhao Hanguin ambaye ni wakala wa meli hiyo nahodha wa meli hiyo alikiri kuwa ni kweli meli hiyo ilikuwa ikifanya shughuli za uvuvi katika ukanda huo na kwamba ni kweli meli hiyo ilivyokamatwa Machi 8 mwaka 2009 na boti ya askari wa doria wa nchi za Tanzania,Afrika Kusini,Botswana na leseni yake ilikuwa ikimaliza muda wake Desemba mosi mwaka 2008 na kwa upande wake wakala huyo wa meli alikiri kuwa kampuni yake ndiyo iliyoshughulika meli hiyo kutoka Bandari ya Mombasa kuja Tanzania.

Alisema kwakuwa maelezo hayo ya onyo ya washtakiwa hao wawili yameonyesha washtakiwa hao wanakili kuwa meli hiyo ilifanya uvuvi katika katika eneo hilo na kwamba walikuwa wakiitumia leseni hiyo ambayo ilikuwa imeishamalizika muda wake na hivyo wakati meli inakamatwa Machi 3 mwaka 2008 leseni hiyo ilikuwa imeshakwisha muda wake na kwamba tani 296 za samaki na kilo tatu za utumbo wa samaki hao zilikamatwa ndani ya meli hiyo na samaki hao wakiwa wanavuja damu kuwa ni dhahiri washtakiwa hao walitumia meli hiyo kufanya uvuvi katika katika ukanda wa bahari wa Tanzania.

“Mahakama hii baada ya kujiuliza maswali hayo mahakama hii inasema upande wa jamhuri umeweza kuthibitisha kesi yao kwa washtakiwa hao wawili ambao ni Nahodha na wakala na imewaachiria huru washtakiwa watatu kwasababu ushahidi haujawagusa. Nahodha na wakala nimewatia hatiani katika kosa la kwanza la kufanya uvuvi bila leseni ambapo kila mmoja atalipa faini ya Shilingi Bilioni moja au kwenda jela miaka 20 kila mmoja:

“Katika kosa la pili nimetia hatiani mshtakiwa mmoja tu ambaye ni Nahodha wa meli ambapo atapaswa alipe faini ya Shilingi bilioni 20 au kwenda jela miaka 10, na katika kosa la tatu mahakama hii inawaachiria huru washtakiwa wote kwasababu jamhuri imeshindwa kuthibitisha kosa hilo la kusaidia kutendeka kwa kosa hilo na kwamba adhabu zote hizo zinakwenda pamoja”alisema Jaji Mwarija.

Baada ya kuwatia hatiani washtakiwa hao jaji huyo alitoa fursa kwa mawakili wa washatkiwa waseme lolote kabla ya hajatoa adhabu ndiyo wakili Bendera aliinuka kwenye kiti na kupinga hoja wakili Mganga iliyodai serikali imepata hasara katika kuendesha kesi hiyo kwani meli hiyo hipo na samaki walikamatwa na washtakiwa walitoa ushirikiano wa kutosha tangu walipokamatwa hadi jana walipo hukumiwa.

“Mtukufu jaji washtakiwa uliowakuta na hatia ni raia wa kigeni na wamekaa gerezani kwa takribani miaka mitatu sasa na hiyo ni adhabu tosha na siyo tu ni raia wa kigeni bali ni raia wa China ambao China ni nchi rafiki wa Tanzania na Nahodha ni mtu mzima ana miaka 63 na ana familia.

“ …na kwakuwa tayari wakili wa Mganga ameishawasilisha ombi la kutaka meli itaifishwe na kesi hii imekuwa ikiripotiwa sana na vyombo vya habari hali iliyosababisha washtakiwa wamearibika kisaikolojia na kwakuwa serikali haifanyi biashara tunaomba serikali iifanyie tathimini meli hiyo ina gharama ya kiasi gani na kisha mwenye meli aambiwe ailipe serikali gharama hiyo ili serikali isiendelee kubeba mzigo wa kuitunza meli hiyo kwani tayari vyombo vya habari vimeishaanza kuripoti kuwa meli hiyo inayoshikiliwa imeanza kuzama”alidai wakili Bendera.

Jaji Mwarija alisema kuhusu ombi la Wakili Mkuu wa Serikali Biswalo Mganga liloomba meli ya Tawariq 1 ambayo ilikuwa ni kielelezo cha kwanza, itaifishwe, mahakama hiyo imekubali ombi hilo kwa sababu kifungu cha 18(1) cha Sheria ya Uvuvi katika kina kirefu cha bahari ,kinaeleza mahakama ina mamlaka ya kutaifisha chombo kilichotumika kutendea kosa na kwamba katika kesi hiyo meli hiyo ilitumika kufanya uvuvi haramu.

“Nimeangalia mazingira ya kesi hii, meli hiyo imekuwa na maji mengi tofauti na hali hiyo imenifanya niamini meli hiyo ilikuwa ikifanya uhalifu huo katika eneo la Tanzania kwa mbinu za aina yake na meli hiyo imeonyesha ilikuwa haitambuliwi na mamlaka husika:

“….Na hili kukomesha uhalifu wa aina hii mahakama hii itatoa amri ya kuitafisha meli hiyo kuanzia sasa ili iwe fundisho kwa meli nyingine zinazokuja kufanya uhalifu katika Ukanda wa Tanzania na pia sitatoa amri yoyote kuhusu wale samaki waliokamatwa kwenye meli hiyo na kisha wakagaiwa kwenye taasisi mbalimbali za serikali na washtakiwa kama hawajalidhika wana haki ya kukata rufaa ”alisema Jaji Mwarija.

Baada ya hukumu hiyo kutolewa, wananchi mbalimbali waliofika katika Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara wakiwemo watumishi wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na mabaharia wa serikali ambapo hukumu hiyo ndipo iliposomwa ,waliipongeza ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini inayoongozwa na Dk.Eliezer Feleshi kwa ushindi huo kwani ushindi wa kesi hiyo ni wa kihistoria kwani tangu nchi hii ipate uhuru haijapata kufunguliwa kesi ya aina hiyo katika mahakama za hapa nchini na kwamba hukumu hiyo imedhiirisha kuwa Tanzania siyo shamba la bibi ambalo kila mtu anakuja kuvua samaki kiholela.

Kwa upande wake wakili wa utetezi John Mapinduzi alisema anakusudia kukata rufaa katika mahakama ya rufaa dhidi ya hukumu hiyo kwani hawajaridhishwa na hukumu hiyo.

Novemba 21 mwaka jana, washtakiwa hao walimaliza kujitetea , ikiwa siku chache baada ya mahakama hiyo kuwaona washtakiwa hao watano wanakesi ya kujibu na kuwaachilia huru washtakiwa 31 kwasababu mahakama iliona hawana kesi ya kujibu.Kesi hiyo imekuwa ikiwahusisha wakalimani wa ligha zaidi ya nne tangu ilipofunguliwa katika mahakama hiyo ya chini hadi mahakama Kuu.

Machi 2009 washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kisha kesi hiyo ikahamishiwa Mahakama Kuu wakikabiliwa na makosa ya kuvua samaki bila leseni, kuharibu mazingira katika kina kirefu cha ukanda wa Bahari ya Hindi eneo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusaidia kutendeka kwa kosa hilo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Februali 24 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.