Header Ads

KWA HILI, NAMKUMBUKA MEJA JENERALI KALEMBO




Na Happiness Katabazi

JESHI la Ulinzi katika nchi yoyote ile duniani ni chombo maarufu na muhimu sana. Hakuna njia nyingine ya kumwelezea shujaa wa nchi isipokuwa kupitia taswira ya mwanajeshi.

Na ndiyo maana Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ni chombo cha kujivunia kwa kuwa huliletea taifa letu sifa ya ukakamavu, nidhamu na uwezo mkubwa wa ulinzi wa mipaka ya nchi.
Panapotokea maafa, mara zote tegemeo kubwa la raia ni jeshi lao la ulinzi, kwa kuwa wanajeshi wa jeshi hilo ndio wenye sifa, maarifa, mbinu na vifaa vya kuokoa. Na kwa kawaida wanajeshi ni vipenzi wakubwa wa wananchi wao.

Katika mada yangu ya leo nitajadili kuhusu hali ya uchafu na mwonekano mchafu na usiopendeza katika makazi ya wanajeshi wetu wanaoishi katika maghorofa ya JWTZ Mwenge jijini Dar es Salaam.

Kwa wale ambao tunayafahamu maghorofa hayo tangu miaka ya 1980 na wale wanaopita njia katika maeneo hayo kwasasa watakubaliana na mimi kwamba maghorofa hayo hayavutii tena mbele za macho ya watu kutokana na uchakavu, na baadhi ya wakazi wa maghorofa hayo kushindwa kuimarisha usafi ndani na nje ya inalozunguka eneo hilo.

Ningali nikiyakumbuka maghorofa hayo tangu kipindi kile cha miaka ya 1980-1990 maghorofa hayo yalikuwa yanamuonekano mzuri kwani wakazi waliokuwa wakikaa kwenye maeneo hayo walikuwa wakihakikisha wanayafanyia usafi vya kutosha sambamba na kukata majani yanayoota nje ya maghorofa hayo na kuhakikisha chemba za maji machafu hazitiririshi maji machafu ovyo.

Lakini hali ilivyo hivi sasa katika eneo hilo si ya kuridhisha kwani baadhi ya maghorofa hayo nyavu za kuzuia wadudu wasiingie ndani zimelika vibaya sana na hakuna dalili za wakazi hao kuweka nyavu nyingine.

Licha ya nyavu hizo kutokuwekwa na baadhi ya wakazi katika nyumba hizo pia, wengine wanaishi umo utakuta wamening’iniza nguo zao ndani katika madirisha hayo na mwananchi anayepita nyuma ya maghorofa hayo uziona zikiningia.Sasa sijui hizo nguo za ndani ambazo nyingine ni magagulo ndiyo mapazia?

Ukitazama baadhi ya nyumba hizo utajiuliza wameshindwa kupata fedha za kununulia mapazia ya kutundika madirishani kwani tunachokishuhudia sasa ni nguo za ndani ndio zinatawala kutundukiwa kwenye madirisha hayo.Ni aibu sana.

Ukitazama kwenye baadhi ya kuta za maghorfa hayo hivi sasa utaona kuta nyingi zimechorwachorwa na kuandika maandishi yasiyopendeza na watu wasiyojulikana hali inayosababisha kuwaona wanajeshi wanaoishi hapo wameshindwa kuwathibiti wanaofanya vitendo hivyo ambavyo navyo vinashusha heshima ya wanajeshi wetu wanaoishi humo mbele ya machoni kwa raia.

Nyasi zimejiotea kinyemela katika makazi ya eneo hilo na hatuoni dalili ya wakazi wa eneo kuzikata na kuzichoma moto.Lakini wananchi watambue wakati hali hii ikiendelea kutamalaki katika makazi hayo ya wanajeshi wetu, serikali yetu imekuwa katika vita kuutokomeza ugonjwa wa Maralia.

Ileweke wazi kuwa wananjeshi wetu wanaokaa kwenye nyumba za jeshi wanakaa bure katika nyumba hizo yaani hawalipii kodi, na katika hilo misipingani nalo.Lakini mina hoji inakuwaje serikali kwa moyo safi imewapati nyumba bure lakini nyie baadhi ya wanajeshi wetu mnaoishi humo mshindwe kuzitunza matokeo yake mnazivuja ili mwisho wa siku zisidumu kwa muda mrefu?

Hivi watangulizi wenu waliokuwa wakiishi humo wangezifuja, leo hii mngezikuta nyumba hizo bure leo hii?

Je hizo nyumba za umma mnazozifuja kwa makusudi mngekuwa mmezijenga kwa fedha zenu binafsi mngethubutu kuzifuja hivyo?Maana kuna wengine mnaishi kwenye hayo maghorofa lakini mnajenga nyumba zenu uraiaini Je ikitokea wapangaji wenu watakaokuja kupangisha nyumba zenu mkawashuhudia wanazivuja nyumba zenu mtakubalia?

Hivi mpendwaje nyie wanajeshi na askari wetu mnaishi kwenye nyumba za umma bure,halafu mnakubali nyumba hizo zifujwe na nyie wenyewe au familia zenu?

Nafahamu kuwa kuna watu wanaweza kudai kuwa ni muda mrefu sasa wizara ya Ulinzi haijatoa fedha za kukarabati maghorofa hayo, lakini mjiulize hivi siku ugonjwa mlipuko ukitokea au maralia watakaopata madhara wa kwanza si nyie wakazi wa eneo hilo?

Kwahiyo naamanisha kwamba siyo kila kitu sisi watanzania tusubiri serikali itenge fungu, mwanajeshi analipwa mshahara na malupulu kibao hivi anashindwa ni kununua pazia, kununua kopo la rangi kupaka katika nyuma anayoishi?

Mbona wengi wenu mnapata fedha za kunywea pombe katika mabwalo ya jeshi ambazo tena miongoni mwenu tunawashuhudia mkiagiza bia kwa fujo? Au mnasubiri atokee mwandishi wa habari mkorofi aiingie katika makazi hayo kinyemela apige picha inayoonyesha hali halisi halafu kisha azichukue picha hizo azisambaze kwenye mitandao ya kijamii aseme hayo ndiyo makazi ya wanajeshi wote JWTZ ndiyo muanze kuchukua hatua?

Na kustaajabisha ni hawa hawa baadhi ya wanajeshi wanaume wenye vyeo vya chini ambao wanaishi katika maghorofa na kambi nyingine za jeshi ambao wanashindwa kusimamia usafi katika makazi wanayoishi, pindi wanapofika katika vituo vyao vya kazi alfajiri wanakuwa wamevalia sare za JWTZ safi na ushiriki kufanya usafi katika vituo vyao vya kazi kama kupiga deki,kusafisha uwanja na kazi nyingine.

Na hili nalishuhudia karibu kila siku asubuhi ninavyopita pale nje ya Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi Upanga(Ngome), Kikosi cha 521 Hospitali Kuu JWTZ na Kikosi cha 34 na vikosi vingine vya hapa jijini Dar es Salaam.

Na uchafu huu unanifanya ni mkumbuke mzee Meja Jenerali Mstaafu Said Kalembo enzi zile za miaka 1980 akiwa ofisa wa JWTZ alijiwekea utaratibu mkali wa mara moja kwa mwezi wa kukagua usafi katika makambi ya jeshi hapa jijini na ama hakika wakazi tuliokuwa tikiishi kwenye makambi hayo tuliakikisha makambi hayo yanakuwa masafi muda wote.

Kwa wale wanaomfahamu Kalembo, ni binadamu na kiongozi anayependa usafi na ndiyo maana hata alivyokuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, aliweza kuwanyosha wakazi wa jiji kwa kutenga siku moja ya juma ya kila mwananchi kufanya usafi na kweli alifanikiwa jiji hilo hadi anaondoka lilikuwa wakazi wa eneo hilo wataendelea kumkumbuka katika hilo.

Chini ya Uongozi wa Jenerali Davis Mwamunyange kuna hatua za maendeleo zimepigwa na ninapongeza katika hili. Ila namuomba kiongozi huyo wa JWTZ wasikubali kuwafumbia macho wanajeshi wote wanaokaa kwenye makambi ya jeshi kisha wanayafuja kwa makusudi kwa uchafu kwani ,kwani akumbuke baadhi ya makambi hayo yamejengwa kwa fedha za walipa kodi na makazi hayo yakiwa katika hali ya uchafu yatasababisha wananchi kuwadharau wanajeshi wanaishi humo.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

0716 774494: www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania la Jumanne, Februali 21 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.