Header Ads

UPELELEZI KESI YA KIBANDA UMEKAMILIKA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mhariri Mtendaji na wa Gazeti la Tanzania Daima, Absalom Kibanda na mwandishi Samson Mwigamba umeiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Sambamba na hilo Hakimu Mkazi Waliarwande Lema anayesikiliza kesi hiyo jana saa sita mchana alilazimika kuifuta hati ya kukamatwa kwa washtakiwa hao aliyoitoa saa tatu asubuhi wakati kesi hiyo ilipokuja kutajwa baada ya mawakili wa washtakiwa ambao ni John Mhozya, Juvenalis Ngowi na Nyaronyo Kichere kwenda kumfuata hakimu huyo ambaye alikuwa nje ya chumba chake cha kuendeshea kesi kumweleza kuwa washtakiwa hao walikuwepo katika eneo la mahakama hiyo tangu saa mbili asubuhi na walikuwa wamesimama karibu na chumba kilichokuwa kikiendeshewa kesi hiyo lakini hawakusikia karani wala askari polisi akiwaita kuingia mahakamani.

Saa nne asubuhi wakili wa serikali Elizabeth Kaganda aliingia ndani ya chumba hicho cha kuendeshea kesi bila ya washtakiwa na mawakili wao kuwepo na kuieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwamba wanaomba wapangiwe tarehe ya kuja kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa na pia akaiomba mahakama itoe hati ya kukamatwa kwa washtakiwa kwasababu wameshindwa kutokea mahakamani hapo wakati shauri hilo likiendelea na ombi hilo lilikubaliwa na hakimu Lema ambaye aliairisha kesi hiyo hadi Machi 7 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Baada ya Hakimu huyo kuairisha kesi hiyo washtakiwa hao ambao walikuwa wamesimama kwenye kordo ambalo linatazamana na mlango wa chumba ambacho hakimu huyo alikuwa akiendeshea kesi hiyo na hakimu huyo akafunga mlango huo na kuondoka kwenda katika ofisi nyingine iliyopo ndani ya mahakama hiyo na ndipo mawakili washtakiwa wakaanza kumtafuta wakili Kaganda kumweleza hawakusikia kesi yao ikiitwa na kwamba walikuwepo katika eneo hilo la mahakama tangu saa mbili asubuhi.

Kufuatia hali hiyo gazeti ambalo lilikuwepo ndani ya eneo hilo la mahakama tangu saa mbili asubuhi na kuwashuhudia washtakiwa na mawakili wao wakiwa wamesima katika eneo la maegesho ya magari na kisha washtakiwa hao na mawakili hao wakaenda kusimama katika eneo la mapokezi la mahakama hiyo ambalo limepakana na chumba anachoendeshea kesi hakimu huyo kwa muda wote huo hadi pale walipokuja kuelezwa kuwa kesi hiyo imeishamalizika bila ya wao kuwepo mahakamani na kutokana na hali hiyo hakimu Lema ametoa hati ya kukamatwa kwa washtakiwa na kwamba Lema ameishatoka ofisini kwake.

Hali iliyosababisha mawakili washtakiwa hao kuanza kuhaha kumsaka Hakimu Lema ambaye alikuwa amekwenda kwenye ofisi nyingine iliyopo ndani ya mahakama hiyo na kufanikiwa kumpata na kumweleza kuwa wao na washtakiwa walikuwepo ndani ya viwanja vya mahakama hiyo tangu saa mbili asubuhi na kwamba hawakusikia kesi yao ikiitwa na ilipofika saa sita wakili wa serikali Kaganda aliwaita mawakili wa washtakiwa na waandishi wa habari na kuwaeleza kuwa amekubali maelezo ya mawakili washtakiwa na kwamba ile amri aliyoitoa ya kukamatwa kwa washtakiwa kwa kushindwa kutokea mahakama ameifuta.

Desemba 21 mwaka jana, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo na wakili Kaganda alidai wanakabiliwa na kosa moja la kuwashawishi askari na maofisa wa jeshi la polisi, magereza na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) kutoendelea kuitii serikali iliyopo madarakani kwa sasa ambayo inaongozwa na Rais Jakaya Kikwete kinyume na kifungu cha 46(b),55(10(a) na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Wakili Kaganda alidai Novemba 30 mwaka huu,gazeti la Tanzania Daima la siku hiyo toleo Na.2553 lilichapisha waraka uliokuwa na kichwa cha habari kisemacho “Waraka Maalum kwa Askari wote” ambao uliandikwa na mshtakiwa huyo kupitia safu yake ijulikanayo kwa jina la ‘Kalamu ya Mwigamba’.

Alidai kupitia walaka wake huo kwa makusudi na kwa nia kuvunja sheria za mamlaka ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliwashawishi askari na maofisa wa jeshi la polisi, Magereza na JWTZ kutoendelea kuiiti serikali iliyopo madarakani.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Februali 16 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.