Header Ads

DOWANS YAIBWAGA TENA TANESCO MAHAKAMANI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali ombi la Shirika la Umeme (TANESCO) lilokuwa linaomba mahakama iwaruhusu kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa nchini kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa Septemba 28 mwaka jana,ambayo iliruhusu tuzo ya Kampuni ya Dowans iliyopewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuhuhishi wa migogoro ya Kibiashara(ICC) isajiliwe hapa nchini kwasababu hiyo haina mamlaka ya kuwaruhsu kwenda katika mahakama hiyo ya juu nchini.

Tuzo hiyo ya dola za Marekani milioni 65 (takriban sh bilioni 94) iliyotolewa Novemba 15, mwaka (2010); tuzo na (ICC).

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Dk.Fauz Twaibu wakati kesi hiyo ilikuja kwaajili ya kutoa uamuzi kuhusu pingamizi la awali lilowasilishwa na wakili wa mdaiwa (Dowans), Kennedy Fungamtama ambalo liliomba mahakama hiyo itupile mbali ombi la mlalamikaji lilokuwa linaomba mahakama hiyo iwapatie kibali cha cha kwenda kuikatia rufaa hukumu iliyotolewa na Jaji Emilian Mushi wa mahakama kuu, Oktoba mwaka jana.

Jaji Dk.Twaibu alisema baada kusikiliza hoja za pande zote mbili anatupilia mbali ombi hilo kwasababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kuwaruhusu kwenda kukata rufaa mahakama hiyo ya juu na kwamba Tanesco bado wana njia nyingine ya kufika mahakama ya rufaa na siyo njia hiyo waliyoitumia ya kuomba ridhaa katika mahakama kuu kukata rufaa na uamuzi huo unatokana na mazingira halisi ya kesi hiyo yalivyo.

“Kutokana na mazingira ya kesi hii na tangu ilipofunguliwa kule ICC, mkataba ulioingiwa na pande hizi mbili umenifanya nifikie uamuzi wa kulikataa ombi la Tanesco na ninaiarisha kesi hii hadi Machi 18 mwaka huu, mahakama hii siku hiyo itakuja kulisikiliza ombi la Tanesco linalotaka mahakama hiyo itoe amri ya kusitisha utekelezwaji wa hukumu ya mahakama kuu ambayo iliisajili tuzo ya Dowans”alisema Jaji Twaibu.

Oktoba mwaka jana, Tanesco waliwasilisha ombi hilo lililokataliwa jana kutaka waruhusiwe kukata rufaa katika mahakama ya rufaa na Januari mwaka huu, wakili wa Dowans ,Fungamtama aliwasilisha pingamizi hilo la awali ambalo jana lilitolewa uamuzi huo.

Kuwasilishwa kwa ombi hilo mbele ya Jaji Twaibu na Tanesco kupitia wakili wa kampuni ya uwakili ya Rex Attoney ,Hawa Sinare ,kulitokana na hukumu ilitolewa na Jaji Emilian Mushi , Septemba 28 mwaka jana alikubali ombi la Dowans la kusajili tuzo waliyopewa na ICC isajiliwe na mahakama ya Tanzania. aidha, jaji aliiamuru TANESCO kulipa gharama zote za uendeshaji wa kesi hiyo, na Dowans ianze taratibu za kukazia hukumu ya Mahakama ya ICC.

Jaji Mushi alisema baada ya kuipitia hukumu ya ICC amebaini kuwa haina makosa ya kisheria kama anavyodai mlalamikaji, na ndani ya hukumu hiyo alikuta kiambatanisho ambacho ni mkataba kati ya TANESCO na Dowans uliosainiwa Juni 23, mwaka 2006; na kufafanua kwamba pande zote mbili katika mkataba huo zilikubaliana kwamba uamuzi wa ICC ndiyo utakuwa wa mwisho, na utazibana pande zote mbili na hautaweza kukatiwa rufaa.

Jaji huyo alisema kifungu cha 14 (f) cha mkataba huo kinasomeka hivi: “The parties waive any right to challenge or contest the validity or enforceability of this arbitration agreement or any arbitration proceeding or award brought in conformity with this section.” Kwa tafsiri nyepesi, Fungamtama alisema kifungu hicho kinasema, TANESCO na Dowans katika mkataba wao walikubaliana kwa maandishi kuweka kando haki za kupinga au kuhoji mwenendo na tuzo zitakazotolewa na baraza la usuluhishi.

Jaji akasema: “Sasa kwa mujibu wa mkataba huo ni wazi kuwa TANESCO na Dowans walikubaliana kuwa endapo utatokea mgogoro baina yao utapaswa upelekwe ICC tu na ICC itakapotoa hukumu ya mgogoro baina yao, pande hizo mbili hazitakuwa na mamlaka ya kuikatia rufaa hukumu hiyo ya ICC.

Jaji alisema hoja ya TANESCO kuwa mwenendo wa hukumu ya ICC ulikuwa na mapungufu ya kisheria, haikupaswa kupelekwa mbele yake kwani Tanasco walikuwa ni wadaiwa katika kesi iliyofunguliwa ICC na walipaswa kuiwasilisha hoja hiyo ICC kabla ya mahakama hiyo ya kimataifa kutoa hukumu yake na kuikumbusha TANESCO kuwa ni yenyewe iliyoingia mkataba wa POA na Dowans ambao kwa ridhaa yao waliridhia kuwa hukumu itakayotolewa na ICC haitakatiwa rufaa.

Septemba 6 mwaka huu, Jaji Emilian Mushi alitoa uamuzi wa kuyatupilia mbali maombi ya wanaharakati waliokuwa wakiongozwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ambao waliiomba mahakama hiyo ikatae kusajili tuzo iliyotolewa na Mahakama ya ICC kwa kampuni ya Dowans Holdings SA(Costa Rica) na Dowans Tanzania kwa sababu wanaharakati hao hawana haki wala mamlaka ya kupinga hilo.

Mahakama ya ICC ilitoa hukumu ya kesi ya Dowans dhidi ya TANESCO, Novemba 15 mwaka jana baada ya kampuni hiyo kuishinda TANESCO katika kesi yake ya kudai fidia ya kuvunjiwa mkataba iliyokuwa imefunguliwa rasmi Novemba 20 mwaka 2008 na kupewa Na. 15947/VRO ambapo Mahakama ya ICC iliitia hatiani TANESCO kwa kosa la kuvunja mkataba na Dowans na ikaiamuru iilipe fidia ya dola za Marekani milioni 65 na riba ya asilimia 7.5.

Hukumu hiyo ya ICC, muda mfupi baada ya kutolewa ilizusha malumbano makali baina ya wananchi, wanaisiasa, mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa kauli zinazopishana huku wachache wakitaka serikali iilipe Dowans na wengine wakisema kulipwa fidia kampuni hiyo ni ufisadi.

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, ndiye aliyekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari kuhamasisha umma na serikali isiilipe Dowans. Kwa upande mwingine, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Fredrick Werema na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, walitaka Dowans ilipwe, hali iliyosababisha baadhi ya wananchi kuwashambulia kwa maneno makali wale wote waliokuwa wakitaka Dowans isajiliwe kisha ilipwe tuzo yao.

Malumbano hayo nje ya mahakama yalisababisha pia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuunda Kamati ya Wabunge kujadili hukumu hiyo na kisha wabunge watatu wa chama hicho, George Simbachawe (Kibakwe), Mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes, Mbunge wa Viti Maalumu, Angellah Kairuki na raia wengine wanne kufungua kesi ya Kikatiba Na. 5/2011 dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na TANESCO ambayo imeanza kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Njegafibili Mwaikugile, Agustine Shangwa na Projest Rugazia.

Kwa mujibu wa hati ya madai, walalamikaji hao wanaiomba mahakama itoe amri ya kuizuia serikali isiilipe Kampuni ya Dowans na endapo malipo hayo yatafanywa kwa kampuni hiyo ni wazi wadaiwa hao ambao wanaiwakilisha serikali kwa ujumla watakuwa wamevunja ibara 26(2),27(1) na 27 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambazo mahakama hiyo ina wajibu wa kuilinda ibara hizo zisivunjwe.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Februali 21 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.