Header Ads

MARANDA AANZA KUJITETEA KESI YA EPA

Na Happiness Katabazi

MWEKA HAZINA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma, Rajabu Maranda, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa alichokizingatia katika mchakato wa kudai deni katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu ya Tanzania ni kupata fedha na si kutazama nyaraka.


Maranda alitoa maelezo hayo mbele ya jopo la mahakimu wakazi, Saul Kinemela, aliyekuwa akisaidiana na Elvin Mgeta na Focus Bambikya ambapo jana ilikuwa ni mara yake ya kwanza kupanda kizimbani kujitetea katika kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8 katika akaunti ya EPA, inayomkabili yeye na binamu yake Farijala Hussein.

Akiongozwa na wakili wake, Majura Magafu, kutoa ushahidi wake ambapo ushahidi aliokuwa akiutoa ulikuwa ukitofautiana na vielelezo vya upande wa mashtaka na maelezo aliyoyatoa wakati alipohojiwa kwenye Tume ya Rais ya Kuchunguza Wizi wa EPA, alidai kwamba yeye aliweka umuhimu katika kupata fedha toka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwanza na si kutazama nyaraka ambazo ni hati ya idhini ya kudai deni la kampuni ya BC /Cars Export ya Mumbai India na hati za usajili wa kampuni yao ya Kiloloma&Brothers iliyotolewa na BRELA kwa sababu nyaraka hizo zilikuwa zimeshapokelewa na Farijala.

Maranda alidai licha ya kutokuwa makini kuzikagua nyaraka hizo pia alikana madai ya kuibia BoT na kusisitiza fedha hizo aliingiziwa kihalali kwenye akaunti yake na akakana kuitambua kampuni ya Kiloloma & Brose Enterprises ila akakiri anaitambua kampuni ya Kiloloma &Brothers ambayo yeye ni miongoni mwa wamiliki wake.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati Magafu na Maranda:

Wakili: Unadaiwa ulijipatia ingizo la sh bilioni 1.8 kwenye akanti yako mkijidai mmepewa idhini na kampuni hiyo ya India. Ieleze mahakama ukweli ni upi?

Maranda:Nakumbuka mwaka 2005 Farijala alikuja na mtu aitwaye Charles Issac Kissa, akamtambulisha kwangu na Kissa akanieleza ana shida anaomba nimkopeshe sh milioni 500, kwani alikuwa amepewa kazi na BC/Cars ya kudai deni lake ambalo walikuwa wakiidai BoT kwa miaka 20.

Nilimuuliza dhamana yake nini akasema hana, hivyo nikamshauri aende benki akaonyeshe nyaraka zinazoonyesha amepewa kazi hiyo.

Wakili:Baada ya Kissa kushindwa kupata kitu cha kuweka dhamana, alifanyaje?

Maranda:Nilimshauri aende nyumbani akatafakari na atuuzie ile kazi yake ili sisi tudai lile deni zima na atukabidhi sisi kwa yule anayedai ili mimi na Farijala tudai na yeye akataka atuuzie kampuni yake ya Kiloloma&Brother, lakini sisi tulikataa kwani hatukujua mbeleni kungetokea nini.

Ninakumbuka siku hiyo hatukfikia mwafaka aliporudi kesho yake akasema alikuwa tayari kukubaliana na sisi kwa utaratibu kwamba amana yake atupatie nusu na tukafungue akaunti pamoja ili siku deni likilipwa atupatie fedha zetu na tulikubaliana naye kwani tuliona hilo ni la msingi.

Wakili:Hii kampuni ya Kiloloma &Brothers nani alikuwa mmiliki wake?

Maranda:Charles Issack Kissa. Na tulikubaliana naye na tukamwambia Kisssa aende BRELA akaingize jina langu na la Farijala kama wamiliki pia wa kampuni hiyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa,Aprili 16 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.