Header Ads

MAJAJI WAITOA JASHO SERIKALI KORTINI DAR

.RUFAA YA MGOMBEA BINAFSI

Na Happiness Katabazi

NAIBU Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, amedai kuwa hakuna mahakama yoyote nchini ambayo inaweza kusikiliza kesi ya kutaka kuwepo kwa mgombea binafsi.


Masaju ambaye anasimama kwa niaba ya serikali, alitoa dai hilo jana mbele ya jopo la majaji saba wa Mahakama ya Rufaa nchini lililokuwa likiongozwa na Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani, aliyekuwa akisaidiwa na majaji Januari Msofe na Eusebio Munuo.

Majaji wengine wanaosikiliza rufaa hiyo ambayo kesi ya msingi ilifunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila ni Nataria Kimaro, Mbarouk Mbarouk, Sauda Mjasiri na Bernad Ruhanda waliokuwapo wakati mwanasheria huyo akiwasilisha hoja zake za kupinga hukumu ya Mahakama Kuu.

Akiwasilisha hoja zake mbele ya jopo hilo, ambalo jana lilianza kusikiliza rufaa ya kupinga kuwepo mgombea binafsi nchini na huku akitumia kesi mbalimbali zilizotolewa na Mahakama Kuu ya India, Kenya na Malawi na huku akikabwa na maswali ya mara kwa mara toka kwa jopo hilo yaliyokuwa yakimlazimisha atoe hoja zake kwa vielelezo na si vinginevyo. Masaju alidai, Mahakama Kuu ilikosea katika hukumu yake kwa sababu hapa nchini hakuna mamlaka yenye uwezo wa kusikiliza kesi hiyo isipokuwa majukwaa mbalimbali (forums).

Masaju alidai sababu nyingine ya wao kupinga hukumu hiyo, ni kwamba Mahakama Kuu ilijipachika mamlaka ya kibunge ya kutunga sheria.

Mbali ya hilo, Masaju alidai pia kuwa katika hukumu yake Mahakama Kuu ilikosea kisheria kwa kuiweka Katiba ya nchi katika vyombo vya kimataifa na pia ilikosea kuitolea maamuzi kesi hiyo bila kuweka suala hilo bayana, hivyo akaiomba mahakama hiyo ya rufani kutengua hukumu hiyo kwa gharama.

Hata hivyo, majaji hao kwa nyakati tofauti walimkatisha Masaju kuwasilisha hoja zake na kumkumbusha kwamba madai yake kuwa Mahakama Kuu ilikosea kutumia sheria za kimataifa zinazohusu haki za binadamu yalikuwa yakiacha maswali.

“Lakini mbona wewe wakati unawasilisha hoja zako na ulikuwa unatumia kesi za India, Malawi ili zikusaidie kuunga mkono hoja zako na kwa maana hiyo nawe unapofanya hivyo unakosea?

“… Hizo hukumu zilizotolewa na Mahakama ya India na Malawi uliyoitumia na unaomba mahakama iitumie kufikia maamuzi yake umeisoma yote na tumekusikiliza sana ukisema hapa nchini hakuna mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hii ikiwemo hata Mahakama ya Rufaa ambayo miongoni mwa majaji wake ni sisi ambao ndiyo tunaisikiliza rufaa hiyo lakini umeshindwa kabisa kutueleza ni mahakama ipi inastahili kusikiliza kesi hii na kama unasema hakuna mahakama ya kusikiliza kesi hii mbona Mwanasheria Mkuu amekata rufaa katika Mahakama ya Rufaa?” walihoji majaji hao.

Maswali hayo yalisababisha umati wa watu waliohudhuria katika Ukumbi Namba Moja wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuangua vicheko na Naibu Mwanasheria Mkuu huyo kukaa kimya na kuishia kujifuta jasho mara kwa mara tangu alipoanza kuwasilisha hoja zake saa 3:00 asubuhi hadi saa 6:30.

“Umedai huridhiki na hukumu ya Mahakama Kuu kwa sababu ilitumia sheria za vyombo vya kimataifa, sasa sisi tunakutaka uisome Ibara 9 (f), 30 (3) (5) 108 (1) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, usome kwa sauti zinasemaje;

“Ibara ya 9(f) inasema kwamba ‘heshima ya binadamu inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata Kanuni za Tangazo la Dunia kuhusu haki za Binadamu. Ibara 30 (3) inasema; “mtu yeyote anayedai kuwa sharti lolote katika Sehemu hii ya Sura hii au katika sheria yoyote inayohusu haki yake au wajibu kwake, limevunjwa, linavunjwa au inaelekea litavunjwa na mtu yeyote popote katika Jamhuri ya Muungano, anaweza kufungua shauri katika Mahakama Kuu.

“Na ibara 30 (5) inasema; ‘Endapo katika shauri lolote inadaiwa kwamba sheria yoyote iliyotungwa au hatua iliyochukuliwa na serikali au mamlaka nyingine inafuta au inakatiza haki, uhuru na wajibu muhimu zitokanazo na ibara ya 12 hadi 29 za Katiba ya Nchi hii, na Mahakama Kuu inaridhika kwamba sheria au hatua inayohusika, kwa kiwango inachopingana na Katiba ni batili au kinyume cha Katiba basi Mahakama Kuu ikiona kuwa yafaa au hali au masilahi ya jamii yahitaji hivyo, badala ya kutamka kuwa sheria au hatua hiyo ni batili, itakuwa na uwezo wa kuamua kutoa fursa kwa ajili ya serikali....” Masaju alinukuu ibara hizo.

Baada ya kumaliza kuzisoma, majaji hao walimuuliza kama bado anaendelea kusimamia hoja zake zinazodai Mahakama Kuu haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi ile na ilikosea kutumia sheria za nje katika hukumu ile wakati Ibara ya 9(f) ya Katiba ya nchini inatamka wazi kwamba Tanzania imeridhia utekelezaji wa Tangazo la Dunia kuhusu haki za Binadamu na kwamba ibara ya 30(3)(5) zinaainisha wazi Mahakama Kuu ina mamlaka hayo ya kusikiliza kesi hiyo na kutamka sheria ni batili kwa mujibu wa Kanuni na Tamko la Haki za Binadamu?

“Mmmh! Mbona nimeishasema sana hapa kwamba Mahakama Kuu na hata hiyo Mahakama Rufaa haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, Tanzania ni taifa hivyo lina sheria zake kwa hiyo kitendo cha Mahakama Kuu kutumia sheria za nje katika hukumu ile ni kuvunja Katiba ya nchi na walikiuka viapo vyao walivyoapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo wakati wanaapa waliahidi kuhifadhi Katiba ya nchi,” aliendelea kudai Masaju na kusababisha watu kuangua vicheko vya chinichini.

Majibu hayo ya Masaju yalisababisha Jaji Mkuu amtake aendelee kurudia matamshi yake kwa kusema wao ni wagumu kuelewa hivyo aendelee kurudiarudia ili wamuelewe, hatua ambayo ilisababisha vicheko tena ndani ya chumba cha mahakama.

Masaju aliendelea kudai kwamba majaji watatu wa Mahakama Kuu ambao walitoa hukumu ile Salum Massati (sasa Jaji wa Mahakama ya Rufani), Jaji mstaafu Amir Manento na Thomas Mihayo (mstaafu) walivunja Katiba na kuongeza kuwa anashangazwa na kuhumu ile na akaifananisha na hukumu zinazotolewa na mahakimu.

Hakuishia hapo alikwenda mbele zaidi na kudai kuwa hukumu ya majaji hao watatu ni yao na si ya Watanzania wote kwani miaka ya nyuma yalishakusanywa maoni ya kutaka uwepo wa mgombea binafsi lakini asimilia 92 ya wananchi walikataa.

Maelezo hayo ya Masaju yalisababisha Jaji Mkuu Ramadhani alazimike kutumia mfano wa maoni ya asilimia 80 ya wananchi waliotaka mfumo wa chama kimoja uendelee mbele ya Tume ya Jaji Francis Nyalali, jambo ambalo hata hivyo lilipingwa na serikali na kusababisha kuanza kutumika kwa mfumo wa vyama vingi.

Kutokana na maelezo hayo, Jaji Mkuu alisema hoja ya Masaju kuhusu maoni ya wananchi walio wengi kukataa mgombea binafsi haina msingi katika rufaa hiyo.

Wakipangua hoja za Masaju, mawakili wa mjibu rufaa, Richard Rweyongeza na Mpare Mpoki, walianza kwa kuiomba Mahakama ya Rufani itupiliwe mbali rufaa hiyo kwa gharama.

Wakifafanua walidai, hoja kwamba, Mahakama Kuu ilitumia sheria za nje siyo ya msingi kwa sababu Ibara ya 9(f) ya Katiba ya nchi inaitaka itumie sheria hizo hivyo ibara hiyo haikuwekwa kwenye Katiba kama pambo bali iliwekwa ili itumike kikamilifu na kwamba Mahakama Kuu ilitoa hukumu sahihi.

Akiichambua hoja kwamba Mahakama Kuu ilijipachika jukumu la kibunge la kutunga sheria, Rweyongeza na Mpoki ambao walikuwa wakiwasilisha hoja zao kwa vielelezo, walisema hoja hiyo haina msingi kwani Mahakama Kuu imepewa mamlaka chini ya Ibara 30 (5) ya Katiba na katika hukumu ile Mahakama Kuu haikutunga sheria, ila ilielekeza hitilafu iliyoiona katika Ibara 21 (1) (c), 39 (1) (c) (b) na 69 (1) (b) ya Katiba ya nchi na ilitoa muda ibara hizo zirekebishwe.

“Hivyo dai kwamba Mahakama Kuu ilijipachika jukumu la kibunge na kutunga sheria si la msingi ...ila tunakubali Bunge lina mamlaka ya kutunga sheria zinazofaa kama ilivyoainishwa kwenye Ibara ya 28 (2) ya Katiba, lakini Bunge halina mamlaka ya kubadilisha misingi ya Katiba lakini kitendo cha Bunge kuweka ibara ya 21 (1) (c), 39 (1) (C) katika Katiba ya nchi limevunja misingi ya Katiba hivyo Bunge ndilo lilivunja Katiba na siyo Mahakama Kuu.

“Ni rai yetu kwa hayo niliyoyaeleza hapo juu kumbe Mahakama Kuu ina mamlaka pindi inapoona kifungu fulani cha sheria kinapingana na Katiba kifanye nini? Kumbe uamuzi uliofikiwa na Mahakama Kuu ulikuwa ni kitu kizuri kwani ilifikia hukumu ile ya kuwepo kwa mgombea binafsi kwa sababu ilichokifanya kipo ndani ya ibara ya 30 (5) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alidai Rweyongeza.

Baada ya pande zote mbili kumaliza kuwalisha hoja hizo, Jaji Mkuu aliahirisha kesi hiyo hadi leo ambapo marafiki wa mahakama akiwemo Mkuu wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Paramagamba Kabudi na Profesa Jwani Mwaikusa, watatoa maoni ya kuishauri mahakama kuhusu rufaa hiyo.

Mara ya kwanza, serikali ilikata rufaa dhidi ya hukumu ya Mahakama Kuu, katika mahakama hiyo ya rufaa mwaka 2007, ambapo ilidai mahakama hiyo ya chini ilikosea kisheria kutafsiri Ibara ya 21(1)(c), 39(1)(c) (b) na 69(1)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977.

Hata hivyo, rufaa hiyo ilitupwa na Mahakama ya Rufaa baada ya mahakama hiyo kukubaliana na ombi la wakili wa Mtikila, Richard Rweyongeza, kwamba rufaa hiyo haina msingi na kwamba imejaa dosari za kisheria.

Awali katika hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa Mei 2006, iliruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi katika uchaguzi, kwa sababu Katiba ya nchi inatoa haki hiyo.

Mwaka 1993, Mtikila alishinda kesi kama hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma iliyokuwa ikisikilizwa na Jaji Kahwa Lugakingira, lakini licha ya uamuzi huo, serikali ilipeleka bungeni muswada wa kupinga hukumu hiyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Aprili 9 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.