Header Ads

MKURUGENZI WA EASY FINANCE KORTINI

Na Happiness Katabazi

MMOJA wa wakurugenzi wa Kampuni ya kutoa mikopo nchini ya Easy Finance, Aloycious Gonzaga (43) na mkewe, Magreth Gonzaga (38), jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka manne ya kula njama na kuwasilisha hati ya kiwanja ya kughushi na kisha kujipatia isivyo halali sh milioni 50.


Mbali ya washitakiwa hao ambao ni mke na mume, mshitakiwa mwingine ni Anthony Patrick (25), ambaye ni mshitakiwa wa kwanza.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Salome Mwandu, Mwendesha Mashitaka, Inspekta Emma Nkonya, alidai kuwa washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka manne.

Alidai shitaka la pili ni kughushi, ambapo Desemba 31 mwaka jana katika Kampuni ya uwakili ya Solanus Mhenga hapa jijini walitenda kosa la kula njama kughushi hati ya kibali cha kugawa kiwanja Na. 27005, kitalu 201, Mbezi Beach na kujaribu kuonyesha hati hiyo ni halisi na imetolewa na Msajili wa Ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Inspekta Nkonya alidai shitaka la tatu ni la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, ambapo shitaka hili linamhusu mshitakiwa wa kwanza Patrick, kwamba mnamo tarehe na mwaka huo katika Skyline General Business International Ltd kwa makusudi alijipatia sh milioni 50 kutoka kwa Jackson Swai kwa kumuuzia kiwanja hicho kilichopo kitalu Na. 27005 Mbezi Beach, huku akijua hati hiyo ya kiwanja ni ya kughushi.

Alidai shitaka la nne ni la kuwasilisha nyaraka za kughushi, kwamba Patrick akiwa katika ofisi za Skyline General Business International Ltd zilizopo Mtaa wa Livingstone hapa jijini aliwasilisha nyaraka hizo za kughushi kwa lengo la kuonyesha hati hiyo ya kibali cha kugawa kiwanja ni halisi.

Hata hivyo washitakiwa wote walikana mashitaka yote na Hakimu Mkazi Mwandu akitoa masharti ya dhamana, alisema ili mshitakiwa apate dhamana ni lazima awe na wadhamini wawili wa kuaminika na mmoja kati yao awe ni mfanyakazi wa serikali, ambao watasaini bondi ya sh milioni 40 kwa kila mshitakiwa mmoja na walitimiza masharti ya dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 14 mwaka huu.

Wakati huo huo, wafanyakazi watatu wa Benki ya Stanbic, Grace Mushi, Gerald Msegeya na Robi Nyamhanga na mfanyabiashara, Nyakaliro Mauma, walifikishwa mbele ya hakimu huyo wakikabiliwa na mashitaka manne ya kula njama, kughushi na kuibia benki hiyo sh milioni 32.

Inspekta Nkonyi alidai kuwa Juni 2009 katika Benki ya CRDB katika Tawi la Morogoro, mkoani Morogoro walijitambulisha kuwa ni Issa Singano na Michael Sarungi na walifungua akaunti Na. 01J1078287500 kwa jina la Uduzungwa Heritage Ltd huku wakijua wanadanganya.

Alidai shitaka la tatu ni la kughushi Tanzania Interbank Settlement System (TISS) yenye Kumbukumbu Na. IND/TISS/565/09 ya Juni 30, mwaka jana, kuonyesha kwamba TISS ni halisi na imetolewa na Diesel Auto Electric Services Ltd yenye akaunti Na. 01400503589 kwa ajili ya kuipatia fedha Kampuni ya Uduzungwa Heritage Ltd kupitia akaunti Na. 01J1078287500 katika Benki ya CRDB Tawi la Morogoro kwa kuhamisha sh milioni 32 kwenye akaunti hiyo.

Aidha, alidai shitaka la nne ni kwa ajili ya mshitakiwa wa pili, wa tatu na wa nne ambalo ni la kusaidia kutendeka kwa kosa hilo, Juni 2009 katika Benki ya Stanibic Ltd Industrial, wakijua hati TISS ni ya kughushi na wakashindwa kuchukua hatua ya kujiridhisha kwenye mtandao wa kibenki kwamba Kampuni ya Uduzungwa ilikuwa ikiiba fedha za Benki ya Stanbic kupitia akaunti hiyo ya Udizungwa.

Aidha, washitakiwa hao walikana mashitaka yote na hakimu huyo alisema ili mshitakiwa apate dhamana ni lazima wawe na wadhamini wawili, mmoja awe ni mtumishi wa serikali, ambapo wadhamini hao watasaini bondi ya sh milioni 20 kwa kila mshitakiwa na washitakiwa wote walipata dhamana baada ya kutimiza masharti na kesi hiyo itatajwa Aprili 14, mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi,April 1 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.