Header Ads

MGOMBEA BADO ALITESA TAIFA

*MJADALA WAKE WATAWALA NEC YA CCM,MAHAKAMA YA RUFAA

Na Happiness Katabazi

SUALA la mgombea binafsi limeendelea kuwa tete, na juzi lilizua mjadala mkali katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM); na jana lilizua ubishi wa kisheria katika Mahakama ya Rufaa kwa siku ya pili mfululizo.


Habari kutoka ndani ya kikao cha NEC, zinasema juzi suala la mgombea binafsi lilileta ubishi mkubwa, huku wajumbe wengi wakisisitiza kwamba serikali lazima ifanye lolote inaloweza kulizima kabisa, ili mgombea binafsi asiruhusiwe, kwa maelezo kuwa akiruhusiwa atakuwa mwiba mkali kwa chama.

Hata hivyo, wajumbe wawili vigogo, John Malecela na Samuel Sitta waliwasihi wajumbe walegeze msimamo kwa maelezo kuwa nyakati zimebadilika, na kwamba hata wakikataa, mahakama inaweza kutoa uamuzi wasioupenda.

Kwa mujibu wa habari hizo, hatimaye wajumbe walikubaliana kwamba hatima ya suala hili ibaki mahakamani, na kwamba mahakama ikishatoa uamuzi, uheshimiwe.

Jana, mvutano wa kisheria uliendelea katika Mahakama ya Rufaa, miongoni mwa magwiji wa sheria, ambao waliitwa kutoa maoni yao kama marafiki wa mahakama kuhusu hukumu ya Mahakama Kuu iliyoruhusu mgombea binafsi nchini, mwaka jana. Magwiji hao ni wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Palamagamba Kabudi na Profesa Jwani Mwaikusa, wakishirikiana na Mkurugenzi wa Mashitaka wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (DDP), Othman Masoud.

Walikuwa wanaishauri Mahakama ya Rufaa kabla haijatoa hukumu ya rufaa iliyofunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka jana kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyoruhusu mgombea binafsi, katika kesi ya msingi iliyofunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila.

Profesa Mwaikusa alieleza jopo la majaji saba wanaosikiliza kesi hiyo kwamba lile ni suala la haki za binadamu, na kwamba mahakama, kwa mamlaka yake, haina kikomo cha kujadili haki hiyo.

Alisema Katiba ya nchi ipo kwa ajili ya kulinda haki za binadamu na kwa msingi huo haki za binadamu ni mama wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977; na kuongeza kuwa kama kuna kifungu kinavunja haki za binadamu basi kifungu hicho ni wazi kinakiuka haki za binadamu kwa sababu haki za binadamu zilianza, Katiba ikafuata.
“Kwa uamuzi ule wa Mahakama Kuu wa kubatilisha vifungu vya ibara 21(1) (c), 39(1) (c) (b) na 69(1) (b) za Katiba ya nchi, kama kuna ibara zinapingana, ibara inayopaswa kutumika ni ile inayolinda haki za binadamu.”

Kuhusu Mahakama Kuu kama ilikuwa na uwezo au la, alisema:

“Mimi nasema ilikuwa na uwezo wa kutamka ibara hizo ni batili kwani Katiba inalinda haki za binadamu na haki hizo za binadamu zilianza Katiba ikafuata hivyo haki hizo ni sheria mama.”

Jopo la majaji hao wa Mahakama ya Rufaa linaongozwa na Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani, likiwashirikisha pia Jaji Januari Msofe na Eusebio Munuo, Natalia Kimaro, Mbarouk Mbarouk, Sauda Mjasiri na Bernard Ruhanda.

Kwa upande wake, Profesa Kabudi alisema mahakama haikumuita mahakamani hapo aseme mgombea binafsi awepo au asiwepo.

“Ila iliniita niwasaidie kujibu kisheria na kikatiba kama ndani ya Katiba kuna ibara inapingana na ibara nyingine mahakama ina inauwezo wa kutamka ibara hizo ni batili.…Jibu langu ni rahisi sana mahakama za Tanzania hairuhusiwi kutamka ibara au kifungu cha sheria kinavunja kifungu kingine isipokuwa pale tu Katiba yenyewe iruhusu mahakama ama wazi wazi au kimkandomkando,” alisema Profesa Kabudi.

Alitoa mifano ya maamuzi yaliyotolewa kwenye kesi mbalimbali katika nchi ya Afrika Kusini, alisema katika nchini nyingine, katiba zinazipa mamlaka mahakama zao uwezo wa kutamka kifungu au ibara moja inavunja ibara nyingine, kwahiyo panapotokea mgongano wa ibara kama ilivyotokea katika kesi ya mgombea binafsi iliyofunguliwa na Mtikila ni kazi ya mahakama kusoma vifungu vya sheria na ibara za katiba kwa pamoja, na kisha kutafuta uwiano, na si kutengua au kuzivunja ibara hizo.
“Ni haki ya kila mwananchi kwenda mahakamani kudai haki, akinyimwa au kupewa ni uamuzi wa mahakama. Hivyo, Mtikila alikuwa sahihi kwenda mahakamani kufungua kesi hiyo, na jukumu la kusema haki yake ilivunjwa au la ni la mahakama,” alisema Profesa Kabudi.
Naye DPP wa Zanzibar, Othuman Masoud, alisema kuruhusu mgombea binafsi kutaondoa haki nyingine, mfano za haki ya wanawake kuruhusiwa kushiriki kwenye ngazi za maamuzi kama ilivyotamkwa kwenye ibara 66(b) ya Katiba na kuongeza kuwa Katiba imeweka utaratibu wa jinsi vyama vya siasa vitakavyofanya kazi yake, lakini haijasema kama endapo mgombea binafsi ataruhusiwa atafuata utaratibu upi.

Jaji Mkuu Ramadhani baada ya kusikiliza ushauri wa wanataaluma hao wa sheria, alisema anaahirisha usikilizaji wa rufaa hiyo, na kwamba mahakama itatoa tarehe ya siku ya kutoa hukumu hiyo. Rufaa hiyo ilianza kusikilizwa jana na kuhudhuriwa na umati mkubwa watu wa kada mbalimbali.

Juzi Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, wakati akiwasilisha hoja zake, alidai kwamba hapa nchini hakuna mahakama yenye mamlaka ya kutengua ibara za katiba, akaiomba mahakama hiyo itengue hukumu ya Mahakama Kuu. Mawakili wa Mjibu Rufaa, Richard Rweyongeza na Mpare Mpoki, walisisitiza kwamba hukumu ya mahakama kuu ilikuwa sahihi, wakaiomba Mahakama ya Rufaa itupilie mbali rufaa hiyo .

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Aprili 10 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.