Header Ads

SHAHIDI KESI YA EPA AUGUA GHAFLA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana ilishindwa kuanza kusilikiza ushahidi katika kesi ya wizi wa sh bilioni 6 katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu, inayomkabili Johnson Lukaza na nduguye Mwesigwa Lukaza kutokana na shahidi kuugua ghafla.


Wakili Mwandamizi wa Serikali, Fredrick Manyanda, alidai mbele ya jopo la mahakimu wakazi, Phofily Lyimo, Edson Mkasimongwa na Salome Mwandu, kuwa wasingeweza kuendelea na kesi hiyo kwa kuwa shahidi, Mary Kiwia, waliyekuwa wamemuandaa ameugua ghafla.

“Tunaomba kesi iahirishwe kusikilizwa kwa sababu leo shahidi tuliyekuwa tumemuandaa ameugua ghafla na tulikuwa hatujaandaa shahidi mwingine” alidai Wakili Manyanda.

Hakimu Mkazi Lyimo alikubaliana na ombi hilo na akaiahirisha kesi iyo hadi leo ambapo shahidi wa upande wa mashitaka anatarajiwa kutoa ushahidi wake.

Hii ni mara ya pili kwa shahidi huyo kuugua pindi inapofika wakati wa kutakiwa kupanda kizimbani kutoa ushahidi wake.

Mara ya kwanza ilikuwa Juni 8 mwaka jana, alipofika mahakamani hapo wakati akisubiri kupanda kizimbani kutoa ushahidi wake aliugua ghafla na hivyo kufanya mahakama kuahirisha usikilizwaji wa shauri hilo.

Mbali na Johnson, mshitakiwa mwingine ni Mwesigwa Lukaza ambapo wote kwa pamoja wanatetewa na wakili wa kujitegemea Alex Mgongolwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne Aprili 20 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.