Header Ads

'UTOAJI FEDHA EPA ULIKUWA SAHIHI'

Na Happiness Katabazi

MENEJA wa Akaunti ya Fedha za Nje katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Steven Mwakalukwa (55) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam kuwa benki hiyo iliidhinisha Kampuni ya Kenerl Ltd inayomilikiwa na Johnson Lukaza na nduguye Mweisigwa Lukaza ilipwe deni la sh bilioni sita kwa kuwa ombi lake lilikidhi matakwa ya kisheria na lilipita kwenye mlolongo sahihi.


Mwakalukwa alieleza hayo jana wakati akihojiwa na wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa, mbele ya jopo la mahakimu wakazi, Prophil Lyimo, Edson Mkasimongwa na Salome Mwandu, alipokuwa akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo.

Meneja huyo ambaye ni shahidi wa pili wa upande wa Jamhuri, alidai mwaka 2005 alikuwa akifanya kazi katika Idara ya Fedha za Nje BoT na majukumu yake yalikuwa ni kupokea majalada yanayoingia katika Idara ya Malipo na kwamba ombi la Kenneld Ltd alihusika na malipo yake kwa njia ya ujumbe wa kibenki.

Alidai kampuni hiyo ilikuwa ikitaka ilipwe deni la Kampuni ya Marubeni ya Japan na kuongeza kuwa Desemba mosi mwaka 2005 aliyekuwa Gavana marehemu Daudi Balali aliidhinisha deni hilo lilipwe na Desemba 8 mwaka huo, BoT iliandikia barua kampuni hiyo kuijulisha kwamba tayari imeishawaingizia kiasi hicho cha fedha kwenye akaunti ya kampuni hiyo yenye Na. 0220031004 iliyopo kwenye Benki ya Euro Africa, ambayo kwa sasa inatambulika kama Bank of Africa (BOA).

“BoT hailipi deni kiholela, hivyo ombi la kulipwa deni liliwasilishwa ofisini kwetu na kampuni ya washitakiwa, lilipita kweye idara ya madeni kisha likafikishwa kwa gavana na gavana akaidhinisha,” alieleza. Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa leo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Aprili 22 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.