Header Ads

WAZEE EAC WAITEKA MAHAKAMA KUU DAR

Na Happiness Katabazi

WAZEE wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jana walizusha tafrani katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, muda mfupi baada ya Jaji Njengafibili Mwaikugile kutoa maelekezo ya kuwataka waende wakatafakari upya na kumletea taarifa sahihi zitakazomwezesha kufikia uamuzi wa kutoa haki katika shauri lao.


Wazee hao ambao wanakadiriwa kufikia zaidi ya 100, walizingira viwanja vya Mahakama Kuu kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa sita mchana, hali iliyosababisha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), wakiwa kwenye gari aina ya Defender, yenye namba za usajili T220 AMV kuwasili katika viwanja hivyo na kuwatawanya wazee hao.

Tanzania Daima Jumatano, ilishuhudia askari hao wakiwa wamebeba silaha nzito na kuvalia mabomu ya machozi kiunoni, tayari kuwakabili wazee hao ambao walikuwa wakali mithili ya mbogo.

“Leo hatuondoki hapa, tunalala hata kama ni mwezi mzima. Tumechoka kupigwa tarehe, leo tuliambiwa ni siku ya hukumu, lakini tumejikuta tunapangiwa tarehe nyingine kuja kuchukua mafao yetu. Kibaya zaidi jaji anatuambia mambo mengine tusiyoyataka. Leo hatuondoki hapa,” alisikika akisema mzee mmoja wa makamo ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja kutokana na purukushani iliyokuwepo.

Hata hivyo Polisi na FFU walipofika, hawakutumia nguvu kuwatawanya badala yake iliwachukua wawakilishi wao saba na kuondoka nao hadi katika ofisi ya Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa mahojiano.

Wakati wawakilishi wao saba wakichukuliwa na polisi hadi Ofisi ya Kanda Maalum ya Dar es Salaam, wazee wengine zaidi ya 100 waliandamana kujua hatma ya wenzao ambao hata hivyo waliachiwa baada ya kuhojiwa kwa muda.

Awali Jaji Mwaikugile anayesikiliza kesi hiyo, alikataa ombi la wazee hao kutaka mahakama iwatambue wawakilishi wapya katika kukazia hukumu ya kesi ya madai Na.95/2010 na badala yake aliwataka mawakili wao wa zamani, Adronicus Byamungu na Rukwalo na wakili wao mpya, Pius Chabruma, kukaa pamoja ili waondoe hati ya kusudio la kukata rufaa na kuwataka kurudi mahakamani hapo Aprili 30.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na vurugu hizo, Msajili wa Mahakama Kuu Wilaya ya Dar es Salaam, Lameck Mlacha, alikiri kutokea kwa vurugu hizo za wazee.

“Kama mlivyoshuhudia, tafrani iliyokuwa ikiendelea katika viwanja vya mahakama yetu. Hao wazee wameleta rabsha na walitaka kuingia ndani ya mahakama ili wawashambulie wenzao saba kwa madai kwamba wamewasiliti; lakini polisi wamefanikiwa kuwadhiti na tunapenda kuutangazia umma kwamba rabsha hizo hazijaleta uharibifu katika ofisi za mahakama,” alisema Mlacha.

Kwa upande wake, Kamanda Kova, naye alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kuongeza kwamba wamezungumza na wazee hao na kufikia uamuzi wa kusitisha tafrani hiyo na kutekeleza maagizo ya mahakama.

“Kinachoonekana katika tafrani hiyo ni wazee hao kugawanyika katika makundi mawili ambayo hayaaminiani na kundi jingine lilifahamu jana kesi yao ilikuja kwa ajili ya kutolewa hukumu wakati si kweli kesi hiyo ilikuja kwa ajili kusikiliza hoja,” alisema Kova.

Baada ya kuzungumza na waandishi wa habari, Kova alilazimika kutoka ndani ya ofisi yake na kusimama katika uwanja wa ofisi na kuanza kuwahutubia wazee hao kilichotokea mahakamani hapo jana.

Wazee hao walimwelewa na ilipofika majira ya saa 9:21 alasiri, walitawanyika huku wengine wakimpongeza Kova kwa kuwapa ufafanuzi bila kutumia nguvu.

Awali katika kesi ya madai 95/2003 iliyofunguliwa na wazee 31,831 hao dhidi ya serikali, Mahakama Kuu ilitoa hukumu ya maridhiano na ikaamuru wazee hao walipwe sh bilioni 117 lakini baadaye waliwasilisha ombi la mapitio ya hukumu hiyo na Jaji Katherine Oriyo alilitupa ombi hilo.

Baada ya ombi hilo kutupwa, wazee hao waliwasilisha hati ya kutaka kukata rufaa, lakini waligawanyika baada ya wengine kutaka kukazia hukumu ya awali.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano Aprili 14 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.