Header Ads

GAZETI LA MTANZANIA LATAKIWA LIMPE MIL.45 ALIYESANIFU JENGO LA SOKO LA KARIAKOO

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemuamuru Mhariri wa gazeti la Mtanzania na Kampuni ya Habari Corporation kumlipa fidia ya jumla ya sh milioni 45 Msanifu wa Majengo ambaye ndiye alichora ramani ya jengo la Soko la Kariakoo Dar es Salaam,Beda Jonathan Amuli kwa kumkashfu kuwa hana taaluma ya usanifu majengo.


Wadaiwa katika kesi hiyo ya madai kashfa Na 29/2008 iliyofunguliwa na Amuli dhidi ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Kariako Kuboja Ng’ungu,Mwariri wa Gazeti la Mtanzania na Kampuni ya Habari Coporation inayochapisha magazeti la Bingwa,The African, Rai,Dimba na Mtanzania ambapo mlalamikaji huyo alikuwa anaomba alipwe sh bilioni tano kama fidia ya kuchafuliwa jina lake kutokana na habari iliyochapishwa na gazeti hilo la Na 4214 la Novemba 23 mwaka 2007 iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho;

“Soko kuu la Kariakoo lipo katikati ya eneo la Kariakoo Dar es Salaam, Kitalu namba 32,limepakana katika maungano ya mitaa mine ya Nyamwezi,Mkunguni, Swahili, Sikuuu na Tandamti. Meneja Mkuu wa Soko ,Kuboja N’ungu anasema mchoro wa jengo hili ulibuniwa na Mtanzania ambaye hakwenda shule kwa ajili ya usanifu wa majengo (Local Architect)anaishi maeneo ya Kigamboni, Dar es Salaam”.

Hukumu hiyo imetolewa hivi karibuni na Jaji Profesa Ibrahim Juma ambapo alisema baada ya kupitia utetezi na vielelezo viliwasilishwa na pande zote mbili amefikia uamuzi wa kukubaliana na hoja za mlalamikaji(Amuli) kwamba habari hiyo ilimshushia heshima, haina ukweli wowote na ili mletea madhara mbele ya jamii kwani habari hiyo ilikuwa ni ya uongo kwani mlalamikaji huyo ni kweli ana taaluma ya usanifu wa majengo na shahada ya usanifu majengo aliipata katika Taasisi ya Teknolojia nchini Israel mwaka 1964.

Jaji Juma alisema mlalamikaji huyo Amuli alifaulu kwa kiwango cha juu kabisa kozi yake hiyo na kwamba ndiye alikuwa Mwafrika wa kwanza toka Tanganyika kupata shahada hiyo ya usanifu majengo na kwamba baada ya kuitimu kozi hiyo msanifu huyo alijiunga na kampuni Zevet International Architect and Engineers of Tel Aviv na kuwa kampuni hiyo ndiyo ilikuwa imeshinda tenda ya kuchora mchoro wa ujenzi wa Hoteli ya Kilamanjaro ambayo sasa inatambulika kwa jina la Kempinski.

Jaji huyo alisema kampuni ya Usanifu Majengo ya ZEVET ilimtuma mlalamikaji (Amuli) jijini Dar es Salaam kama mwakilishi wake ambapo aliweza kusimamia ujenzi wa jengo la iliyokuwa Hoteli ya Kilimanjaro ambapo kampuni ilifanyakazi na mlalamikaji kwa miaka mitano na kisha mlalamikaji alimia katika kampuni nyingine ya usanifu majengo ya BJ AMULI na kwamba moja ya kazi kubwa kampuni hiyo iliyopata ni mradi wa ujenzi wa jengo la Soko la Kariakoo kati ya mwaka 1972-1974 na kisha mlalamikaji ndiye pia aliyechora mchoro wa jengo la Chuo cha Usimamizi wa Fedha(IFM) na Chuo cha Mafunzo cha Benki ya Taifa ya Biashara(NBC) ambacho kwa sasa ndicho Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani Iringa.

“Kwa kazi hizo za usanifu majengo ambazo zilitolewa mahakamani hapa na mdaiwa kama vielelezo kuwa yeye ni msomi wa fani ya usanifu majengo na miongoni mwa kazi alizowahi kuzifanya kupitia taaluma yake ni hizo hapo juu na upande wa wadaiwa wameshindwa kuthibitisha madai ya mlalamikaji ,mahakama hii pia imengalia haki itendeke kwa pande zote mbili licha ni kweli habari hiyo ni kweli ilichapwa na mdaiwa wa pili na wa tatu na likasambazwa mikoa yote ya Tanzania na ni kweli ilimletea usumbufu mlalamikaji…mahakama hii inatoa hukumu ya kukubalina na madai ya mlalamikaji na ina mwamuru mdaiwa wa kwanza na wapili kumlipa fidia ya jumla ya milioni 45 pamoja na riba mlalamikaji kuanzia siku ambayo hukumu hii imesomwa badala ya bilioni tano .”alisema Jaji Profesa Juma.Hukumu imetolewa Mei 5 mwaka 2011.

Chanzo:katabazihappy.blogspot.com

No comments:

Powered by Blogger.